NAMNA YA KUSHIGHULIKA NA TABIA ZA WATOTO ILI UWE NA WATOTO WENYE UTII



                                                                     Mwl. Faraja Gasto

Utangulizi
Katika dunia tunayoishi kumesikika vilio kutoka kwa wazazi wakilia kwa sababu watoto wamekuwa wakaidi, watukutu, hawaambiliki, hawashauriki n.k. Wakati hayo yakiendelea kutokea, wazazi wamefanya jitihada mbalimbali ili kuwafanya watoto wao wawe watii, wazazi wengine wamediliki kwenda mbali zaidi kwa kuwachoma vidole watoto wao, kuwaua n.k kwa kuwa watotop hawashikiki.
Nakumbuka wakati Fulani nilishuhudia mama mmoja akimpiga mtoto wake, alipoona haitoshi akachukua majivu kutoka kwenye jiko akawa anampaka mtoto wake huku akimfinya, mtoto Yule alilia kwa uchungu sana, lakini lengo la Yule mama lilikuwa si kumuumiza mtoto wake bali ni kuona kwamba labda anaweza akabadilika baada ya kumpiga.
Wazazi wengi wamekuwa wakihangaika sana kubadili tabia za watoto wao bila mafanikio na hatimaye watoto wengi wamezidi kuharibika.
Biblia inasema “watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa” (Hosea 4:6a) wazazi wengi kwa kukosa maarifa wamejikuta wakiharibikiwa watoto. Neno la Mungu lina majibu ya kutosha juu ya namna ya kubadilisha tabia za watoto.


KWA NINI WATOTO WENGI WANA TABIA MBOVU
1.Kwa kuwa tuko katika nyakati za mwisho (2 Timotheo 3:1-2)
Dalili mojawapo ya nyakati za mwisho ni suala la watoto kutotii wazazi wao, unapoona watoto wanapoteza utii kwa wazazi basi ni vema ujue tuko katika nyakati za mwisho. 

2.Mazingira waliyokulia
Kama mtoto amekulia kwenye mazingira ya watu wenye tabia mbovu ni rahisi sana na yeye akajikuta ana tabia mbovu ndio maana maandiko yanasema mlee mtoto katika njia impasayo naye hataiacha hata atakapokuwa mzee (Mithali 22:6)

3.Wengine wamerithi tabia
Naamini umeshawahi kusikia wazazi au watu wakisema “yaani huyu mtoto amefanana kila kitu na marehemu babu yake, bibi yake, shangazi yake, mjomba wake n.k” maana yake ni kwamba kuna uwezekano mtoto akajikuta amerithi tabia Fulani, kwa kuwa hili ni suala linatembea kwa kufuata mfumo wa damu, ukisoma Biblia utaona kuna tabia ambazo alikuwa nazo Ibrahimu tabia hizo zikaonekana kwa Isaka na kwa Mjukuu wa Ibrahimu aitwaye Yakobo.

JINSI YA KUSHUGHULIKIA TABIA ZA WATOTO ILI WAWE NA TABIA NJEMA

1.Omba Mungu azibue masikio yao
(Isaya 50:5) “Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikiurudi nyuma”
Nadhani umeshawahi kuona mzazi akimvuta masikio mtoto wake halafu wakati huohuo unasikia mzazi akisema “wewe mtoto mbona una masikio magumu”
Sina uhakika kama wazazi wengi huwa wanajua wanachokisema, na kama wangekuwa wanajua shida iko kwenye masikio basi wangeshughulika na masikio ya watoto wao na watoto wangepona.
Ukisoma hilo andiko hapo juu utaona kuwa Mungu alipomzibua sikio Nabii Isaya kuna mambo yalitokea (a) ukaidi uliondoka kwenye moyo wake (b) hakurudia kufanya mambo ambayo si mazuri, mambo aliyoyafabnya awali ndio maana anaseam wala sikurudi nyuma tena.
Kwa hiyo masikio yanapozibuliwa ghafla utashangaa mtoto anaanza kuwa wa tofauti, tabia za watoto zinabadilika.

2.Omba Mungu ageuze moyo wa mtoto uuelekee moyo wako
TAHADHARI: Unapoomba namna hiyo hakikisha moyo wako ni mnyofu kwa Mungu kwa kuwa kama moyo wako si mnyofu kwa Bwana basi hata mtoto atajikuta akiwa si mnyofu kwa Bwana
 Kuna wakati Yoshua aliwaambia watu “mimi na nyumba yangu nitamtumikia Bwana” (Yoshua 24:14-15)  maana yake ni kwamba Yoshua alikuwa na uhakika kuwa mioyo ya watu wa nyumba yake iko pamoja na yeye ndio maana alipata ujasiri wa kuwaambai watu kuwa mimi na nyumba yangu nitamtumikia Bwana.
(Malaki 4:5-6)
Ninachotaka uone kwenye andiko hilo ni kwamba moyo wa mtoto unaweza ukamuelekea mzazi na pia moyo wa mtoto unaweza ukaenda kinyume na mzazi wake, kinachotokea pale moyo wa mtoto unapoenda kinyume na mzazi wake ni kwamba mtoto huyo hawezi kuwa mtii.

3.Mlee katika njia inayompasa
(Mithali 22:6) “mlee mtoto katika njia impasayo)
Biblia inaposema njia impasayo maana yake ni kwamba kila mtoto huwa ana aina yake ya malezi inayomfaa, kwa hiyo unapokosea katika aina ya malezi inayomfaa mtoto maana yake ni kwamba utajikuta umemfanya mtoto aharibikie mikononi mwako kwa kuwa wewe ndiye umefanya makosa.
Kumlea mtoto kunahitaji hekima na maelekezo ya Mungu aliyekupa huyo mtoto, watu wengi wanakosea katika hili baada ya kupata watoto basi wanamuachia mfanyakazi wa ndani(houseboys/girls) ndiye ahusike kulea mtoto.
MFANO: Wakati Mfalme Herode alipokuwa amekusudia kumuuua Yesu, Mungu alitoa maelekezo kuhusu mahali ambapo Yusufu na Mariamu walitakiwa kwenda kuishi ili mtoto awe salama, baada ya kupata malekezo ya Mungu ndipo Yusufu na Mariamu wakakimbilia Misri mpaka walipopata maelekezo mengine ndipo waliporudi tena nchini wao (Mathayo 2:13).
àNi vema ujue kuwa Mungu anaweza kukuongoza katika kumlea mtoto wako katika njia inayompasa.

Chapisha Maoni

0 Maoni