(Nehemia 9:17)
"na katika kuasi kwao wakaweka JEMADARI, ILI WAIRUDIE HALI YA UTUMWA"
UTANGULIZI
Musa alikuwa akikwea mlimani ili kusemezana na Mungu juu ya mambo mbalimbali.
Wakati fulani alipanda mlimani akachelewa kurudi, wana wa Israeli walipoona Musa amechelewa kurudi wakakusanyana ili wapate kiongozi mwingine atakayewarudisha kule Misri, kiongozi huyo ndiye anaitwa JEMADARI WA UTUMWA yaani kiongozi anayewarudisha watu utumwani kwenye mateso (Nehemia 9:17).
Ninapoongelea jemadari wa utumwa naongelea mtu au watu wanaokurudisha utumwani au wanaokusababishia matatizo pia naongelea mambo au vitu vinavyowarudisha au vinavyowapeleka watu utumwani, kwenye mateso au kwenye matatizo.
BAADHI YA MAJEMADARI WA UTUMWA
1. ANASA NA DHAMBI ZINGINE.
(Luka 15:11-16)
Huyo kijana ambaye habari yake imeandikwa kwenye andiko hilo aliomba urithi kwa babaye, babaye akampa mali, baada ya siku si nyingi aliondoka kwa babaye ili awe huru kuishi anavyotaka.
Biblia inasema alitumia zile mali kuishi maisha ya anasa hatimaye mali zilikwisha akaishia kuishi mabaya.
Anasa ndizo zilikuwa jemadari wa utumwa wa huyu kijana.
Zinaa, uasherati, ulevi, matumizi ya madawa ya kulevya nakadhalika vimesababisha watu kuwa masikini na kupata matatizo ya aina mbalimbali, dhambi ni jemadari wa utumwa.
2. MATUMIZI MABAYA YA FEDHA NA MALI.
Pale inapotokea matumizi yakawa makubwa kuliko mapato ni rahisi mtu kuingia kwenye madeni nakadhalika, pale inapotokea mtu akawa na tabia ya kutumia tu bila kuweka akiba atajikuta kwenye mahangaiko siku za usoni.
Matumizi mabaya ya fedha na mali ni pamoja na kuwa na matumizi makubwa kuliko mapato.
Matumizi mabaya ya fedha na mali ni pamoja na kutumia tu bila kuweka akiba.
(Mithali 6:6-8) Biblia inaeleza kuhusu mdudu aitwaye chungu huwa hatumii mapato tu bali huwa anatumia kidogo na kuweka akiba kwa ajili ya wakati ujao.
3. UVIVU WA KUTOFANYA KAZI ZA MIKONO.
kwa mujibu wa Biblia mtu yeyote asiyetaka kufanya kazi, anaitwa mvivu (Mithali 21:25).
Mvivu anapenda kutumia vya wengine kwa kuwa yeye hana kitu, anasubiri kuletewa tu (Mithali 12:27).
(Mithali 6:9-11) Biblia inasema mtu mvivu hujikuta kwenye umasikini, umasikini unatesa pia unaweza kuathiri maisha ya watu kwa viwango vikubwa sana.
4. MARAFIKI WABAYA.
Marafiki wabaya ni marafiki wanaokushauri vibaya au marafiki wenye tabia mbaya.
Mtu yeyote mwenye marafiki wabaya au mtu yeyote anayeambatana na marafiki wabaya ataishia kwenye mateso na matatizo.
Aina mojawapo ya marafiki ambao tunatakiwa kujitenga nao ni wale wanaowahi kukasirika au kughadhibika (Mithali 22:24).
Hiki ndicho Biblia inasema kuhusu mtu mwenye hasira sana.
"Mtu wa hasira huchochea ugomvi; Na mtu mwenye ghadhabu huasi sana"
Ukiambatana na mtu huyo utaishia kupata hasara, mateso na matatizo, marafiki wabaya ni majemadari wa utumwa.
HITIMISHO
Unaweza kuepuka utumwa au mateso au matatizo mbalimbali kwa kuepuka hao majemadari wa utumwa.
Usikubali kurudi utumwani kwa kujiweka chini ya utawala wa hao majemadari wa utumwa.
Jiweke chini ya jemadari mwema ambaye ni Mungu mwenyewe, lishike neno lake na ishi kwa kufuata neno lake na kubali kuongozwa na Roho Mtakatifu UTAKUWA HURU KWELIKWELI, UTAPATA AMANI NAKADHALIKA.
0 Maoni