MAMBO YA KUFANYA ILI KUEPUKA KAZI YA KUOMBEA NDOA MARA KWA MARA


✍Faraja Gasto

IKUHIZI KUNA MAKUTANO YA MAOMBI YA KUOMBEA NDOA, sio vibaya ila kabla haujaombea ndoa yako nikukumbushe yafuatayo.

1. Hakikisha unamtendea mwenza wako haki, ikiwemo ile haki iliyoandikwa katika 1 Wakorintho 7:3-5.

2. Hakikisha unatimiza wajibu wako kwa mwenza wako, mke umtii mumeo KAMA KUMTII BWANA (Waefeso 5:22-23)(1 Petro 3:1-6) mstahi mumeo au mfichie aibu mumeo au usifanye jambo litakalosababisha mumeo aaibike (Waefeso 5:33) mume umpende mkeo na umpe heshima (Waefeso 5:25)(1 Petro 3:7).

3. Hakikisha kwa namna yoyote haushiriki kudhoofisha au kuangamiza ndoa yako, usiombee ndoa kwa kinywa chako huku unaivunja kwa mikono yako (Mungu hadhihakiwi), hakikisha kinywa na mikono yako vishirikiane kulinda ndoa yako, usiache umepanda mbegu mbaya ndani ya mumeo au mkeo halafu ukaenda kuiombea ndoa yako, ulichopanda utavuna (Wagalatia 6:9).

4. Jitenge na ushauri wa wazazi, ndugu, marafiki na jamii unaolenga kuua ndoa yako HAKIKISHA MSHAURI WA NDOA YAKO NI MUNGU (NENO LAKE NA WATUMISHI WAKE).

-Si kila wakati ushauri wa wazazi ni mzuri (kumbuka nao ni wanadamu tu), wanaweza kukupa ushauri kwa kukuonea huruma ila wanaua ndoa yako bila hata wao kujua, uwe na akili.

Biblia inatambua kuna mashauri mabaya (Mithali 15:26)(Ezekieli 11:2) kwa hiyo uwe makini na ushauri unaopewa.

5. Kila mwanamume kuna namna anavyopenda, usitake kupendwa katika namna anavyopendwa jirani yako au ndugu yako au mama yako, NAMNA ZA KUPENDA ZINATOFAUTIANA, kubaliana na namna mumeo anavyopenda ITAKUPUNGUZIA MSONGO WA MAWAZO NA MIFUNGO ISIYO YA LAZIMA.

Mzungu akipewa maua anatafsiri ni ishara ya upendo, je! sisi waafrika tukipewa zawadi ya maua tunatafsiri ni upendo? au mpaka tupewe pesa nakadhalika.

6. Hakikisha unakuwa mwepesi wa kukubali makosa yako na kujirekebisha endapo utakosea, refa wa ndoa ni Mungu hivyo basi tulitumie neno la Mungu kujisahihisha ili kuepuka mifungo isiyo ya lazima ya kuombea ndoa, usimpe mtu yeyote nafasi ya kuwa refa wa ndoa yako ILA MUNGU TU.

7. Kabla haujaingia kwenye ndoa FUMBUA MACHO YAKO pia INGIA UKIWA NA AKILI TIMAMU, usiingie kwenye ndoa ukiwa umefumba macho au ukiwa umepagawa na kinachoitwa mapenzi, umbo la mwanamke, muonekano wa mwanamume, kazi ya mwanamke au mwanamume. 

Mwanamke usiingie kwenye ndoa huku akili umeziacha nje ya ndoa, akili zitahitajika mbele ya safari (Tito 2:4)

Mwanamume, usiingie kwenye ndoa huku umeacha akili zako nje ya ndoa kwa kuwa akili zitahitajika mbele ya safari ndio maana imeandikwa "kaeni na wake zenu kwa akili" (1 Petro 5:7).

Unamkumbuka Yakobo mtoto wa mzee Isaka ambaye habari zake zimeandikwa kwenye kitabu cha MWANZO 29:15-28.

Yakobo alimpenda Raheli ila siku ya arusi akalala na Lea, yaani ni sawa na kusema unafunga ndoa kanisani na ANA ila unajikuta usiku umelala na ROSE, cheka kidogo 🤣🤣🤣🤣🤣🤣.

Ilipofika asubuhi ndipo Yakobo aligundua  kuwa amelala na mtu ambaye hakuwa sahihi, ILIMBIDI AOE WOTE WAWILI (RAHELI NA LEA).

IKO HIVI: Usijifanye bingwa wa kupenda, mapenzi haujayaanza wewe, KAMA UMEBAINI MTU ANAYETAKA KUKUOA AU UNAYETAKA KUMUOA SIO SAHIHI ACHANA NAYE KABLA HAUJAMUOA AU KABLA HAJAKUOA, hiyo itakuepushia maombi ya kufunga ambayo sio ya lazima huko mbele ya safari.

Mungu ameruhusu tuzijaribu (tuzichunguze) roho kama zimetokana na Mungu, kama tumeruhusiwa kuzichunguza roho kwa nini tusichunguze mambo ya kimwili? usiache kumchunguza mtu anayetaka kukuoa au unayetaka kumuoa (nendeni hospitali mkapime afya zenu, fahamuni historia zenu na za familia zenu) ILA KAMA UTASEMA MUNGU AMEKUAMBIA UMUOE AU UOLEWE NA HUYO MTU MTAJUANA NA MUNGU ila nimekutahadharisha.

8. Kabla haujamuombea mmeo au mkeo HAKIKISHA UMEMSAMEHE  (Marko 11:25)

NB: 

1. Wazee wetu hapo zamani hawakuwahi kuwa na makongamano ya kuombea ndoa ILA NDOA ZILIDUMU (haina maana walikuwa hawana migogoro au kuhitilafiana) ilikuwepo lakini ndoa zilidumu kwa kuwa WALIZINGATIA MAAGIZO NA KANUNI ZA MUNGU ZA NDOA, simaanishi tuache makongamano ya kuombea ndoa zetu ila ninachoamini ni kwamba KAMA WANANDOA WATAZINGATIA MAAGIZO NA KANUNI ZA MUNGU KUHUSU NDOA HATUTAKUWA NA MAKONGAMANO YA KUOMBEA NDOA.

2. Wazee wetu wengi hapo zamani hawakufunga ndoa kanisani au msikitini ila ndoa zao zilidumu kwa kuwa WALIZINGATIA MAAGIZO NA KANUNI ZA MUNGU ZA NDOA, sijasema msifunge ndoa makanisani ila nafundisha misingi ya ndoa.

3. Fundi na refa mzuri wa ndoa ni Mungu, wanandoa wakijitenga na Mungu WAMEKWISHAAAAAAA.

Chapisha Maoni

0 Maoni