UWEKEZAJI KIBIBLIA




FARAJA GASTO

Je! unatamani kufanikiwa?
Je! umewahi au unatamani ufanye biashara kubwa?
Je! unatamani kufanya kitu kikubwa maishani mwako?
Nahitaji kuongea na watu ambao wamejibu ndio kwenye maswali hayo, kitu ninachohitaji kusema nao ni kwa habari ya kitu kinachoitwa uwekezaji(investment).
Uwekezaji  si jambo geni masikioni au maishani mwa watu kwa kuwa uwekezaji ni kitu ambacho tumeumbwa nacho yaani ni hamu ambayo iko ndani ya kila mwanadamu kwa kuwa kila mwanadamu huwa ana msukumo wa kuwekeza haijalishi anawekeza nini, wapi na kwa wakati gani, kwa kuanza nataka nieleze maana ya uwekezaji ambayo ni rahisi kwa kila mtu kuielewa.

Uwekezaji ni hatua inayohusisha kutoa kitu au vitu au kuweka kitu au vitu au kutawanya vitu ulivonavyo kwa lengo la kupata kitu kingine na mara nyingi huwa ni kwa lengo la kupata faida kwa siku za usoni.
Kwa hiyo kwa tafsiri hiyo ni kwamba uwekezaji unahusisha mambo kadhaa; kutawanya au kuweka kitu au vitu mahali Fulani, kupata faida, kwa wakati ujao.
SWALI: Je! Mungu anataka tupate faida? Jibu ni ndio Mungu anataka tupate faida (Isaya 48:17).

Faida ni nini?
Faida ni nyongeza(addition) anayoipata mtu kutokana na uwekezaji wake.
Kwa tafsiri hiyo ni kwamba huwezi kupata faida kama haujaamua kuwekeza. Unaweza ukajiuliza
Nini uwekeze?
Lazima uwekeze
1.Muda
2.Mali
3.Nguvu
Ni vema ufahamu katika dunia hii wanaofanikiwa na watakaoendelea kufanikiwa ni watu wasiogopa kuwekeza kwa sababu hakuna faida nje na uwekezaji, ukiona mtu kafaidika nenda kamuulize alifaidikaje nina uhakika jibu atakalokupa atakuambia alitoa au aliwekeza. Wakristo wengi wanasahahu kuwa unapotoa sadaka unakuwa unawekeza na ipo siku utavuna faida na kutokana na kusahau hili wakristo wengi wamekuwa si watoaji wa sadaka na kwa kuwa si watoaji angalia maisha ya wakristo wengi ni maisha duni.

Mambo ya kufahamu unapotaka kuwekeza?
1.Lazima uwekeze kwa malengo
(Mathayo 25:14)
Unaposoma andiko hilo utaona kuwa huyo jamaa alipotaka kusafiri na alipoona ilikuwa safari itakayomgharimu muda mrefu na ukizingatia ni safari ambayo haitaongeza kipato chake ndipo akaamua kuwekeza ili atakapokuwa amerudi akute faida(Mathayo 25;27).

2.Lazima uwe na ufahamu juu ya mahali unapowekeza
(Mathayo 25:14-15)
Tunaona huyo aliwekeza fedha zake kwa watu anaowafahamu kwa kuwa walikuwa watumwa wake nandio maana alipowekeza aliwekeza kwao na huku akijua uwezo wa kila mmoja.
Suala la kufahamu mahali unapowekeza linatumiwa sana na taasisi za kifedha na ndio maana unapoomba mkopo benki watakuambia leta barua ya utambulisho, jaza fomu na uweke picha zako na pia leta wadhamini ili ikitokea umekimbia wawepo watu watakaowajibika kulipa deni lako.
Na hata kama una mpango wa kufanya biashara lazima uwe na ufahamu wa kutosha juu ya biashara unayotaka kuifanya ili usije kuwekeza na hatimaye ukaharibikiwa badala ya kufanikiwa.

3.Lazima uwe na subira
(Mathayo 25:19)
Tunaona katika andiko hilo baada ya kuwekeza alisafiri na akarudi baada ya siku nyingi ndipo akafanya hesabu kujua faida aliyoipata kulingana na kile alichoamua kuwekeza.
4.Unapowekeza ni vema uwe na uhakika wa kupata faida
(Mathayo 25:14,20-27)
Tunaona katika andiko hilo huyo jamaa aliwekeza akiwa na uhakika wa kupata faida na ndio maana alipotoka safarini alikuja kupiga hesabu na watumwa wake kwa sababu alijua lazima kuna faida ambayo imepatikana.
5. Unapopata fedha jifunze kuizalisha
Watu wengi hususani akina mama ambao hukopa pesa kwenye vikundi vya kuwezeshana aua katika taasisi za fedha baadhi yao wanapozipata huwa wanaanza kwa kununua vitu vya ndani kama runinga, makochi n.k na mwisho wa siku wanajikuta hawajaitumia hiyo fedha kuzalisha kitu chochote na hiki ndicho alichofanya mtumwa mmojawapo wa Yule tajiri, baada ya kupata fedha anasema alikwenda kuificha chini ya ardhi (Mathayo 25:25).

Chapisha Maoni

0 Maoni