(1 Wakorintho 6:19)
Biblia inasema miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu anayekaa ndani yetu, miili sio mali yetu wenyewe.
Kila mmoja ana wajibu wa kutunza mwili aliopewa maana miili sio mali yetu ni mali ya Mungu, ametupa miili kwa ajili ya utukufu wake.
Kuharibu mwili wako ni jambo baya, linamchukiza Mungu.
JINSI WATU WANAVYOHARIBU MIILI YAO
1. Kuondoa uhalisia wa miili yao kwa kujibadili rangi ya ngozi, maumbile nakadhalika.
2. Kuchanja chale za kimaagano, kiibada na kuweka alama mbalimbali kwenye mwili (Walawi 19:28).
3. Uvutaji wa sigara, ulevi na yanayofanana na hayo.
BAADHI YA SABABU KWA NINI TUTUNZE MIILI YETU
1. Miili ni Mali ya Mungu sio mali yetu (1 Wakorintho 6:19).
2. Roho yako inategemea sana mwili wako, roho yako ikishindwa kuutumia huo mwili itaondoka ndani ya mwili huo na wewe utakufa (Yakobo 2:26a).
3. Huwezi kutimiza malengo bila mwili, huwezi kumtumikia Mungu bila mwili nakadhalika, maisha yako kwa ujumla yanauhitaji mwili wako.
4. Miili yetu ni viungo vya Kristo (1 Wakorintho 6:15).
BAADHI YA NJIA ZA KUTUNZA MWILI
1. Usafi (Waefeso 5:25-27)
Kanisa ni mwili wa Kristo, Kristo anautunza mwili wake kwa kuusafisha ili mwili ukae katika hali nzuri. Kuusafisha ni kuhakikisha unaondoa kitu kibaya kinachoweza kuathiri mwili.
2. Kuulisha mwili (chakula) (Waefeso 5:29)
Kanisa ni mwili wa Kristo, Yesu Kristo anautunza mwili wake kwa kuhakikisha mwili unapata chakula.
Hivyo basi na sisi tunaweza kuitunza miili yetu kwa kuhakikisha tunakula chakula, kazi mojawapo ya chakula ni kuutunza mwili.
3. Kutatua matatizo ya mwili.
Kanisa ni mwili wa Kristo, Kristo hutunza kanisa lake kwa kutatua matatizo mbalimbali ya mwili wake.
Kwa mfano Sauli alikuwa ni tishio kwa mwili wa Kristo, Yesu alichofanya ni kukutana na Sauli na kumbadilisha, mabadiliko ya Sauli yalikuwa ni suluhu au ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ya kanisa (Matendo ya Mitume :9:1-22).
Hakikisha unapata ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ya mwili wako.
4. Mazoezi ya mwili (1 Timotheo 4:8)
Yapo aina mbalimbali ya mazoezi, yapo mazoezi magumu na mazoezi mepesi ambayo kila mtu anayaweza bila kujali jinsia, umri nakadhalika.
Baadhi ya aina za mazoezi ni kutembea umbali fulani, kupanda na kushuka kwenye sehemu za miinuko au milima midogo, kukimbia, kuruka kamba, kunyanyua vitu nakadhalika.
5. Pata muda wa kupumzika
Mwanzilishi wa utaratibu wa kupumzika ni Mungu mwenyewe tangu Mwanzo, alitenga siku maalumu kwa ajili ya mapumziko (SIKU YA SABATO). Hakuruhusu mtu yeyote kufanya kazi.

0 Maoni