Neno ustahimilivu linaweza kutafsiriwa kwa namna mbalimbali kutegemeana na muktadha, hususani wapi neno hilo limetumika.
Maana mojawapo ya neno ustahimilivu ni uwezo wa kubaki imara na kusonga mbele japokuwa kuna magumu, adha, kero, vikwazo, lawama na mambo yanayoudhi (2 Timotheo 3:10-11) (Zaburi 69:7)(Zaburi 89:50) (1 Wakorintho 4:12) (2 Wathesalonike 1:14).
Kubaki imara ni pamoja na kutofanya maamuzi mabaya kutokana na jambo fulani lililojitokeza, kubaki imara ni pamoja na kutofanya mambo kwa pupa, kubaki imara ni pamoja na kutoendeshwa na hisia zako, kubaki imara ni kubaki katika wajibu wako kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria bila kujali mazingira nakadhalika.
Mfalme Daudi ni mojawapo ya kiongozi wa mfano wa kuigwa kwenye mambo mbalimbali ikiwemo USTAHIMILIVU.
Wakati fulani alipofika mahali panaitwa Bahurimu ghafla akaja mtu aliyeitwa Shimei akaanza kumlaani, kumtukana na kumrushia mawe Mfalme Daudi na walinzi wake, walinzi wake walihamaki mmoja wao akaomba kibali kwa Mfalme Daudi ili akate kichwa cha Shimei lakini Mfalme Daudi hakukubaliana na jambo hilo la kumuua Shimei.
NB: Kiwango cha ustahimilivu hupimwa kwa njia mbalimbali ikiwemo vile unavyowatendea wakosoaji wako au wapinzani wako. Kama unawatendea mabaya wakosoaji au wapinzani wako, hiyo ni dalili mojawapo ya kukosa ustahimilivu.
MAMBO BAADHI YATAKAYOKUSAIDIA KUONGEZA NA KUDUMISHA USTAHIMILIVU NDANI YAKO
1. Usiwe na haraka kufanya maamuzi linapotokea jambo fulani linaloudhi.
2. Jifunze kutawala hisia zako ili zisikuendeshe, jambo mojawapo la kukusaidia kuzitawala ni hisia zako ni kutoziamini hisia zako kwa kuwa hisia zinabadilika.
3. Fahamu kuwa kukosolewa au kupingwa ni jambo la kawaida, wewe sio wa kwanza kupingwa au kukosolewa, hata Mungu anapingwa na kukosolewa na watu wengi sana lakini Mungu anawatendea mema wanaompenda na wanaompinga.
4. Usiangalie leo, angalia kesho, usiangalie hapo ulipo angalia mbele (Waebrania 12:2). Kuna mambo unaweza kuyafanya leo lakini kesho yatakuletea majuto na matatizo makubwa sana, hivyo basi unapotenda jambo usiangalie leo tu angalia na kesho, usiangalie hapo ulipo tu angalia mbele.

0 Maoni