MBINU RAHISI ZA KUKUSAIDIA KUYAELEWA MAANDIKO YA BIBLIA


 UTANGULIZI

Watu wengi wanaposoma maandiko ya Biblia wengine hushindwa kuyaelewa kutokana na sababu mbalimbali, hii shida ya kutoelewa maandiko ya Biblia haijaanza leo ilianza tangu zamani sana hata wanafunzi wa Yesu Kuna wakati hawakuelewa maandiko (LUKA 24:45).

Kutokuelewa maandiko ni mojawapo ya tatizo linalowasumbua watu wengi sana waliomo makanisani na walio nje ya kanisa.

Shetani hapendi watu wayaelewe maandiko kwa kuwa anajua wakiyaelewa maandiko watapata faida nyingi sana (Mathayo 13:15,19,23)

Maandiko ya Biblia ndio maandiko ya ajabu sana kuliko vitabu vyote kwenye hii dunia, kwa sababu maandiko ya Biblia;-

1. Yanaweza kuzungumza na mtu anapoyasoma kwa kuwa kwenye maandiko kuna sauti ya Mungu (2 Timotheo 3:16)

2. Yanaweza kumuelekeza mtu jambo la kufanya (Yoshua 1:8) Yoshua aliambiwa azingatie maandiko kwa kuwa katika maandiko atapata maelekezo ambayo anatakiwa kuyatendea kazi.

3. Yanaweza kugusa nafsi na moyo wa mtu ndio maana watu wanaweza kuchomwa mioyo yao wanaposikia ujumbe uliomo kwenye maandiko ya Biblia (Matendo 2:37-38), watu wanaweza kulia wanaposikia maandiko ya Biblia (Nehemia 8:1-9), watu wanaweza kupata mguso wa kiroho wanaposikia maandiko (Luka 24:32)

4. Yanaweza kumuhekimisha mtu. (2 Timotheo 3:15)

5. Ni silaha mojawapo dhidi ya shetani na kazi zake (Mathayo 4:4-11).

6. Maandiko yanaweza kukufunulia yaliyojificha (Siri) (Danieli 9:1-3) Danieli aliposoma vitabu akakutana na maandiko ya Nabii Yeremia ambayo yalimfunulia siri iliyokuwa imefichika kwenye maandiko yale kuhusu muda ambao utumwa wa waisraeli ulipaswa kuisha.

MADHARA YA KUTOKUELEWA MAANDIKO YA BIBLIA

Kutokuelewa maandiko kumesababisha mambo mbalimbali kutokea

1. Kupotosha maandiko au kutumia maandiko vibaya (isivyo halali) (2 Petro 3:16)

2. Kutokuona umuhimu wa kusoma Biblia

3. Kutokuona umuhimu wa kuwa na Biblia (kununua Biblia), Biblia inasema tununue kweli (Mithali 23:23)

4. Kuzuka kwa imani potofu na mafundisho yasiyo sahihi, kwa mfano kuna maandiko yanasema "mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume na mwanamume asivae mavazi yampasayo mwanamke"  (Kumbukumbu la torati 22:5). Hilo ni andiko mojawapo ambalo limezua mambo mengi kwenye jamii ya wakristo, watu wengi kwa Kutokuelewa andiko hilo wamezusha mafundisho ambayo sio sahihi.

5. Kuongezeka kwa madhehebu mbalimbali, Zipo sababu mbalimbali ambazo husababisha madhehebu mbalimbali kuzuka, sababu mojawapo ni KUTOKUYAELEWA MAANDIKO. Madhehebu yameanza tangu zamani sana kwa mfano kwenye Biblia utaona baadhi ya madhehebu ya MAFARISAYO (Matendo ya Mitume 15:5), MASADUKAYO (Matendo ya Mitume 5:17) , WANAZORAYO (Matendo ya Mitume 24:5)

6. Watu wanabaki kuwa wachanga kiroho na wanachukuliwa huku na kule kwa mafundisho ya waalimu wa uongo, Mitume wa uongo, manabii wa uongo nakadhalika (Mathayo 22:29). Biblia imeeleza habari ya watu wa Beroya walikuwa wana utaratibu wa kuchunguza maandiko, walikuwa hawaamini ovyoovyo mpaka wamechunguza maandiko (Matendo ya Mitume 27:12)

7. Huwezi kujua kuomba kwa usahihi na kuwa mwombaji unayepata matokeo ya maombi kama hauyajui maandiko.

MBINU RAHISI ZA KUKUSAIDIA KUYAELEWA MAANDIKO YA BIBLIA

1. Soma maandiko (soma Biblia) (Mathayo 21:42)(Luka 24:27)

Baadhi ya mbinu za kusoma Biblia (a) soma kwa kutafuta unachotaka kusoma au kutafuta habari unayotaka kuisoma (Luka 4:17) (b) Soma sura nzima (c) soma mistari inayozungumzia mada zinazofanana (d) soma tafsiri tofauti tofauti za Biblia 

2. Kama haujaelewa andiko fulani, tafuta mtu wa kumuuliza ili akufafanulie (Matendo ya Mitume 8:26-37)

Kuna wakati ili uyaelewe maandiko lazima upate wa kukufundisha maandiko, kama haujaelewa maandiko usione aibu kuuliza, sisi ni wanafunzi wa Yesu, mwanafunzi anayeuliza ndiye hupata ufahamu.

3. Chunguza maandiko (Matendo 17:11)

Kuchunguza maandiko ni kulinganisha kama mahubiri uliyohubiriwa yanafanana na kilichoandikwa kwenye maandiko (hicho ndicho walifanya waberoya). Sikuhizi si ajabu kuona watu wanasikiliza mahubiri na hawana Biblia kwa hiyo wanaweza kudanganywa kwa wepesi sana.

Kuchunguza maandiko ni kutaka kufahamu tafsiri ya maneno, kutaka kufahamu kwa nini mambo hayo yaliandikwa, mazingira ya walioandikiwa yalikuaje.

Kwa mfano maandiko yanasema  "mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume na mwanamume asivae mavazi yampasayo mwanamke"  (Kumbukumbu la torati 22:5). Hilo ni andiko mojawapo ambalo limezua mambo mengi kwenye jamii ya wakristo.

Ili uweze kulielewa andiko hilo lazima uchunguze (a) wanawake na wanaume walioandikiwa hilo andiko walikuwa wanavaa nguo za aina gani (b) je kwetu sisi tunawezaje kulitumia hilo andiko.

4. Mwambie Roho Mtakatifu akutie kwenye kweli yote kuhusu jambo fulani unaposoma maandiko (Yohana 16:13).

5. Muombe Bwana Yesu afunue akili zako au azitie nuru akili zako upate kuelewa maandiko (Luka 24:45)



Chapisha Maoni

0 Maoni