(2 Wafalme 17:24-28)
Lengo la somo hili ni kukupa ufahamu wa kiroho kuhusu mazingira ili ikusaidie jinsi ya kuishi kwenye mazingira fulani bila kuathiriwa na nguvu za giza zinazotawala mahali fulani pia ikusaidie ufahamu wa jinsi ya kuyaombea mazingira unayoishi.
UTANGULIZI
Zipo tafsiri mbalimbali za neno mazingira ila tafsiri maarufu ni ile isemayo "mazingira ni jumla ya vitu vyote vinavyomzunguka mtu" kama vile ardhi, miti, watu, mawe nakadhalika.
Mazingira yote unayoyaona hapa duniani yanatawaliwa kwa jinsi ya rohoni na Mungu au shetani haijalishi watu wanafahamu au hawafahamu.
Roho inayotawala katika mazingira fulani huathiri wanaokaa kwenye mazingira hayo ndio maana unaweza kukuta watu wanaoishi katika mazingira fulani wana tabia zinazofanana, wana misimamo ya aina fulani, wana imani ya aina fulani (kwa mfano kukeketa, wakifagia hlwakati wa usiku hawatoi uchafu nje nakadhalika).
BAADHI YA MIFANO YA ROHO ZINAZOTAWALA MAZINGIRA
MFANO WA 1: Nabii Isaya alisema yeye ni mtu mwenye midomo michafu kwa kuwa anaishi kwenye jamii ya watu wenye midomo michafu (Isaya 6:5).
MFANO WA 2: Yakobo alilala mahali fulani, alichukua jiwe la mahali pale akalilalia, ghafla aliota ndoto na katika ndoto Mungu alizungumza na Yakobo, Yakobo alipoamka alisema "Mungu yuko mahali hapa, mahali hapa panatisha kama nini bila shaka hapa ni nyumba ya Mungu ni lango la mbinguni (Mwanzo 28:11-17), Mungu alikuwa anatawala mahali pale.
MFANO WA 3: Musa alifika kwenye mlima Horebu na aliona kichaka kinawaka moto lakini hakiteketei alipogeuka kutazama, Mungu alimuita Musa Kisha akamwambia "vua viatu vyako kwa kuwa hapo ni mahali patakatifu" maana yake ni kwamba Mungu alikuwa anamiliki maeneo yale.
MFANO WA 4: Mfalme wa Ashuru alileta watu kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu, akawaweka katika miji ya Samaria badala ya wana wa Israeli; wakaumiliki Samaria, wakakaa katika miji yake, Biblia inasema walipoanza kukaa kule hawakumcha Mungu aliyetawala yale maeneo hatimaye Mungu alipeleka Simba wakaanza kuwaua wale watu (2 Wafalme 17:24-27). Waliuawa kwa kuwa hawakutenda yaliyomfurahisha Mungu aliyetawala lile eneo.
BAADHI YA MBINU ZA KUBAINI ROHO INAYOTAWALA MAZINGIRA FULANI
1. Angalia tabia za watu wa eneo fulani, Nabii Isaya alisema ana midomo michafu kwa kuwa anakaa kwenye jamii ya watu wenye midomo michafu (Isaya 6:5)
2. Angalia madhabahu zilizopo kwenye eneo hilo hilo ni madhabahu za Mungu au shetani, Mtume Paulo alisema alipofika Athene aliona madhabahu imeandikwa "kwa mungu asiyejulikana" (Matendo ya Mitume 17:22-23).
BAADHI YA HATUA ZA KUCHUKUA IKIWA MAZINGIRA YANATAWALIWA NA ROHO CHAFU
1. Usiwahi kuanzisha vita na roho inayotawala au zinazotawala mazingira fulani, nashauri unaweza kupambana na roho chafu za eneo fulani ikiwa unafanya kazi kwenye eneo hilo, unaishi kwenye eneo hilo au ikiwa Roho Mtakatifu amekuruhusu kushughulikia roho hiyo.
2. Mwanga damu ya Yesu kwenye mazingira hayo ili kuyakomboa na kuyatiisha chini ya Mungu.
3. Injili ni silaha mojawapo dhidi ya roho zinazotawala eneo fulani, silaha mojawapo iliyowasaidia Mitume kuangusha ngome za roho chafu za maeneo mbalimbali.
HITIMISHO
Baada ya kugundua kuwa mazingira yanatawaliwa kwa jinsi ya rohoni na Mungu au shetani unapaswa kuchukua hatua ili ikiwa mazingira yanatawaliwa na roho chafu usije kuathiriwa na kazi za roho hizo chafu.

0 Maoni