Ukisoma Biblia utagundua kuwa kazi mojawapo ya shetani na ufalme wake ni kuvunja watu mioyo (KUNA WATU WANA UPAKO WA KUZIMU WA KUVUNJA WATU MIOYO, KUNA WATU WANAKALIWA NA PEPO WA KUVUNJA MOYO WENGINE, KUNA WATU WANATUMIWA NA PEPO WA KUVUNJA MOYO) ili shetani na ufalme wake watende kazi zo kwa kuwa wanafahamu mwanadamu akivunjika moyo mambo mbalimbali hutokea kama vile;-
1. Uwezo wake wa kufikiri unapungua.
2. Hushindwa kufanya maamuzi sahihi.
3. Hupoteza matumaini.
4. Mwanadamu anaweza akajikuta amekuwa mtu wa kukiri mambo mabaya nakadhalika.
Nadhani unafahamu kuwa ukienda hospitalini hakuna daktari ambaye atakuvunja moyo hata kama anaona una hali mbaya sana, daktari atakutia moyo atakuambia usijali utapona kabisa, anachofanya ni kukutia moyo kwa kuwa kutia moyo ni tiba mojawapo ya kisaikolojia.
Pepo hawa wa kuvunja moyo hufanya kazi kwa ustadi sana ili kuhakikisha wanawavunja watu mioyo, pepo hawa hutumia watu, hutengeneza mazingira au hali fulani za kuvunja moyo, pepo hawa wanaweza kumletea mtu picha mbalimbali ndani yake zinazomvunja moyo, pepo hawa hutumia habari mbaya kama silaha yao, pepo hawa wanaweza kutoa vitisho kupitia ndoto au kupitia watu pia pepo hawa huinua watu wa kukudharau au kudharau unachofanya au kudharau jitihada zako ili kukuvunja moyo nakadhalika.
Kuvunjika moyo ni tatizo ambalo huwasumbua watu wengi sana duniani ndio maana utaona kuna upako wa kuwaganga watu mioyo au kazi mojawapo ambayo Mungu hufanya ni kuwaganga watu mioyo (Isaya 61:1).
PEPO WA KUVUNJA MOYO WALIWASHAMBULIA WAISRAELI KUPITIA WAPELELEZI KUMI
Wapelelezi kumi waliotumwa na Musa kule Kanisani walitumiwa na pepo hawa ili kuwavunja moyo Waisraeli, wale wapelelezi waliwaletea wana wa Israeli habari mbaya zilizowavunja moyo kabisa (Kitabu cha Hesabu 13:32-33, Hesabu 14:1-11).
PEPO WA KUVUNJA MOYO WALIMSHAMBULIA NEHEMIA NA WENZAKE WAKATI WA UJENZI WA KUTA ZA YERUSALEMU NA MALANGO YAKE
Kuna watu waliinuka wakati Nehemia na wenzake wanaendelea na ujenzi wa Kuta za Yerusalemu na malango yake, watu hao ni Sanbalati, Tobia, waarabu, waashdodi na waamoni (Kitabu cha Nehemia 4:7-8).
Biblia inasema watu walikuwa na moyo wa kufanya kazi (Kitabu cha Nehemia 4:6) lakini ghafla waliinuka watu wakaanza kuwavunja moyo, walidharau ile kazi waliyokuwa wanafanya, walifanya mashauri ya kuikwamisha ile kazi isifanyike pia walitoa vitisho vingi ili kuwavunja moyo waache kufanya ile kazi.
Lakini mtumishi wa Mungu aliyeitwa Nehemia alisimamia vema ile kazi kuhakikisha inafanyika na inakamilika.
PEPO WA KUVUNJA MOYO WALIMSHAMBULIA NABII ELIYA KUPITIA YEZEBELI
Nabii Eliya ni mtumishi wa Mungu ambaye Mungu alimtumia kwa viwango vikubwa sana ikiwemo kufufua wafu, lakini pepo walifanya vita sana na Nabii Eliya kupitia mwanamke (malkia) aliyeitwa Yezebeli, Yezebeli alimpelekea Nabii Eliya ujumbe kwamba "kesho nitakuua).
Ujumbe huo ulimvunja moyo sana Nabii Eliya hatimaye akaanza kuomba Mungu aiondoe roho yake ili afe.
Nabii Eliya alisahau kuwa Mungu alimuhifadhi wakati fulani Mfalme Ahabu aliagiza watu wamtafute kila mahali lakini watu hawakumpata Nabii Eliya (Kitabu cha 1 Wafalme 18:7-10), kutokana na kuvunjika moyo Nabii Eliya alipoteza matumaini, imani yake ilitindika akasahau kuwa Mungu aliwahi kumuhifadhi alitafutwa kila mahali na hawakumpata.
PEPO WA KUVUNJA MOYO KWA WAOMBAJI
Kama wewe ni muombaji (mtu unayemuomba Mungu) kati ya pepo ambao watakushambulia ni pepo wa kuvunja moyo ili ukate tamaa uache kumuomba Mungu.
Yesu alitoa mfano kuhusu maombi kupitia kisa cha mjane aliyekuwa anadai haki yake, Yesu akasema kulikuwa na upinzani mkubwa unaolenga kuzuia mjane asipate haki yake lakini mjane hakukubali kuvunjika moyo alikazana kudai haki yake mpaka akapata (Kitabu cha Luka 18:1-8).
BAADHI YA DALILI ZINAZOONYESHA UNASHAMBULIWA NA PEPO HAWA
1. Kuvunjika moyo au kukata tamaa.
2. Kupoteza matumaini.
3. Kila wakati kujiona hauwezi, kujiona mnyonge, kujiona dhaifu.
BAADHI YA DALILI ZINAZOONYESHA MTU FULANI ANA PEPO LA KUWAVUNJA MOYO WENGINE AU ANATUMIWA NA PEPO WA KUWAVUNJA MOYO WENGINE.
1. Dharau (mtu anayedharau wengine).
2. Mtu anayewaletea wengine habari mbaya.
3. Mtu anayewatazamisha wengine kwamba ni dhaifu, hawawezi kufanya wanachofanya au wanachokusudia kufanya (wapelelezi kumi waliwaletea Waisraeli habari iliyowatazamisha kuwa wao ni wanyonge, dhaifu na hawawezi kukabiliana na wenyeji wa Kanaani).
4. Mtu anayewafanya wengine kupoteza matumaini.
BAADHI YA MAMBO YA KUFANYA ILI KUWASHINDA HAWA PEPO
1. Tumia jina la Yesu kama silaha dhidi ya hawa pepo.
2. Usiwape nafasi ya kukuvunja moyo, jitazame kama Mungu anavyokutazama na sio jinsi hao pepo wanavyokutazamisha.
3. Usiwe mwepesi kumwambia kila mtu habari zako, hatua zako au jitihada zako, mtaji wa hawa pepo ni taarifa zako, JIFUNZE KUFICHA TAARIFA ZAKO ZISIJULIKANE KWA WEPESI AU KWA KILA MTU, kuna watu wakisikia unafanya jambo fulani au unataka kufanya jambo fulani watakuvunja moyo mpaka utaacha kufanya unachofanya.

0 Maoni