VITA VYA KIROHO KATIKA NJIA

 


UTANGULIZI

Ukizitazama njia au barabara kwa macho ya damu na nyama huwezi kuona yanayofanyika kwenye njia hizo au barabara hizo, ila ukizitazama njia au barabara kwa jinsi ya rohoni utagundua kuwa kwenye barabara kwenye njia ni uwanja wa vita vya kiroho.

Soma baadhi ya shuhuda zifuatazo;

1. Siku fulani nikiwa natembea usiku nilikutana na kijana mdogo wa kiume akiwa anazoa mchanga njiani, nikamuuliza mbona unazoa mchanga unaenda kujenga au unataka mchanga wa kufanyia nini, yule kijana akanijibu kuwa "bibi amenituma huu mchanga" nikamuuliza amekutuma mchanga ili aufanyie nini, akanijibu kuwa "bibi huwa anautemea mate halafu anazungumza maneno juu ya mchanga huo".

2. Siku fulani kijana mmoja akanijia akitaka nimuombee miguu yake ilikuwa imepatwa na ganzi, nikamuuliza umekuwaje, akanijibu kuwa alikuwa anatembea njiani aliona cheni ya kuvaa shingoni akairuka kisha akaendelea na safari lakini ghafla akapatwa na ganzi na akawa hawezi kutembea.

3. Kama unaishi bara la Afrika utakuwa shahidi kuna wakati unaweza kukuta sindano kwenye njia panda, au kuna vyungu au kuna nazi ikiwa na maneno fulani nakadhalika.

Unapaswa kufahamu kwenye njia au kwenye barabara ni uwanja mmojawapo wa kufanyia vita za kiroho.

BAADHI YA MIFANO KUHUSU VITA ZA KIROHO KWENYE NJIA AU BARABARA

1. Katika njia au barabara huwekwa mitego ya aina mbalimbali kwa jinsi ya rohoni (Ayubu 28:10).

2. Sehemu mojawapo katika njia au barabara ambapo watu wanaomtumikia shetani hufanyia vita ni njia panda (Ezekieli 21:21).

Mfalme wa Babeli alienda njia panda ili kufanya uganga.

3. Hesabu 22:23-31

Malaika alisimama njiani ili amuue Balaamu.

NAMNA YA KUSHINDA VITA ZA KIROHO ZA KWENYE NJIA

1. Jizoeze kumwomba Mungu awe pamoja na wewe njiani, kila mahali utaenda awe na wewe.

Yakobo aliwaambia watu wake "tuondoke, tupande kwenda Betheli, nami nitamfanyia Mungu madhabahu huko; yeye aliyenisikia siku ya shida yangu, AKAWA PAMOJA NAMI KATIKA NJIA YOTE niliyoiendea" Mwanzo 35:3

Unapopanga kwenda mahali fulani jizoeze kumwomba Mungu awe na wewe njiani. 

2. Jizoeze kumwomba Mungu akuongoze njiani.

Mungu huwaongoza watu njiani (Mwanzo 24:48).

Ukimpa Mungu nafasi ya kukuongoza njiani, utatembea salama atakuepusha na mambo mabaya ya njiani atakuzuia kupita kwenye njia ambayo sio salama kwako.

Popote utakapokanyaga, utakanyaga na yeye na hakuna kitakachokudhuru.

3. Jizoeze kukemea pepo, roho chafu au nguvu za giza ambazo hukaa njiani kwa ajili ya makusudi mbalimbali.

Usisahau kuwa malaika wa Mungu alikaa njiani ili kuhakikisha Balaamu hafiki anakoenda (Hesabu 22:23-31).

Vivyo hivyo nguvu za giza nazo kuna wakati huwa ziko njiani au barabarani ili kutenda kazi mbalimbali, jizoeze kukemea nguvu za giza ambazo ziko kinyume na wewe ambazo ziko njiani.

HITIMISHO

Vita vya kiroho ni mojawapo ya somo muhimu unapaswa kujifunza kwa kina sana kwa kuwa tunashambuliwa na nguvu za giza kwa namna mbalimbali, lazima tumshinde shetani.

Njiani au barabarani ni mahali ambapo kila mtu hupita, hapo ni mahali ambapo watu wanaomtumikia shetani hupatumia kama uwanja wao mmojawapo wa vita.

Nimekufundisha mambo machache yakuwekee msingi wa kuwa mshindi kwenye vita vya kiroho kutokea kwenye njia au barabara.

JIFUNZE zaidi kwenye Biblia, mpe Mungu nafasi ya kukufundisha.


Chapisha Maoni

0 Maoni