UTANGULIZI
Taifa la Yuda limewahi kuwa na Wafalme wengi sana lakini Mfalme aliyekuwa bora sana na wa pekee kuliko Wafalme wengine ni Mfalme Yosia (2 Wafalme 23:25).
Mfalme Yosia alianza kutawala akiwa na umri wa miaka nane (8), soma habari hiyo ya kushangaza kwenye (2 Wafalme 22:1).
Mfalme Yosia alikuwa mtoto wa Mfalme Amoni ambaye aliuawa (2 Wafalme 21:23) baada ya Mfalme Amoni kuuawa ndipo Yosia akawa Mfalme akapata nafasi ya baba yake (2 Wafalme 21:24).
Huyo ni Mfalme aliyefanya matengenezo (Reformation) makubwa sana katika taifa la Yuda, baadhi ya matengenezo aliyoyafanya ni pamoja na kukarabati nyumba ya Mungu na kuondoa miungu iliyokuwa inaabudiwa katika nchi.
MISINGI YA MATENGENEZO YA NCHI WAKATI WA UTAWALA WA MFALME YOSIA
1. NI KITABU CHENYE MANENO YA MUNGU AU MANENO YA MUNGU
(2 Wafalme 22:10-11)(2 Wafalme 23:1-2)
Kitabu cha torati (maneno ya Mungu) ndio yalikuwa msingi wa matengenezo makubwa ya nchi aliyoyafanya Mfalme Yosia.
Kwa mantiki hiyo ni kwamba Mungu alihusishwa kwenye matengenezo ya nchi, kwa sababu maneno yake ndio yaliyomchochea Mfalme Yosia kufanya matengenezo makubwa ya nchi kwenye utawala wake.
2. USHIRIKISHWAJI WA WADAU MUHIMU KATIKA MATENGENEZO YA NCHI
Mfalme Yosia alitambua wadau muhimu katika matengenezo ya nchi waliokuwepo nyakati zile ni viongozi wa dini, wazee na wataalamu mbalimbali. Alijiweka karibu na watu hao ili wafanye kazi pamoja kuhakikisha nchi inarudi katika hali nzuri.
HITIMISHO
Mfalme Yosia alifanya matengenezo katika taifa lake kwa kuwa alitendea kazi maneno ya Mungu pia alishirikisha wadau muhimu katika nchi. Hivyo basi kila anayekusudia kufanya matengenezo makubwa katika nchi yake ni muhimu ajifunze kupitia kisa hicho cha Mfalme Yosia (2 Wafalme sura ya 21 na 22).

0 Maoni