JINSI YA KUKABILIANA NA WATU WENYE ROHO YA WIVU WA KISHETANI

 


UTANGULIZI

Ukisoma Biblia utagundua kuwa wivu ni kitu cha kiroho ndio maana hata Mungu anasema yeye ni Mungu mwenye wivu (Kutoka 20:5), wivu ni roho (Hesabu 5:30), kuna wivu unaotokana na Mungu na wivu unaotokana na shetani (Yakobo 3:14).

Watu wenye roho ya wivu kutoka kwa shetani wapo kila mahali kuanzia kwenye familia, mtaani, kazini, sehemu za biashara, makanisani nakadhalika

BAADHI YA DALILI ZA MTU MWENYE ROHO YA WIVU WA KISHETANI

1. Hapendi wengine wasifiwe au wapongezwe, wakisifiwa au wakipongezwa wengine yeye anachukia sana

Sauli aliposikia Daudi anasifiwa alichukia sana (1 Samweli 18:6-9)

2. Hapendi kuona mwingine au wengine wanapata, anataka apate yeye tu au abaki yeye tu

Herode aliposikia kuna Mfalme mwingine amezaliwa aliua watoto wote ili asitokee mtu wa kukaa kwenye Ile nafasi. (Mathayo 2:1-).

3. Akiona mwingine amepata kitu fulani (kazi, Mali n.k) anatamani na yeye apate, ukipata kitu halafu ukaona mtu mwingine na yeye anatafuta kama hicho ili mlingane, mtu huyo ana Roho ya wivu KUWA MAKINI NAYE (Mwanzo 30:1-24).

4. Anachukia anaposikia maono, ndoto au mipango ya mtu 

Ndugu zake Yusufu waliposikia ndoto za Yusufu walimchukia sana (Mwanzo 37:3-28)

Ukiona mtu amebadilika ghafla baada ya kumwambia malengo yako, maono yako au mipango yako, Kaa mbali na huyo mtu ni hatari kwako, Yusufu alijipata kwenye matatizo makubwa baada ya KUELEZA ndoto zake.

5. Kukupeleleza mambo.

Ukiona mtu anakupeleleza sana mambo yako anataka ajue mambo yako, ajue kuhusu wewe, ajue mipango yako, KUWA MAKINI NA MTU HUYO.

(Mathayo 2:1-8) Mfalme Herode aliposikia kuna Mfalme mwingine amezaliwa aliwatuma mamajusi wawe kama wapelelezi wake wamletee habari kuhusu Yesu.

6. Ubinafsi (bora tukose wote).

(1 Wafalme 3:16) Habari ya hawa makahaba wawili na hukumu ya Mfalme Sulemani inafundisha mambo mengi sana.

Kahaba mmoja aliona ni heri mtoto akatwe vipande viwili ili wote wakose mtoto, hiyo ni roho ya wivu.

Mtu mwenye wivu yuko tayari mkose wote, anaweza kufanya lolote ili mkose wote kitu au jambo fulani.

Ukiona mtu yuko tayari mkose wote kuliko wewe upate, fahamu kuwa mtu huyo ana roho ya wivu.

JINSI YA KUKABILIANA NA WATU WENYE ROHO YA WIVU

1. Jizoeze kuficha taarifa zako, ficha taarifa za mipango yako.

(Mwanzo 37:3-28) Ndugu zake Yusufu waliposikia ndoto za Yusufu walizidi kumchukia sana, wivu uliwatesa (Yusufu alipendwa sana na baba yao halafu anaota ndoto zinazoonyesha atakuwa mtu mkubwa), kilichomponza Yusufu ni kuweka wazi ndoto zake, kuwaambia watu ndoto zake.

Kilichosababisha Herode akaua watoto ni kwa sababu alisikia habari kuna Mfalme mwingine amezaliwa.

2. Jitenge na mtu mwenye wivu (Kaa mbali naye)

Biblia inasema Mfalme Sauli alimwonea wivu Daudi (1 Samweli 18:9) baada ya hapo Mfalme Sauli alikuwa anapanga kumuua Daudi 

(1 Samweli 19:10-12) Daudi aliamua kujitenga na Mfalme Sauli mwenye wivu aliyekuwa anamuwinda.

Malaika alimwambia Yusufu mchukue Mariam mkeo na mtoto mkimbilie Misri.

Jitenge na watu wenye wivu kwa usalama wako.

3. Maombi au kumuomba Mungu.

Mungu ndiye ambaye anaweza kutuokoa na mipango ya watu wenye wivu.

4. Hekima ya Mungu ni muhimu sana katika kukabiliana na watu wenye wivu.

(1 Wafalme 3:16-28) Hekima aliyokuwa nayo Mfalme Sulemani ilimsaidia Kahaba mmoja kupata haki yake, mwenzake alimwonea wivu kwa sababu yeye ana mtoto wakati mwenzake amefiwa mtoto.

Kama isingekuwa hekima ya Mungu kuwemo ndani ya Mfalme Sulemani, wote wangebaki bila watoto.

Kuna hekima ya Mungu ya kukusaidia kuishi salama katikati ya watu wenye roho ya wivu.




Chapisha Maoni

0 Maoni