✍Faraja Gasto
Lengo la kujifunza jambo hili ni ili tujue namna ya kubaini vyanzo vya matatizo yanayoendelea au yanayotokea kwenye maisha yetu kwa kuwa hatuwezi kupata ufumbuzi wa matatizo bila kujua vyanzo vya matatizo.
UTANGULIZI
Yako matatizo ambayo yanaendelea kwenye maisha ya watu, kwenye familia, kwenye koo, kwenye nchi nakadhalika.
Mara nyingi watu hupambana na matokeo ya tatizo badala ya kushughulikia vyanzo, kwa mfano ukikata matawi ukaacha shina lazima huo mti utachanua tena, ila uking'oa shina na mizizi yake huo mti ndio utakuwa mwisho wake.
BAADHI YA MIFANO YA WATU WALIOPAMBANA NA MATOKEO BADALA YA CHANZO CHA MATOKEO HAYO
1. Wasafiri waliokuwa wanaenda Ninawi.
(Yona 1:1-14) Walipoona dhoruba inatokea walitupa mizigo baharini wakidhani kuwa jambo hilo litaifanya merikebu iwe nyepesi isizame lakini kutupa mizigo baharini haikuwasadia chochote.
Walikuwa wanapambana na matokeo ya tatizo badala ya kushughulika na chanzo cha tatizo ambacho ni Yona.
Chanzo cha ile dhoruba haikuwa upepo bali ni abiria waliyembeba ambaye ni Yona alikuwa anamkimbia Mungu.
Walipojua chanzo cha kukishughulikia, bahari ilitulia (Yona 1:15).
2. Balaamu
(Hesabu 22:22-35)
Balaamu alidhani kumpiga punda itasababisha punda aache kumwangusha lakini tatizo lile halikuisha.
Hapa nataka nichomeke jambo hili; usidhani kumpiga mtoto mara kwa mara ndio itakuwa dawa ya tatizo la mtoto, nimewahi kuona wazazi fulani wakimpiga mtoto mara kwa mara kwa kuwa mtoto wao alikuwa anajinyea na kujikojolea mara kwa mara lakini fimbo haikumaliza tatizo lile.
Ni kweli fimbo au mapigo yana nafasi yake katika kuadibisha watoto lakini si kila wakati fimbo itakuwa dawa ya matatizo ya mtoto.
Mungu alipomfungua Balaamu macho akaona malaika ndipo alibaini chanzo cha punda kumwangusha Balaamu ni malaika aliyesimama njiani.
3. Mfalme Daudi.
(2 Samweli 21:1) Kulikuwa na njaa kwenye nchi kwa miaka mitatu.
Ndani ya muda wote serikali ilitafuta ufumbuzi wa tatizo lakini hawakupata ufumbuzi.
Kwa mfano kuna wakati fulani kwenye nchi ya Tanzania palikuwa na uhaba wa sukari ilibidi serikali iagize sukari kutoka nje ya nchi, wakati huohuo serikali ilikuwa inawakamata walioficha sukari na wale wanaouza sukari kwa bei ambayo serikali haikupanga, hiyo yote ilikuwa mikakati ya kuhakikisha nchi inakuwa na sukari.
Vivyo Mfalme Daudi na serikali walifanya jitihada za kuhakikisha nchi inaondokana na njaa lakini tatizo lile halikuisha mpaka Mungu alipomuambia Mfalme chanzo cha tatizo lile (2 Samweli 21:1).
MAMBO YATAKAYOKUSAIDIA KUJUA VYANZO VYA MATATIZO MBALIMBALI (YA KWAKO BINAFSI, YA FAMILIA, UKOO, NCHI NAKADHALIKA)
1. Omba Mungu akufungue macho ili uweze kuona katika roho (kuona yanayoendelea kwenye ulimwengu wa roho).
Ukweli ni kwamba kuna mambo hayaonekani kwa macho haya ya kimwili mpaka kutumia vifaa maalumu kama vile mashine za mionzi kama x-ray, CT scan, wakati mwingine watu hutumia darubini (microscope).
Mambo mengine huwezi kuyaona kwa x-ray, CT scan, microscope nakadhalika, mengine yanaonekana kwa jinsi ya rohoni lazima macho yako yaone kwa jinsi ya rohoni.
(Hesabu 22:22-35)
Balaamu hakujua chanzo cha ajali kwenye safari ni malaika aliyesimama njiani kumpinga, alipofunguliwa macho ndipo alipobaini chanzo cha tatizo lile.
Haya ni mambo baadhi yatakayokusaidia kuona katika roho; jizoeze kujifunza neno la Mungu kwa kuwa vitu vyote vi wazi mbele ya neno la Mungu (Waebrania 4:12-13) pia jizoeze kuomba Mungu akufungue macho ili uweze kuona ambavyo kwa macho ya kimwili huwezi kuona (2 Wafalme 6:17)
2. Kumtafuta BWANA.
-Kumtafuta BWANA ni kuacha mambo yako kwa ajili ya kumuomba Mungu au ni kutenga muda maalumu kwa ajili ya kuomba na kumuuliza Mungu kuhusu mambo mbalimbali.
(Yoshua 7:1-26)(Yoshua 8:1-29)
Jeshi la Israeli lilipigwa na Jeshi la Ai, jambo hilo lilimuhuzunisha sana Yoshua.
Yoshua hakujua katikati yao kuna tatizo, Yoshua akaamua kumtafuta Mungu, ndipo Mungu alipomwambia Yoshua chanzo cha Jeshi la Israeli kupigwa kule vitani.
(2 Samweli 21:1) Kama Mfalme Daudi asingemtafuta Mungu asingejua chanzo cha tatizo la njaa kwenye nchi yake.
3. Waendee wataalamu.
Kuna matatizo mengine Mungu ameshawapa watu maarifa ya kuyatatua na kuyatibu, kwa mfano kuna wakati sikio langu la kushoto lilikuwa linavimba mpaka likawa kubwa nikaenda hospitali fulani nikapewa dawa ikanisaidia kwa muda fulani lakini tatizo likarudi tena ikabidi niende hospitali nyingine kuonana na mtaalamu wa masikio na koo, akanichunguza kisha akaniandikia dawa za kutumia, nilipotumia zile dawa nikapona kabisa tatizo halikurudi tena, nilikutana na mtu anayejua chanzo cha tatizo lililokuwa linanisumbua.
4. Kufanya vikao au kusemezana.
- Ukweli ni kwamba kuna matatizo mengine yatapata ufumbuzi kwa kusemezana au kufanya vikao.
(Yona 1:1-14) tatizo lililowapata wasafiri hawa walipata ufumbuzi wake kwa kusemezana au kufanya vikao.
5. Kujua historia yenu (familia ya historia, ukoo wenu, kabila lenu nakadhalika).
-Ukweli ni kwamba kuna matatizo mengine ni ya kurithi yanatoka kizazi mpaka vizazi vingine, hili hata wanasayansi wanalikubali, kuna matatizo mengine yanatokana na laana.
Kwa mfano Kaini aliwahi kuua mtu, tunaona kwenye uzao wake kuna kitukuu chake aliyeitwa Lameki naye aliua mtu (Mwanzo 4:23-24)
Kwa mfano ukisoma Biblia utagundua kuwa kuzaa kwa uchungu ni matokeo ya laana, kila mwanamke ili azae lazima awe na uchungu.
Hivyo kujua historia kutakusaidia kubaini vyanzo vya matatizo na utakuwa na mwanga au mahali pa kuanzia kushughulika na matatizo husika.
HITIMISHO
Huwezi kupata ufumbuzi wa tatizo lolote hapa duniani kama haujui chanzo cha tatizo.
Kujua chanzo cha tatizo ni hatua ya kwanza ya kuelekea kwenye kupata ufumbuzi wa tatizo.
0 Maoni