UWINDAJI: FUNDISHO KUHUSU UINJILISTI


 

"Mwindaji mvivu hatapata anachowinda, lakini mwenye bidii atafanikiwa (Methali 12:27 BHN)"

UTANGULIZI 

Yesu na shetani wote wanaelezewa kwenye Biblia kama simba, Yesu ni simba wa kabila la Yuda (Ufunuo wa Yohana 5:5) na Shetani anaelezewa kama Simba aungurumaye anayetafuta mtu wa kummeza (1 Petro 5:8).

Ukitaka kielewa kwa haraka kwa nini Yesu aitwe Simba wa kabila la Yuda rejea alichosema mtumishi wa Mungu Yakobo siku alipowaita watoto wake wamsikilize, Yakobo alieleza kuhusu mwanaye Yuda, soma (Mwanzo 49:9-10).

Simba ana sifa nyingi sana, sifa mojawapo ya Simba ni mnyama MWINDAJI.

Shetani ni mwindaji mwenye bidii sana, amefananishwa kama simba aungurumaye akitafuta mtu ammeze (1 Petro 5:8).

Yesu mwenyewe alikuwa mwindaji.

Nimekutazamisha mambo hayo ili kuweka msingi wa kile ninachokusudia kukufundisha kuhusu uwindaji.

MAMBO BAADHI UNAYOPASWA KIFAHAMU KUHUSU UWINDAJI 

1. Mwindaji ana mitego ya aina mbalimbali kutegemeana na anachowinda, mitego ya kutega ndege ni tofauti na mitego ya kutega wanyama pia ni tofauti na mitego ya kutega samaki.

2. Mwindaji anapaswa kuwa na shabaha, mwindaji anapaswa kujua kulenga shabaha.

3. Mwindaji hufuatilia kile anachokiwinda ili ajue makazi ya anachowinda, chakula cha mnyama anayemuwinda, njia ambazo myama anayewindwa hupita. Ufuatiliaji huo humsaidia mwindaji kujua wapi ataweka mtego wake ili akamate mawindo.

4. Mwindaji lazima ajue kutega mitego na kutumia silaha za aina mbalimbali kutegemeana anachowinda.

UWINDAJI WA WATU

Sisi tuliookoka tumeagizwa kusababisha wengine waokoke, kwa hiyo ni muhimu sana kujitazama kama wawindaji ambao tuna wajibu wa kumletea Mungu mawindo ya aina mbalimbali (ambao hawajaokoka ni mawindo).

Sisi hatuwindi wanyama bali tunawinda watu ili waje kwa Yesu Kristo wamwamini, ili tuwe wawindaji wazuri lazima tujifunze mbinu za kuwinda na tuwe na bidii katika kuwinda.

BAADHI YA MBINU ZA KUTUSAIDIA KUWINDA 

1. Kuzungukazunguka huku na kule, lazima tuipeleke injili huku na kule (kwenye radio, mitandao, mitaani, mashuleni, vyuoni nakadhalika).

Shetani anapowinda huwa hakai sehemu moja, biblia inasema "shetani huzungukazunguka akitafuta mtu ammeze" (1 Petro 5:8) pia kitabu cha Ayubu kinatuthibitishia kuwa shetani huzungukazunguka huku na kule akitafuta mtu wa kushughulika naye (Ayubu 2:2).

Shetani anapozungukazunguka huku na kule huwa haendi bila lengo, huwa anakwenda kwa nia ya kuwinda (shetani ni mwindaji).

2. Kutega mitego, nimekuambia mwindaji lazima ajue kutega mitego mbalimbali ili afanikiwe kukamata mawindo.

Kwa mfano shetani alipoenda kukutana na mwanamke (Eva) alianza kumtega kwa maneno yenye kushawishi ili ale lile tunda hatimaye akala na mumewe akala wote wakawa mawindo ya shetani (Mwanzo 3:1-6).

 Mbinu hiyohiyo shetani aliitumia ili kumtega Yesu ili amanase (Mathayo 4:1-11).

Yesu mwenyewe alikuwa mwindaji, ambaye alizunguka huku na kule ili kumletea Mungu Baba mawindo. Kwa mfano alipokutana na mwanamke msamaria alianza kwa kumtega kwanza, alimwambia "nipe maji ninywe" hapo ndipo mazungumzo yalianzia hatimaye yule mwanamke alimwamini Yesu na kupitia ushuhuda wake, wengine wakamwamini Yesu (Yohana 4:7-39).

(Zaburi 91:3)(Mithali 6:5) Biblia inatuhabarisha kuwa mwindaji huwa anayo mitego yake.

Kwa mfano Yesu alipowaita wakina Petro na wengine aliwaambia "nifuateni nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu" (Mathayo 4:19).

Huwezi kuwa mvuvi kama hujui kutega mitego, vivyo hivyo huwezi kuwa mwindaji mzuri kama hujui kutega mitego.

Yesu alipokuwa duniani alifanya uwindaji, alitega watu kwa njia mbalimbali, nimekuonyesha mfano wa mwanamke msamaria jinsi Yesu alivyomtega kupitia mazungumzo hatimaye yule mwanamke aliishia kumwamini Yesu.

Nimekuonyesha mfano wa shetani alivyomtega Yesu na alivyomtega mwanamke kule kwenye bustani ya Edeni, rejea kitabu cha Mwanzo sura ya tatu msitari wa kwanza mpaka msitari wa sita.

3. Kusubiri mawindo, wakati wa kusubiri mawindo ni wakati wa kutulia na kusubiri ili anayewindwa aje mahali sahihi.

Simba anapowinda, hutulia mahali fulani akisubiri mnyama atakayepita karibu naye ili amkamate.

4. Lazima tujifunze kutumia silaha mbalimbali za kiroho ili tufanikiwe kuzitumia kwa usahihi na tulenge shabaha ili kumletea Mungu mawindo (tusababishe watu kumwamini Yesu).

Mzee Isaka alimwambia mwanaye Esau, chukua silaha zako ukawinde (Mwanzo 27:1:3). Lazima ujifunze kutumia silaha za Mungu ili umletee Mungu mawindo. 

HITIMISHO

Isaka alimwambia mwanaye Esau akawinde kisha aandae chakula kizuri ili ale halafu ambariki, Esau kwa kuwa alitamani kubarikiwa alikwenda kuwinda (Mwanzo 27:1-4).

Vivyo tunapaswa kufahamu kuwa Baba yetu aliye mbinguni anataka twende ulimwenguni kote tukamletee mawindo (tukawafanye watu kuwa wanafunzi wa Yesu - tuhubiri injili ili watu wamwamini Yesu).

Jambo la pekee ambalo Baba yetu anapenda sana kuliona, ni kuona tunamletea mawindo (tunaleta watu kwa Yesu). 

Chapisha Maoni

0 Maoni