ELIMU YA AWALI KUHUSU MALANGO - Sehemu ya 1


 UTANGULIZI

Baada ya Mungu kumaliza kazi yake ya uumbaji alimpa mtu mamlaka ya kumiliki na kutawala dunia na vilivyomo hivyo basi hakuna chochote kingeweza kuingia duniani bila mtu kuruhusu ndio maana dhambi iliingia duniani kupitia mtu (Warumi 5:12)

Hakuna chochote kinaweza kutendeka hapa duniani bila mlango fulani kufunguka, Mungu akitaka kufanya jambo humu duniani lazima apate mlango wa kuutumia kupitisha vitu vyake na shetani vivyo hivyo akitaka kufanya jambo duniani lazima apate mlango wa kuutumia.

Jambo mojawapo ambalo Mungu alimwambia Ibrahimu ni kwamba "uzao wake utamiliki mlango wa adui zao" (Mwanzo 22:15-17) wakati Rebeka anaondoka kwao baraka mojawapo aliyoondoka nayo ni baraka ya kumiliki mlango wa adui zake (Mwanzo 24:59-60)

Kwa nini suala la kumiliki malango linepewa kipaumbele? ni kwa sababu kwenye mlango ndiko mambo mbalimbali hupitia.

Kama umeokoka (umezaliwa mara ya pili) wewe ni uzao wa Ibrahimu (Wagalati 3:29) kwa hiyo una haki ya kumiliki mlango wa adui zako sawasawa na ahadi ya Mungu kwa Ibrahimu au sawasawa na agano la Mungu kwa Ibrahimu.

Kumiliki malango ni Nini? ni kuwa na mamlaka kwenye milango mbalimbali (uwezo na haki ya kufunga na kufungua au kutumia mlango huo kukunufaisha, kudhibiti mlango huo Ili usitumike kuleta mabaya kwenye maisha yako.

MAMBO UNAYOPASWA KUFAHAMU KUHUSU MALANGO

1. Kuna aina nyingi sana za malango kwa mfano mtu ni mlango (Luka 10:24)(Yohana 10:7)(Zaburi 135:19)(Warumi 5:12), muda ni mlango, kazi au biashara ni mlango wa kiuchumi, ardhi ni mlango, mipaka ni milango, kinywa ni mlango, pua ni mlango, macho ni mlango, masikio ni mlango nakadhalika.

2. Mlango ni sehemu yoyote au ni kitu chochote ambacho vitu huingia au kutokea.

3. Milango inamilikiwa kwa jinsi ya rohoni na jinsi ya mwilini (Zaburi 22:15-17), Kwa mfano kama mlango wako wa uchumi unamilikiwa na shetani kila fedha au faida utakayopata kupitia mlango huo zitafanya kazi za shetani, hizo fedha zitaishia kutibu magonjwa au zitapotea nakadhalika.

4. Kila mlango una funguo yake au funguo zake (Mathayo 16:19(Isaya 22:20-22)

5. Aliye na funguo ndiye mwenye mamlaka kwenye mlango (Ufunuo wa Yohana 3:8), kama hauna ufunguo huwezi kufungua mlango uliofungwa.

Kwa mfano Nuhu aliunda Safina ila Mungu alifunga mlango wa Safina, naamini hata Nuhu alitamani kuwafungulia wengine waingie gharika ilipoanza ila hakuweza kufungua kwa kuwa aliyefunga Safina ni Mungu (Mwanzo 7:16).

Fuatilia sehemu ya pili ya somo .......................

Chapisha Maoni

0 Maoni