BAADHI YA SABABU KWA NINI HUPASWI KUWATEGEMEA WANADAMU



1. Kila anayetegemea wanadamu amelaaniwa.

(Yeremia 17:5)

2. Wanadamu wanakufa

Wafilisti walimtegemea Goliathi akauawa hatimaye wote walikimbia kwa kuwa tegemeo lao halipo, familia ya Mzee Yakobo (Israeli) walimtegemea Yusufu kwa kuwa alikuwa mfanyakazi katika serikali ya Misri , Yusufu aliwaombea kwa Mfalme Farao ili wapate pa kulishia mifugo yao Mfalme Farao alikubali hilo ombi (Mwanzo 47:1-11) lakini ilifika hatua Yusufu akafa Kisha akaanza kutawala Mfalme Farao asiyemjua Yusufu, maisha ya wana wa Israeli yalianza kuwa magumu yenye mateso makali kwa kuwa ambaye angeweza kuwasema au kuwakingia kifua hayupo.

Unayemtegema akifa utahangaika sana ila kama unamtegemea Mungu asiyekufa huwezi kutikiswa na chochote "Wamtumainio Bwana ni kama mlima Sayuni, Ambao hautatikisika, wakaa milele" (Zaburi 125:1).

3. Watu wanabadilika na kubadilishwa.

Kuna wazazi wanajikuta wakiwa na uchungu kwenye mioyo kwa kuwa walitegemea watoto wao watawasaidia baada ya watoto wao kufanikiwa lakini watoto wao wamewasahau na hawajali wazazi.

Hupaswi kuwategemea watu bali Mungu tu kwa kuwa wanadamu wanabadilika na wanabadilishwa.

4. Watu wengine hujipenda wenyewe.

Yusufu alimtafsiria ndoto mtu fulani na akamwambia yule mtu ukipata mema unikumbuke lakini yule mtu alimsahau Yusufu (Mwanzo 40:9-15)

Usiwategemee wanadamu usiweke tumaini kwa wanadamu kwa kuwa watu hujipenda wenyewe.

HITIMISHO

Hata kama una watu wa kukusaidia au kukufanikishia mambo yako usiwategemee mtegemee Mungu tu kwa kuwa wanadamu wanakufa ila Mungu hafi, wanadamu wanabadilika na kubadilishwa ila Mungu habadiliki na habadilishwi, wanadamu hujipenda wenyewe ila Mungu anatupenda sisi wote.

Mordekai alimwambia Malkia Esta kwamba "Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo? (Esta 4:14).

Maana yake ni kwamba Mordekai hakuweka tumaini kwa Esta kwa kuwa Esta ni Malkia na mwanaye aliyemlea bali alimtegemea Mungu ambaye angeweza kuwaokoa wayahudi kwa njia nyingine hata kama Malkia Esta asingejihusisha na suala la wayahudi.

Chapisha Maoni

0 Maoni