UMUHIMU WA KUMUOMBEA MCHUNGAJI NA KUMTIA MOYO


 (Mathayo 4:1-8)(Yohana 10:11,14)

Yesu alijitambulisha kama mchungaji mwema wa kondoo zake, kwa hiyo wanafunzi wake tuwaite kondoo zake.

Iko hivi, wakati Yesu anakutana na Shetani kule nyikani wanafunzi wake hawakuwepo, alikuwa mwenyewe (peke yake) baada ya kutoka kule nyikani ndipo alipowaita wakina Petro na wengine wamfuate atawafanya kuwa wavuvi wa watu.

Nataka utafakari hivi, kama shetani angemshinda Yesu (mchungaji) kule nyikani, yamkini Yesu asingeendelea na kazi iliyomleta duniani, angekuwa chini ya shetani anamtumikia shetani, anaongozwa na Shetani.

SASA FAHAMU HILI

Kila mchungaji ana vita anavyopigana sirini, au ana vita anavyopigana akiwa yeye mwenyewe (peke yake) bila wengine kuwepo, anapigana vita kwa ajili yake na kwa ajili ya kondoo, shetani akimshinda mchungaji hata ninyi kondoo mko kwenye hatari kubwa sana.

Wachungaji hupigana vita zinazowalenga wao binafsi na vita zinazowalenga kondoo.

Daudi alipigana na Simba na dubu akiwa peke yake kule alikokuwa akichunga kondoo wa Mzee Yese (baba yake), Daudi alikuwa akiwapigania kondoo akiwa peke yake, rejea (1 Samweli 17:34-35).

Unajua kwamba mchungaji wako anapigana vita nyingi sirini au akiwa peke yake kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili yako? 

Kama haufahamu nakufahamisha kwamba wachungaji hupigana vita nyingi sirini au wakiwa peke yao ili kuwapigania kondoo, wachungaji hukabiliana na pepo wachafu wanaomshambulia yeye mwenyewe na wanaoshambulia kondoo (waumini), wachungaji hupigana vita hizo wakiwa peke yao WAUMINI HAWAJUI KABISA YANAYOENDELEA SIRINI.

Wachungaji hushambuliwa na Shetani ili kuwadhuru, kuwaharibu na kuwaangamiza wakiwa peke yao (sirini) na hakuna anayejua kuhusu kinachoendelea.

UKIFAHAMU HAYO

1. Mtegemeze mchungaji wako kwa maombi, muombee Mchungaji wako, Mungu ampe kushinda vita zote anazopigana sirini (akiwa peke yake) kwa ajili yake binafsi na kwa ajili ya kondoo.

2. Mtie moyo mchungaji wako kwa kumuheshimu, kunyenyekea chini yake, kumshukuru kwa kazi anazofanya kwa ajili yako hata kama hauoni, pia mtie moyo kwa vitu vya kimwili (fedha, mali, lipia bili za maji, umeme, vocha, lipia tiketi za safari zake binafsi, lisha mchungaji wako, tunza familia yake nakadhalika kama Roho wa Mungu atakavyokuongoza.

Angalizo: Sijasema watumishi wa Mungu wengine wasiombewe au kutiwa moyo, mimi nimekufundisha kuhusu mchungaji.


Chapisha Maoni

0 Maoni