UTANGULIZI
Jambo mojawapo ambalo Mtume Paulo aliliwekea mkazo ni kukaza mwendo (kujibidiisha au kuongeza bidii) Waefeso 3:12-14.
Ona ambacho Mtume Paulo anasema Wafilipi 3:12 "Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu". Mtume Paulo anasema alishikwa na Kristo na anakaza mwendo kulishika lile ambalo kwa ajili yake alishikwa na Kristo, ukisoma Biblia utaona alishikwa na Kristo Ili amtumikie.
Mtume Paulo alipowaandikia wafilipi aliwatazamisha kuwa yeye hajaridhika na utumishi alionao tu, hajaridhika na viwango alivyonavyo vya upako na neema bali anasema "anakaza mwendo" au anaongeza bidii.
Mkristo hapaswi kuwa katika hali ya kuridhika na viwango vile alivyonavyo vya kumjua Mungu au ukomavu bali anapaswa kukaza mwendo zaidi.
Kukaza mwendo ni pamoja kuongeza bidii ya kujifunza neno la Mungu, bidii ya kutoa na kujitoa, bidii ya kushuhudia ili kuwafanya watu kuwa wanafunzi wa Yesu, kujibidiisha katika kumtumikia Mungu.
MAMBO YATAKAYOKUSAIDIA KUKAZA MWENDO
1. Sahau yaliyopita (Wafilipi 3:13)
Mtume Paulo anasema Kuna mambo yalikuwa yanampa faida (Wafilipi 3:7) lakini aliamua kuachana nayo kwa ajili ya Bwana Yesu.
Vivyo hivyo wakati unaendelea na safari ya wokovu hupaswi kuzingatia mambo ya zamani, macho yako yaelekeze kwa Bwana ukijua kwa Bwana Kuna taji ya uzima.
Kuna watu wamejikuta wanarudi nyuma kwa kuyazingatia mambo ya nyuma, yamkini zamani ulikuwa unatumia njia fulani ambayo sio halali kujipatia fedha, sasa umeokoka na Mungu anakuzuia kurudia njia hiyo, epuka kuyazingatia na kuyatafakari mambo ya zamani.
Mkewe Lutu alipotazama nyuma akawa nguzo ya chumvi.
2. Yachuchumilie yaliyo mbele (Wafilipi 3:13)
Mtume Paulo anaposema anayachuchumilia yaliyo mbele anazungumzia kujikita zaidi katika utumishi ambao mwisho wake kuna tuzo (Wafilipi 3:14).
Vivyo hivyo ili mkristo ayachuchumilie yaliyo mbele lazima ajikite zaidi katika mambo yasiyomtenganisha na Kristo, mambo yanayomfanya awe karibu zaidi na Yesu Kristo ambayo ni kama vile maombi, kujifunza neno la Mungu, kuwafanya watu kuwa wanafunzi wa Yesu nakadhalika.

0 Maoni