Wakati mpango wa kuwaangamiza wayahudi ukiendelea kuratibiwa, wakati huo Esta alikuwa Malkia yaani mke wa Mfalme Ahasuero, Malkia Esta alilelewa na Mordekai hatimaye akaja kuwa Malkia.
Wakati mpango ule mbaya ulipokuwa ukiratibiwa, Mordekai alituma ujumbe kwa Malkia Esta, ujumbe huo ni huu "kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo? (Esta 4:14).
Mordekai alitaka Malkia Esta atumie nafasi yake ya umalkia kuzuia mpango ule mbaya usifanikiwe kwa kuwa Mungu alimpa nafasi sio kwa ajili yake tu bali pia kwa ajili ya maslahi ya wayahudi pia Mordekai alimwambia Malkia Esta "hata kama wewe utanyamaza au hata kama wewe hautafanya chochote kitakachopelekea wayahudi wasiangamie basi Mungu atainua mtu mwingine au Mungu atafanya njia nyingine ili wayahudi wasiangamie".
Mordekai aliamini Mungu ana watu wengi au ana njia nyingi ambazo anaweza kuzitumia kuwaokoa wayahudi au kuwasaidia wayahudi wasiangamie. Kumbuka kuwa Mungu aliwahi kumwambia Mtume Paulo asiogope kwa kuwa yeye anao watu wengi katika mji ule ambao anaweza kuwatumia kwa ajili ya usalama wa Paulo Ili asidhurike (Matendo ya Mitume 18:10).
UJUMBE WANGU KWAKO
Hata kama uliowatarajia watakusaidia hawajakusaidiabau hata kama hauna wa kukusaidia usiogope wala usinung'unike, mwamini Mungu yeye anao watu wengi anaoweza kuwatumia kukusaidia, Mungu anazo njia zingi za kukusaidia (Isaya 55:8-9).
Usisahau kuwa Mungu aliwahi kumpelekea chakula Nabii Eliya kwa kuwatumia ndege waitwao kunguru (1 Wafalme 17:4-6).
Usisahau kuwa Mungu aliwahi kumtoa Mtume Petro gerezani bila mtu yeyote kumkatia rufaa mahakamani (Matendo ya Mitume 12:7-12).
HITIMISHO
Hata kama uliotarajia watakusaidia wamenyamaza, hata kama hauna wa kukusaidia usiogope mwamini Mungu, jifunze kwa Mordekai na uamini kuwa Mungu anao watu wengi anaoweza kuwatumia kukusaidia, Mungu anazo njia nyingi za kukusaidia.
Pia nakukumbusha kuwa Mungu amekupa au akikupa nafasi fulani, kazi, mali nakadhalika, hakikisha unaitumia vizuri kwa kuhakikisha unatenda kwa usahihi sawasawa na mapenzi ya Mungu ya kukupa nafasi hiyo, kazi hiyo, mali hizo nakadhalika. Kumbuka Yusufu aliinuliwa na Mungu kule Misri sio kwa ajili ya manufaa ya nchi ya Misri tu, sio kwa ajili ya maslahi yake tu bali pia kwa ajili ya ndugu zake na taifa la Israeli (Mwanzo 45:3-15). Hata kama wewe utanyamaza, Mungu atainua mtu au watu wengine LAKINI HAITAKUWA HERI KWAKO.

0 Maoni