Kwa mfano anayeuza anaweza kukuuzia kitu cha wizi au akakuuzia kitu ambacho sio halisi (not original) au akakuuzia kitu ambacho kina hitilafu (a damaged product) au akakuuzia kitu kwa bei kubwa wakati ungeweza kupata kitu hicho kwa bei ndogo kwa mtu muuzaji mwingine nakadhalika. Usipokuwa makini unaweza kujipata uko matatizoni ikiwa umenunua kitu cha wizi, unaweza kujipata umepoteza fedha bure kwa kununua kitu ambacho sio kizuri, unaweza kujipata umenunua kitu kwa bei kubwa wakati ungeweza kununua kwa muuzaji mwingine kwa bei nafuu.
BAADHI YA MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA MANUNUZI
1. Usiwe na haraka ya kununua, fanya uchunguzi wa bei ili kubaini ikiwa kile unachotaka kinaweza kupatikana kwa bei nafuu kwa muuzaji gani. Kumbuka kuwa kila muuzaji anacholenga ni kupata faida (gaining maximum profit) kwa hiyo usinunue bila kuchunguza bei za wauzaji wengine.
2. Mazungumzo wakati wa manunuzi (bargaining).
Ukweli ni kwamba kuna bidhaa ambazo bei yake imeshawekwa (fixed price) muuzaji hawezi kubadili bei lakini kuna bidhaa ambazo hazina bei maalumu, kwa muuzaji mmoja unaweza kuipata kwa bei fulani na kwa muuzaji mwingine unaweza kuipata kwa bei fulani, jizoeze kufanya mazungumzo na muuzaji kabla ya kununua.
Mazungumzo yana faida nyingi ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kupunguziwa bei (discount).
3. Omba nakala ya manunuzi (receipt) inapobidi.
Nakala ya manunuzi ambayo tumezoea kuiita risiti ni ya muhimu unaponunua kwa kuwa inaweza kukusaidia katika mazingira ya aina mbalimbali.
Kwa mfano miaka kadhaa imepita kuna wakati nilikopa fedha mahali fulani halafu niliweka kifaa changu fulani kama dhamana kwa yule mkopeshaji, wakati fulani yule mkopeshaji alikamatwa na polisi na sikufahamu chanzo cha kukamatwa kwake.
Polisi walinipigia simu ili nikatambue mali yangu, nilipofika polisi wakaniambia nitambue kifaa ambacho ni changu kati ya vitu walivyomkuta navyo yule ndugu, nilipowaonyesha kifaa fulani ni cha kwangu waliniambia tuonyeshe nakala ya manunuzi ya kifaa hicho yaani risiti, nikawaletea nakala ya manunuzi ya kile kifaa kisha nikaondoka kwa kuwa nilikuwa sijamaliza kulipa lile deni nilikiacha kile kifaa.
4. Kagua kifaa kabla haujaondoka nacho kutoka mahali uliponunua.
Nimewahi kununua bidhaa kutoka sehemu tofauti, wakati fulani nilinunua kifaa fulani kumbe kilikuwa na hitilafu (sijui kama muuzaji alijua au hakujua kama kina hitilafu) nilipokipokea nikakikagua nikabaini kina hitilafu, nilipomjulisha aliyeniuzia kuwa kifaa kina hitilafu alikubali kunibadilishia.
Kumbuka si wauzaji wote wanaweza kukubali kukubadilishia bidhaa utakaposema ina hitilafu, kwa hiyo ni vema kukagua kifaa au bidhaa wakati wa manunuzi, ikiwa umenunua sehemu nyingine na bidhaa ikaagizwa kwako ni heri kuikagua kwanza kabla hujaanza kuitumia.
5. Nunua kwa muuzaji anayeweza kuaminika.
Muuzaji anayeweza kuaminika ni pamoja na muuzaji mwenye ofisi au muuzaji aliyesajiliwa au muuzaji anayetambulika. Kununua kwa muuzaji anayetambulika kunarahisisha upatikanaji wake endapo kutatokea dharura au endapo utahitaji bidhaa ambayo umebaini ina ubora.
6. Zingatia mambo ya kisheria wakati wa manunuzi na taratibu zingine ambazo ni rasmi katika manunuzi (formal process of procurement).
Kwa mfano soma habari ya manunuzi ya Nabii Yeremia (Yeremia 32:9-12)
"Basi nikalinunua shamba lile lililoko Anathothi kwa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, nikampimia fedha yake, shekeli kumi na saba za fedha. NAMI NIKAITIA SAHIHI ILE HATI, na kuipiga muhuri, nikawaita mashahidi, nikampimia ile fedha katika mizani. Nikaitwaa ile hati ya kununua, ile iliyopigwa muhuri kama ilivyo sheria na ada, na ile nayo iliyokuwa wazi; na ile hati ya kununua nikampa Baruku, mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, mbele ya uso wa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, na MBELE YA MASHAHIDI wale walioitia sahihi hati ya kununua, mbele ya Wayahudi wote walioketi katika uwanda wa walinzi.
Wakati mwingine katika manunuzi kuna haja ya kuzingatia taratibu za kisheria kama vile kuwepo mashahidi, mwanasheria, viongozi wanaotambuliwa katika mchakato wa manunuzi ya kitu fulani.
7. Shirikisha wataalamu wa kile unachotaka kununua (participatory procurement).
Ukweli ni kwamba kuna manunuzi mengine yanahitaji yashirikishe wataalamu wa hicho unachotaka kununua.
Kwa mfano huwezi kununua mitambo ya kijeshi bila wataalamu wa masuala ya kijeshi kushirikishwa. Huwezi kununua madawa ya binadamu bila kuahirikisha wataalamu.
Usipowashirikisha wataalamu unaweza kujipata umenunua bidhaa ambayo sio bora au bidhaa iliyopitwa na wakati au bidhaa ambayo haihitajiki kwa wakati huo au bidhaa ambayo ipo na ukajikuta umeleta bidhaa kama iliyopo nakadhalika, kuna wakati lazima wataalamu washirikisshwe katika manunuzi.

0 Maoni