Lazima uwe macho sana ili usijikute unatumiwa na shetani, HIZI NI NYAKATI ZA HATARI ONGEZA UMAKINI, TUKO VITANI ONGEZA UMAKINI.
Shetani anatamani kumtumia mtumishi wa Mungu yeyote kwa kuwa anajua akitenda kazi peke yake sio rahisi kufanikiwa ila akitenda kazi kwa kuwatumia watumishi wa Mungu ni rahisi sana mipango yake kufanikiwa.
SOMA MIFANO IFUATAYO
1. Aliyewatuma wapelelezi kumi na mbili kule kanaani alikuwa Mungu, aliwatuma kupitia Musa (Hesabu 13:1-3), hebu kwa sasa tuwaite MITUME.
Mitume kumi walitumiwa na shetani kuleta matatizo makubwa sana kwa wana wa Israeli, hawakujua kuwa walikuwa wanatumiwa na shetani.
Maneno yaliyotoka kwenye vinywa vyao yalisababisha matatizo makubwa sana, shetani alivitumia vinywa vyao bila wao wenyewe kufahamu kuwa wanatumiwa na shetani.
2. Shetani akamwingia Yuda (Luka 22:3)
Yuda alikuwa Mtume wa Yesu Kristo, ni mmojawapo wa wale thenashara (Mitume kumi na mbili wa Yesu Kristo) lakini kuna wakati shetani alimtumia, Yuda hakuwa anajua kama anatumiwa na shetani.
3. Unamjua au unamkumbuka NABII MZEE, kama haumjui Nabii Mzee soma habari hii 1 Wafalme 13:1-32)
Mungu alituma mtumishi wake aende Bethelu, akamwambia wakati ukiwa betheli usile chakula huko Wala usinywe maji na ukitaka kuondoka usipite njia ambayo ulipita wakati unaingia Betheli.
Yule mtu wa Mungu alipomaliza kazi aliyotumwa akaanza safari ya kurudi, lakini kuna jambo lilitokea.
Nabii Mzee alipata taarifa za ujio wa yule mtu wa Mungu, akamfuata akamwambia "malaika wa Mungu aliniambia nikurudishie ule na unywe"
Yule mtu wa Mungu akakubali kula na kunywa kule Betheli lakini ghafla neno la Mungu likamjia Nabii Mzee akamwambia yule mtu wa Mungu "Kwa kuwa umeasi neno la Mungu utakufa"
Nabii Mzee alitumiwa na shetani kumfanya yule mtumishi asitii agizo alilopewa na Mungu, hatimaye yule mtu wa Mungu alikufa.
NAHITIMISHA
1. Shetani hatakuambia nataka nikutumie ila ukimpa nafasi au ukiacha mpenyo kidogo atakutumia kufanya kazi zake hata kama wewe ni mtumishi wa Mungu.
2. Zijaribuni roho (1 Yohana 4:1) jizoeze kuzijaribu roho uone je! zimetokana na Mungu.
Si kila unabii unatoka kwa Mungu, si kila ndoto inatoka kwa Mungu, si kila muujiza unafanywa na Mungu, si kila nguvu ya kusababisha mambo fulani kufanyika au kutokea imetoka kwa Mungu, si kila ufunuo unatoka kwa Mungu, si kila maono yametoka kwa Mungu, si kila wazo linatoka kwa Mungu.
ZIJARIBUNI ROHO.

0 Maoni