(Mithali 14:1)
BAADHI YA DHANA ZA UJENZI (Concepts of building)
1. Kila anayejenga huitwa fundi, kwa hiyo mwanamke amefananishwa na fundi anayejenga nyumba, mwanamke anapaswa kujichukulia kama fundi au kujitazama kama fundi.
2. Kila anayejenga lazima awe na ramani (picha) ya nini anataka kujenga, kwa hiyo mwanamke anapaswa kuwa na picha ndani yake kuhusu nini anachotaka kujenga, yaani awe na picha anataka kujenga nyumba ya aina gani.
3. Huwezi kujenga bila kuweka msingi, picha ya kile unataka kujenga inaamua msingi utakuwa wa aina gani, kwa mfano fundi akitaka kujenga nyumba yenye vyumba vinne lazima msingi uwe sawasawa na picha aliyonayo (ramani). Ndoa zina misingi ya aina tofauti ndio maana hazifanani, kuna ndoa za mfano wa kuigwa na kuna ndoa ambazo zina hali mbaya, kuna wanandoa wanaoga pamoja lakini wengine hawawezi kufanya hivyo, kuna wanandoa wanaweza kukumbatiana lakini wengine hawawezi, kuna wanandoa wanaweza kucheza pamoja lakini wengine hawawezi, kwa mfano kuna siku ambayo Mfalme Abimeleki alichungulia dirishani akamwona Isaka anacheza na Rebeka (anamkumbatia na kumpapasa Rebeka) akatambua kuwa hao ni mke na mume (Mwanzo 26:8), mapenzi hayo ni matokeo ya msingi uliojengwa.
Kama mwanamke anataka kujenga nyumba yenye amani na furaha lazima ajenge msingi wa hicho anachotaka kujenga, msingi ni kitu kinachofanyika kwanza (Mwanzo), kwa hiyo kujenga msingi ni kuanza jambo fulani au ni kujenga tabia fulani ambayo itazaa kitu fulani, kwa mfano kujenga tabia ya kumpokea au kumlaki mumeo akirudi nyumbani haijalishi ana kitu au hana kitu, kumwambia mumeo pole nakadhalika.
4. Aina ya msingi au uimara wa msingi unaamua nyumba iwe imara au isiwe imara (Mathayo 7:24-27).
Biblia inasema mwanamke mpumbavu hubomoa nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe (Mithali 14:1) mwanamke mpumbavu ni pamoja na mwanamke asiye na neno la Mungu moyoni mwake, Yesu amesema "na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga" (Mathayo 7:26).
Neno la Mungu ndilo msingi imara wa chochote ikiwemo ndoa, ukijenga nyumba yako bila neno la Mungu lazima hiyo nyumba ianguke, mwanamke mjenzi ni mwanamke mwenye neno la Mungu, mwanamke anayetii neno la Mungu.
5. Ujenzi ni gharama (Luka 14:28-30, chochote unachotaka kujenga lazima ukubali kulipa gharama zake, kwa mfano kujenga nyumba yenye furaha na amani ni gharama, kama hauko tayari kulipa gharama hizo huwezi kujenga nyumba yenye amani na furaha, gharama mojawapo unayotakiwa kulipa ili kujenga nyumba yako ni kumtumikia mumeo (Bwana wako), Biblia inatujulisha kuwa Sara alimchukulia Ibrahimu mumewe kama Bwana wake (1 Petro 3:6), lazima ukubali kumtii mumeo na kujitiiisha kwake (uwe chini ya mamlaka yake) na kumtumikia.
5. Ujenzi unahusisha vipimo (Mwanzo 6:14-5), Mungu alipomwambia Nuhu ajenge Safina alimpa vipimo ajenge kwa vipimo alivyopewa.
Ujenzi unahusisha vipimo, mwanamke mjenzi lazima ajue kupima mambo mbalimbali, kupima hali ya ndoa yake, kupima hali za watu wa nyumbani mwake ikiwemo mumewe, kupima ni pamoja na kuchunguza hali za watu wa nyumbani mwake (kuchunguza hali zao, mienendo yao nakadhalika), Biblia inasema mwanamke mwema "huchunguza yote yanayofanyika nyumbani mwake, kamwe hakai bure hata kidogo" (Methali 31:27).
Mwanamke mmoja anaitwa Abigail aligundua mumewe ni mwanamume mpumbavu, alijua namna ya kuishi na mwanamume mpumbavu na kumuepusha mumewe na mambo mabaya, soma 1 Samweli 25:25 "nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma" pia unaweza kusoma simulizi ya Nabali na mkewe kwa upana (1 Samweli 25:2-33).
Abigail hakudai talaka kwa sababu mumewe ni mpumbavu, hakuachika kwa kuwa mumewe ni mpumbavu pia hakumtendea mabaya mumewe kwa kuwa ni mpumbavu bali aliishi kwa akili na busara na mwanamume yule mpumbavu. Mwanamke mjenzi huwa haombi talaka, huwa haachiki pia hujenga nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe.
6. Fundi lazima ajue vitu vinavyohitajika ili kujenga, kila anayejenga lazima afahamu atatumia maji, mchanga, saruji nakadhalika.
Mwanamke mjenzi lazima ajue vitu anavyohitaji ili kujenga nyumba yake, Biblia inasema mwanamke mwenye hekima hujenga nyumba yake kwa mikono yake, kwa hiyo kitu kimojawapo unachohitaji kuwa nacho ili ujenge nyumba yako ni hekima.
Chanzo kikuu cha hekima ni Mungu pekee, baadhi ya mbinu za kupata hekima kutoka kwa Mungu ni 1. kuomba (Yakobo 1:5-6), 2. Kuliweka neno la Mungu moyoni mwako (Kumbukumbu la torati 4:6).
HITIMISHO
Ukitaka kuwa mwanamke mjenzi zingatia hayo ambayo nimefundisha, utajenga nyumba yako kwa mikono yako mwenyewe, lakini usipozingatia hayo utabomoa ndoa yako kwa mikono yako mwenyewe.

0 Maoni