HANA: FUNDISHO KUHUSU MAOMBI


 (1 Samwel 1:1-20)

UTANGULIZI

Habari ya Penina na Hana inatoa picha ya makundi mawili ya watu

1. Wenye nacho (wenye kitu).

2. Wasio nacho (Wasio na kitu).

Hana alidharauliwa kwa kuwa HAKUWA NA MTOTO, Penina alimsumbua sana Hana kwa sababu kuna kitu Penina alikuwa nacho na Hana hakuwa nacho.

Kilichomsaidia Hana kupata alichokuwa anataka ni KUCHUKIA ILE HALI YA MANYANYASO NA MASIMANGO YA PENINA.

MAMBO TUNAYOJIFUNZA KUTOKA KWA HANA NI HAYA YAFUATAYO

1. Ili uweze kuomba kwa mzigo na upate majibu ya maombi yako LAZIMA KWANZA UCHUKIE HALI FULANI (hali ya kudhihakiwa, kusemwa vibaya, watu kukuchukilia hauwezi nakadhalika).

Hana alichukia sana yale masimango ya Penina, ule uchungu aliokuwa nao rohoni mwake ulimfanya aombe kwa mzigo sana mbele za Mungu mpaka Kuhani akadhani Hana amelewa (1 Samweli 1:10).

Wewe ndio unajua hali zinazokusumbua, usijifananishe na Penina (usijifananishe na wale ambao Mungu ameshajibu maombi yao) wewe unapaswa kuomba kwa mzigo mpaka yale unayotamani yatokee kwako uyaone yakitendeka.

2. Hana hakupigana na Penina, Hana hakuhangaika kumnyamazisha Penina bali Hana alimpa Mungu nafasi ya kumnyamazisha Penina.

Kumuomba Mungu ni kumpa Mungu nafasi ya kuwanyamazisha maadui au watesi wetu, hakuna haja ya kupigana na maadui kwa nguvu za kimwili, hakuna haja ya kujibishana na maadui zetu SISI TUNAPASWA KUMUOMBA MUNGU, MAJIBU YA MUNGU YATAWANYAMAZISHA ADUI ZETU.

Baada ya Mungu kujibu maombi ya Hana, hatuoni tena masimango na kelele za Penina zikiendelea, majibu ya Mungu yaliufunga mdomo wa Penina.

3. Wakati mwingine kuna sauti huwa zinainuka au kuna watu huwa wanainuka kukuvunja moyo ili uache kuomba Mungu, ukiacha kuomba maana yake ni kwamba unazidi kuwapa nguvu zaidi adui zako kukuinukia HANA HAKUKUBALI KUACHA KUOMBA MAANA ALIJUA AKIACHA KUOMBA HAKUNA MAHALI ATAPATA MSAADA, PENINA ATAZIDI KUMDHARAU.

(1 Samweli 1:13-15) Kuhani Eli alidhani Hana amelewa, akamwambia acha pombe, utalewa hata lini? Ndipo Hana akajibu kuwa mimi sijalewa nina ombi langu kwa Mungu.

Jambo hilo likufundishe kuwa CHOCHOTE KINACHOINUKA KUKUZIA USIOMBE, USIKIPE NAFASI KWA KUWA KUTOKUOMBA NI SAWA NA KUMPA NAFASI ADUI AZIDI KUKUSUMBUA.

Hana angeiacha kuomba unadhani angepataje mtoto? Kama asingepata mtoto unadhani angekaa kwa amani kwenye ndoa yake? 

Hana angeacha kuomba angekuwa amempa nafasi Penina ya kuzidi kumshambulia zaidi kwa maneno, yamkini angekufa kwa Pressure, stress nakadhalika kwa kuwa Biblia inasema maneno ya Penina yalisababisha Hana akashindwa kula chakula (soma 1 Samweli 1:7).

4. Apandaye kwa machozi atavuna kwa kelele za furaha (Zaburi 126:5)

Penina alimsumbua sana Hana, Hana alilia sana akashindwa kula (Soma 1 Samweli 1:7)

Lakini Hana aliamua kwenda kumwaga machozi yake mbele za Mungu (soma 1 Samweli 1:10), aliacha kujiliza mbele ya Penina alimua kwenda kulia mbele za Mungu hatimaye Mungu alijibu maombi yake.

Hilo likufundishe kuwa acha kulia lia mbele ya adui zako, nenda kalie mbele za Mungu kwa maombi, wapandao kwa machozi watavuna kwa kelele za furaha (Zaburi 126:5)

5. Zingatia sana msukumo au wazo ambalo Mungu analiweka moyoni mwako wakati unaomba.

(1 Samweli 1:10-11) Wakati Hana anamuomba Mungu alipata wazo au msukumo ndani yake wa kuweka nadhiri kwamba Mungu akimpa mtoto atamtoa huyo mtoto kwa Mungu.

Kuna wakati unapokuwa unaomba Mungu anaweza kuweka wazo au msukumo ndani yako wa kutoa sadaka kanisani, au kumpa mtu fulani sadaka au kitu, au ukapata msukumo wa kufanya jambo fulani HAKIKISHA UNAZINGATIA SANA KILE AMBACHO ROHO WA MUNGU ANAKUGUSA UFANYE.

Ukifanya hivyo utapokea majibu ya kile ambacho unamuomba Mungu.

6. Imani bila matendo imekufa, kuna wakati baada ya kumuomba Mungu lazima ufanye matendo ya imani.

Kwa mfano Hana aliomba Mungu ampe mtoto lakini Mungu asingeweza kuja kumpa Hana mimba, Biblia inasema baada ya maombi Hana alikutana kimwili na mumewe ndipo akapata mimba (soma 1 Samweli 1:19-20).

Kwa mfano unaomba Mungu abariki kazi za mikono yako, lazima uwe na kitu ambacho utaanza kufanya ili Mungu abariki hapo, huwezi kuomba Mungu abariki kazi za mikono yako wakati haufanyi chochote.

Kuna wakati unapaswa kufanya matendo ya imani ili uone matokeo ya maombi yako.

7. Wakati ulipowadia Hana alijibiwa maombi (soma 1 Samweli 1:20)

Tunachojifunza ni kwamba ni muhimu kujifunza kumsubiri Mungu ajibu sisi kazi yetu ni kuomba, mwenye kazi ya kujibu ni Mungu na Mungu hujibu kwa wakati fulani.




Chapisha Maoni

0 Maoni