Natumaini umewahi kuona misafara ya viongozi mbalimbali, vyombo vya usafiri vinavyokuwa kwenye misafara huwa vinatembea kwenda mbele kwa haraka na kasi.
Katika msafara ikitokea chombo kimojawapo cha usafiri (gari au pikipiki) kikataka kurudi nyuma au kusimama njiani wakati vyombo vingine vinaendelea na safari, BILA SHAKA KUTATOKEA AJALI NA MAAFA MBALIMBALI.
Kama misafara ilivyo ndivyo tulivyo sisi tunaomfuata Bwana Yesu, sisi tuko kwenye msafara kuelekea mbinguni, njia ya kwenda mbinguni ni Yesu mwenyewe (Yohana 14:6) kiongozi wa msafara ni Roho Mtakatifu.
Mtu yeyote anayerudi nyuma au ambaye anasimama huwa anajisababishia matatizo na kuwasababishia matatizo wengine ambao wako kwenye msafara.
JIFUNZE KWENYE MIFANO HII MADHARA YA KURUDI NYUMA
1. Mke wa Lutu (Mwanzo 19:15-38)
Wakati Lutu anatoka kule sodoma na familia yake waliambiwa wasisimame njiani pia wasitazame nyuma.
Mke wa Lutu alipogeuka nyuma akawa nguzo ya chumvi, alikatisha maisha yake.
Mke wa Lutu alisababisha mumewe kukosa mke (Kubaki mgane).
Lakini si hilo tu mabinti wa Lutu walilala na baba yao na wakapata mimba, kama mama yao angekuwepo nina uhakika wasingelala na baba yao.
Hayo yote yalitokea kwa kuwa kuna mtu aligeuka nyuma (alirudi nyuma aliacha kufuata jambo ambalo aliwaambia).
2. Mfalme Farao na jeshi lake (Kutoka 14:5-15)
Lengo la Mfalme Farao kuwafuata Waisraeli baada ya Waisraeli kuondoka pale Misri lilikuwa kuwarudisha tena nchini Misri ili waendelee kuwa watumwa.
Kumbuka Mungu aliwatoa nchini Misri ili waende kwenye nchi iliyojaa maziwa na asali (nchi iliyojaa mema).
Kama wangeamua kurudi nyuma nchini Misri wangeendelea kuwa watumwa wakati kuna nchi yenye mema ambayo alikuwa amewaandalia.
Wangerudi nyuma kule Misri, bila shaka wao na vizazi vyao wangeendelea kuwa watumwa.
3. Mfalme Sauli (1 Samweli 15:11)
Mfalme Sauli alirudi nyuma, aliacha kumfuata Mungu kutokana na kurudi nyuma kwake, Mungu alimkataa asiwe Mfalme wa taifa la Israeli na Mungu akaagiza Daudi apakwe mafuta ili aje kuwa Mfalme wa taifa la Israeli.
HITIMISHO
1. Fahamu kuwa shetani anatamani kukurudisha nyuma, akishindwa kukurudisha nyuma anatamani usimame usiendelee na safari ya kuelekea mbinguni.
2. Ukirudi nyuma utajisababishia matatizo wewe binafsi na watu wengine ambao mko nao kwenye safari moja (utasababisha matatizo kwenye kanisa, familia nakadhalika).
3. Ukirudi kurudi nyuma utakosa mema ambayo Mungu amekuandalia (utakosa mema ya hapa duniani ambayo amekuandalia na utakosa kuingia mbinguni).
4. USIKUBALI KURUDI NYUMA, USIKUBALI KUSIMAMA NJIANI, SONGA MBELE, kumbuka kuwa Mfalme Farao alipowafuata Waisraeli ili kuwarudisha nyuma MUNGU ALIWAAMBIA SONGENI MBELE (Kutoka 14:15).
5. USIKUBALI KIKWAZO KIKAKUFANYA USIMAME NJIANI AU USIENDELEE MBELE wakati yupo Mungu awezaye kuondoa vikwazo vyote.
Hata kama umekutana vikwazo njiani, hata kama vikwazo vimeinuliwa kwa ajili yako ili usiendelee mbele, mwambie Mungu akuondolee vikwazo hivyo na akusaidie uendelee mbele.
Kumbuka Mungu aligawanya bahari ya Shamu ili waendelee mbele (Kutoka 14:15-16).

0 Maoni