NENDA NA WAKATI NA MAJIRA




(Mhubiri 3:3) “Kwa kila jambo kuna majira yake na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu”. Biblia inaposema kuwa kila jambo lina majira yake maana yake ni kwamba kila jambo lina muda wake maalumu wa kulifanya, na kila lengo(kusudi)  lina wakati wake maalumu wa kulitekeleza. Kosa wanalolifanya watu wengi ni kwenda kichwakichwa bila kupambanua nyakati na majira.
Kila mtu ni vema afahamu kuwa muda huwa unakuja na matakwa yake, yaani muda huwa unakuja na vitu ambavyo unavitaka vifanyike ndani ya muda huo na ndio maana ukijaribu kushindana na muda utajikuta umekwama si kimwili hata kiroho pia, ni muhimu kupambanua nini ambacho muda unakitaka ili usije ukajikuta unapanda mbegu wakati wa kuvuna, ili usijikute unang’oa wakati wa kupanda, ili usije ukajikuta uko masomoni wakati wa kuolewa au kuoa.
Kutopambanua nyakati na majira ni kosa ambalo watu wengi hulifanya ndio maana malengo ya watu wengi yamekuwa hayatimii.
(Hagai 1:2-8) Wana wa Israeli walijikuta wakipanda mbegu nyingi katika wakati ambao walitakiwa kuijenga nyumba ya Bwana na mwishowe walijikuta malengo yao hayatimii kwa kuwa walitazamia vingi vikaja vichache yaani mambo yalitokea kinyume na matarajo yao kwa kuwa hawakupambanua kitu walichotakiwa kukifanya katika wakati huo, wakati wa kujenga wao walijikuta wakipanda mbegu.

Faida chache za kupambanua nyakati na majira
a).Inakusaidia kutopoteza nguvu nyingi kwenye jambo lisilo na faida.
(Hagai  1:6) “Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo”. Hawa watu walitumia nguvu nyingi sana kupanda mbegu lakini wakavuna kidogo kwa kuwa hawakupambanua kipi walitakiwa kukifanya kwa wakati huo.

(b).Inakusaidia kufanya jambo sahihi kwa wakati sahihi(right thing on the right time).
Sikuzote jambo sahihi likifanyika kwenye wakati usio sahihi huwa linaoneka kuwa si jambo sahihi na hiki ndicho kilichomponza Musa hata akaihama nchi ya Misri, alitaka kuanza kazi ya uamuzi juu ya wana wa Israeli kabla ya muda ambao Mungu aliukusudia mwishowe aliulizwa “ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu na mwamuzi juu yetu? (Kutoka 2:11-14).
Laiti kama wana wa Israeli wangepambanua ambacho kinawapasa kukifanya kulingana na wakati ingewasaidia kufanya jambo sahihi kwa wakati sahihi.

Chapisha Maoni

0 Maoni