Sisi wanadamu tunapofunika vitu huwa tunakusudia kutunza vitu hivyo dhidi ya uharibifu, kuzuia vitu fulani visiingie ndani ya kile tulichofunika nakadhalika.
Pia katika ulimwengu wa roho kuna vifuniko vya aina mbalimbali, Mungu anavyo vifuniko vyake na shetani naye anavyo vifuniko vyake kwa ajili ya kufunika watu, vitu nakadhalika.
BAADHI YA AINA ZA VIFUNIKO VYA KIROHO
1. NGUVU
Nguvu za Mungu au nguvu za giza zinaweza kutumika kama kifuniko cha kufunika mtu, kitu nakadhalika kwa ajili ya makusudi mbalimbali.
(Luka 1:35)
Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na NGUVU ZAKE ALIYE JUU ZITAKUFUNIKA kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.
Mungu alipotaka bikira Mariamu azae kitakatifu alimfunika kwa nguvu zake. Kinyume chake ni kwamba shetani naye akitaka usizae au usimzalie Mungu matunda anaweza kufunika kwa nguvu zake maana shetani huiga mitindo mbalimbali ambayo Mungu huitumia.
2. ROHO
Roho Mtakatifu au roho za kuzimu zinaweza kumfunika mtu kwa ajili ya makusudi mbalimbali ya Mungu au ya shetani kutegemeana na roho iliyofunika.
(Isaya 30:1 SUV)
Biblia inasema kuwa watu wanaweza kujifunika kwa roho za kuzimu au kwa Roho Mtakatifu, kwa hiyo roho fulani inaweza kuwa kifuniko.
3. MAWE YA KIROHO AU MAWE YA JINSI YA ROHONI
(Ezekieli 28:13)
Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; KILA JIWE LA THAMANI LILIKUWA KIFUNIKO CHAKO, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari.
4. HAKI
(Waefeso 6:14)(Ufunuo wa Yohana 9:9)(Ufunuo wa Yohana 9:14)
DIRII ni kifaa kilichokuwa kinavaliwa vifuani mwa maaskari ili kufunika vifua vyao kwa ajili ya kuzuia mishale au upinde wa maadui usiwadhuru.
Biblia inasema tuvae dirii ya haki vifuani, kwa hiyo HAKI NI KIFUNIKO CHA KIROHO CHA KUJIKINGA NA MAMBO MBALIMBALI KUTOKA KWA SHETANI.
MADHARA YA VIFUNIKO VYA GIZA
1. Vifuniko vya giza vinaweza kukuzuia usione vizuri (Ayubu 22:14)(Isaya 22:8)(2 Wakorintho 3:14)
2. Vifuniko vya giza vinaweza kukuzuia usimwelewe Mungu pia usielewe maandiko (2 Wakorintho 3:14-16)
Biblia inasema YESU aliwafunulia wanafunzi wake akili zao ili waweze kuelewa maandiko (Luka 24:45) maana yake ni kwamba kuna kitu kilikuwa kimefunika akili zao na hawakuelewa maandiko, Yesu akawafunulia akili zao (akaondoa mfuniko uliokuwa umefunika akili zao).
3. Vifuniko vya giza vinaweza kusababisha usikumbukwe wakati unaotakiwa kukumbukwa, Yusufu alimtendea mtu fulani mema na akamwambia ukipata mema unikumbuke lakini yule alimsahau kabisa Yusufu lakini Mungu aliingilia kati yule mtu akamkumbuka Yusufu (Mwanzo 40:12-14, 23) (Mwanzo 41:9-14).
4. Vifuniko vya giza vinaweza kuzuia usitoke ulipo kiroho, kiuchumi nakadhalika, vifuniko vya giza vinazuia mpenyo, vinaweka ugumu ili usitoke hapo nakadhalika.
JAMBO LA KUFANYA
Amuru kwa jina la Yesu ikiwa kuna kifuniko cha giza kimefunika maisha yako KIONDOKE.

1 Maoni
Ameni
JibuFuta