Mwl.Faraja Gasto
Hamasa ni nini?
Hamasa ni kitu kisichoonekana kwa macho kinachokusukuma
ujitoe kufanya jambo fulani kwa moyo wako wote, kwa nguvu zako zote, kwa akili
zako zote n.k. Hamasa hauwezi kuiona ila matokeo yake yanaweza kuonekana.
Hamasa ni kitu kikubwa sana ambacho kinaweza kusababisha
matokeo chanya na pia kama ikikosekana kuna uwezekano wa kupata matokeo hasi
katika jambo fulani.
Tabia tatu za hamasa
1.Huwa inaingia ndani ya mtu kwa njia mbalimbali.
2.Inaweza kuongezeka au kupungua.
3.Inaweza kutoweka kabisa kutegemeana na mazingira fulani
kama vile kuvunjwa moyo, kutoheshimiwa n.k.
Hamasa ni suala la kiroho, maana yake hamasa huwa inavuta
nguvu ya kiroho inayomfanya mtu ajitoe kuhakikisha amefanikisha jambo fulani.
Hamasa imetajwa kwenye Biblia kama “kuamsha
roho” unaposoma Biblia ukaona pameandikwa “Bwana akaamsha roho ya………………………” ufahamu kuwa Biblia inazungumzia
suala la hamasa, kwamba Mungu aliachilia HAMASA/ HAMASIKO ndani ya huyo mtu
ndio maana utaona kila mahali ambapo Mungu alipoziamsha roho utaona kuna kazi
ilikuwa inakwenda kufanyika. (Ezra 1:1)(Hagai 2:14)
Hamasa inaongeza nguvu
ndani ya mtu.
Kwa mfano, wachezaji wanapokuwa wanacheza huwa wanahitaji
hamasa, pamoja na mazoezi wanayofanya wakikosa hamasa lazima watashindwa tu,
washangiliaji ndio huwa wanawatengenezea wachezaji hamasa ya kujikaza ili
washinde. Kwa hiyo wachezaji na washangiliaji wote wana nafasi katika ushindi
wa timu.
NJIA BAADHI ZA
KUTENGENEZA HAMASA/HAMASIKO
1.Kutoa ahadi fulani na
kuitekeleza
(1 Samweli 17:25-32)
Tunaona Daudi aliposikia kuhusu zawadi atazopewa mtu
atakayemuua mfilisti, hamasa iliingia ndani yake akaamua kujitoa kwa ajili ya
kwenda kukabiliana na Goliathi.
Kwa mfano wanafunzi wengi wanaoshindwa (wanaofeli) mitihani
mara kwa mara shida mojawapo inayowafanya washindwe ni kukosa hamasa. Ukitaka
kuamini hili jaribu kulifanyia utafiti, kama una mtoto ambaye amekuwa
anashindwa mitihani jaribu kumuahidi kumpa zawadi endapo atafanya vizuri kwenye
mitihani ijayo, utakapomuahidi utashangaa ghafla ameanza kufanya jitihada za
kujisomea ili aweze kufanya vizuri kwenye mitihani, ninakuhakikishia mitihani
itakayofuata hatapata alama (marks) alizopata kwenye mitihani iliyopita.
2.Kutoa zawadi
Zawadi huwa inamtengenezea hamasa yule anayepewa zawadi,
anapopewa zawadi kwa kile alichofanya huwa inamtia hamasa ya kufanya kwa ubora
zaidi.
3.Kukubali uwezo wa mtu
na kumpongeza au kumshukuru
Jaribu kufikiri mtu unamsaidia halafu hajawahi kukushukuru,
utajikuta hamasa a kuendelea kumsaidia imepotea na hatimaye utaacha kabisa
kumsaidia. Kilichosababisha usindelee kumsaidia ni kwa sababu hamasa
imepotoweshwa na tabia yake ya kukosa shukrani.
Pia unapoukubali uwezo wa mtu ukampongeza kwa kiwango
alichonacho huwa inamtia hamasa ya kuongeza bidii ili aweze kufika viwango
vingine.
4.Kumtia mtu moyo kwa
njia ya kumpa ushuhuda unaoingiza hamasa ndani yake ya kufanya jambo fulani.
(Mathayo 6:25-34)
Yesu aliwatia hamasa wanafunzi kwa habari ya kuutafuta ufalme
wa Mungu na haki yake kwa kuwapa ushuhuda kuhusu ndege wa angani hawapandi wala
hawavuni lakini WANAKULA CHAKULA, tena akazungumza kwa habari ya maua ya
kondeni kwamba Mungu anayatunza. Yesu alichokuwa anakifanya ni KUWATIA HAMASA
ili wautafute ufalme wa Mungu na haki yake.
5.Kumjali mtu kwa
kumjulia hali, kumtembelea, kumuonyesha upendo n.k
(Matendo ya mitume 2:41-47)
Kanisa la kwanza watu walikuwa na hamasa kwa mambo ya ufalme
wa Mungu kwa sababu ya upendo mkubwa sana waliokuwa nao, jaribu kufikiri mtu
ameuza kiwanja chake akakupa wewe fedha ukafanyie mambo yako, unadhani
utajitenga na huyo mtu? HAIWEZEKANI, kinachokufanya uendelee kuwa karibu naye
ni HAMASA iliyoingia ndani yako kupitia upendo uliouona.
Mtu anapokata tamaa kwa ajili ya jambo fulani kwa mfano
watoto hawana ada ya shule, huwa anajikuta hata hamu ya ibada huwa inapotea,
ili apate moyo wa kuendelea kuja kusali lazima HAMASA iingie ndani yake. Kwa
mfano ukimpa pesa akalipie ada ya shule, hilo jambo litampa hamasa ya kuendelea
kusali maana ametiwa moyo.
Kanisa la sasa tumepoteza vitu vingi sana, ndio maana inafika
hatua watu wanakuja kanisani kwa kusuasua, mara leo yupo, kesho hayupo, wengine
inafika hatua wanaacha kabisa wokovu. Kitu kimojawapo kikubwa wanachokosa ni HAMASA
(motivation).
Daudi anaposema alifurahi walipomwambia twende nyumbani mwa
Bwana na akafurahia huo ujumbe ni HAMASA aliyokuwa nayo kutokana na kile
anachopata nyumbani mwa Bwana.
6.Kwa kuonyesha matokeo
ya hicho kilichopangwa au kilichokusudiwa kufanyika.
(Nehemi 2:17-18)
Biblia inasema kwamba Nehemia aliwaambai wayahudi wajenge
kuta za Yerusalemu na kuyatengeneza malango yake ILI WASIWE SHUTUMU (ili
wasiendelee kudhihakiwa au kudharauliwa). Kwa hiyo alimaanisha kwamba kujenga
kuta na kutengeneza malango kutasababisha wao wasidharauliwe na mataifa (hayo
ni matokeo ya kazi hiyo)
Kwa hiyo aliwaonyesha umuhimu wa kujenga kuta na
kuyatengeneza malango ya Yerusalemu ghafla hamasa ikaingia ndani yao wakapata
nguvu wakaanza kujenga.
7.Kiongozi kuwa mstari
wa mbele katika mambo yote
(1 Timotheo 4:11-12)
Mtume Paulo alimkumbusha Timotheo kwamba mambo
aliyomwambia ayaagize na kuyafundisha il awe kielelezo kwao waamini katika usemi
na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.Kiongozi anapokuwa mstari wa mbele katika mambo yote
huwa inawapa hamasa hata wale anaowaongoza, lakini kama kiongozi hayuko mstari
wa mbele katika mambo yote hata anaowaongoza hawawezi wakahamasika kufanya
chochote.
Kwa mfano kama kiongozi akiwa mstari wa mbele katika kutoa
michango, katika maombi, katika kujifunza n.k huwa inawatia hamasa anaowaongoza
ili wafanye kama anavyofanya kiongozi wao.
UHUSIANO ULIOPO KATI YA
KUONA NA KUHAMASIKA
Hamasa pia inapatikana kwa kuona, mtu akiona jambo fulani
limetendeka huwa anahamasika kufanya ili apate matokeo ambayo mwingine
aliyapata.
Kwa mfano kama watu wanachanga pesa halafu hawaoni matokeo ya
hiyo pesa iliyochangwa au kazi ya hiyo pesa iliyochangwa, watu huwa wanajikuta
wamekosa hamasa ya kuchanga pesa zingine maana hawaoni kazi ya hiyo pesa lakini
kama wanaona kilichofanyika huwa wanaendelea kujitoa maana wanaona kazi
inafanyika.
Biblia inasema “tawi lizaalo husafishwa ili lizidi kuzaa”-(Yohana
15:1-2) maana yake ni sawa na kusema kwamba mkulima anapoona zao fulani
linasitawi sana huwa haachi kupalilia na kuwekeza kwenye zao hilo maana linazaa
na linamletea faida lakini kama haoni matunda yoyote basi hamasa ya kuendelea
kulima zao hilo itatoweka.
Jaribu kufikiri mzazi ambaye ana watoto watatu wanaosoma,
halafu mmoja akawa anafanya vizuri kuliko wengine lazima atajikuta anakuwa
karibu na anamjali yule anayefanya vizuri kwa sababu anaona matokeo yake, kwa
hiyo yale matokeo anayoyaona ndio yanampa hamasa zaidi ya kuwa karibu na
huyo mtoto na kuwekeza fedha za kutosha
ili asome vizuri.
Mungu akubariki kwa kujifunza, japo nimekupa angalau kwa sehemu somo hili ili liweke kitu ndani yako.
0 Maoni