(Nehemia 9:17)
"na katika kuasi kwao wakaweka JEMADARI, ILI WAIRUDIE HALI YA UTUMWA"
UTANGULIZI
Musa alikuwa akikwea mlimani ili kusemezana na Mungu juu ya mambo mbalimbali.
Wakati fulani alipanda mlimani akachelewa kurudi, wana wa Israeli walipoona Musa amechelewa kurudi wakakusanyana ili wapate kiongozi mwingine atakayewarudisha kule Misri, kiongozi huyo ndiye anaitwa JEMADARI WA UTUMWA yaani kiongozi anayewarudisha watu utumwani kwenye mateso (Nehemia 9:17).
Hivyo basi ninapoongelea jemadari wa utumwa naongelea viongozi ambao wanawarudisha watu kwenye utumwa au kwenye mateso kwa njia mbalimbali.
BAADHI YA MAJEMADARI WA UTUMWA
1. Mfalme Farao aliyetawala baada ya Yusufu kufariki.
(Kutoka 1:6-14)
Mfalme aliyepita alihakikisha wananchi wanaishi vizuri lakini alipoingia Mfalme mpya, alihakikisha wana wa Israeli wanaishi maisha magumu sana.
IKO HIVI: Kiongozi wa taifa lolote au mtawala wa nchi akihakikisha kunakuwa na sheria kandamizi, uvunjaji wa haki za binadamu na mazingira yasiyo rafiki ya kiuchumi, kiongozi huyo au mtawala huyo ni jemadari wa utumwa, anawarudisha watu kwenye utumwa na mateso.
2. Serikali nyingi za nchi za bara la Afrika.
Serikali nyingi za nchi za bara la Afrika ni majemadari wa utumwa kwa kuwa hazina upendo wa dhati na wananchi, serikali nyingi hutumia madaraka yao kujinufaisha wenyewe na kunufaisha watu wachache wakati wengi wanaumia.
Afrika kuna sheria nyingi kandamizi, uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu, matatizo mbalimbali ya kitaasisi na kijamii na mazingira ya kiuchumi yasiyo rafiki ambayo yanapelekea maisha ya wananchi kuwa mabaya, japokuwa haina maana kwenye mataifa yaliyo nje ya Afrika hayana matatizo.
3. Mfalme Rehoboamu (mtoto wa Mfalme Sulemani)
(1 Wafalme 12:1-14)
Mfalme Rehoboamu hakuwa na majibu mazuri kwa wananchi, hakuwatumikia wananchi hatimaye watu waliasi serikali yake.
Rehoboamu alikuwa na mpango wa kuwarudisha wana wa israeli kwenye utumwa (1 Wafalme 12:11).
HITIMISHO
Ili uwe kiongozi au mtawala ambaye unapendwa na kukubalika kwa wananchi, kiongozi au mtawala ambaye hautawarudisha utumwani wananchi;-
1. Kubali kuwatumikia watu, wape watu majibu mazuri ya maswali waliyonayo, tatua matatizo ya watu(1 Wafalme 12:7).
2. Penda watu, pambania maisha yao (1 Samweli 22:2)
0 Maoni