NAMNA YA KUUTOKOMEZA UKRISTO
UTANGULIZI
Kumekuwepo jitihada mbalimbali zilizofanywa na watu mbalimbali kwa lengo la kutokomeza ukristo usiwepo, JITIHADA HIZO NI PAMOJA NA KUTESA NA KUWATISHIA WAKRISTO WASIHUBIRI INJILI AU WASITOE MAFUNDISHO KUHUSU UKRISTO (Matendo ya Mitume 4:17-18, Matendo ya Mitume 8:3) na KUUA WAKRISTO (Matendo ya Mitume 12:1-5). Ninapozungumzia ukristo nazungumzia ufuasi au kumfuata Yesu Kristo na imani ya kikristo kwa ujumla.
Baadhi ya watu waliofanya jitihada za kuutokomeza ukristo ni pamoja na Mfalme Herode na Sauli anayejulikana kwa wengi kama Mtume Paulo, yule mwandishi wa nyaraka kadhaa zinazopatikana kwenye vitabu vya agano jipya kama vile waraka kwa Wakorintho, Wakolosai, Wathesalonike nakadhalika.
Pamoja na jitihada hizo kufanyika, ukristo bado unaendelea sana japo umedhibitiwa kwa kiasi Fulani kwenye baadhi ya maeneo na nchi baadhi lakini ukristo bado upo na unaendelea kushamiri.
KWA NINI UKRISTO HAUJATOKOMEZWA?
Jitihada za kuutokomeza ukristo hazijawahi kuzaa matunda kwa sababu waliotaka kuutokomeza ukristo hawakulijua jambo hili au kama walilijua basi hawakulitilia maanani.
JAMBO HILO NI HILI “huwezi kutokomeza ukristo kwa kuua wakristo kwa kuwa wakristo ni MATAWI TU” Yohana 15:1-5. Kila anayetaka kuhakikisha mti au miti inatokomea huwa anang’oa shina au mashina, ukikata matawi ukaacha shina lazima huo mti utachanua kwa kuwa utatengeneza matawi mengine kwa hiyo KUUA WAKRISTO NI SAWA NA KUKATA MATAWI TU.
NAMNA YA KUUTOKOMEZA UKRISTO
Ili mtu yeyote aweze kuutokomeza ukristo lazima ang’oe shina (LAZIMA AMUUE YESU KRISTO)
Kutokomeza ukristo ni mojawapo ya kazi ngumu sana, ni kazi ya kujichosha, kupoteza muda na kujiumiza.
Sauli wakati anafanya harakati za kutokomeza ukristo aliambiwa “HUWEZI KUUPIGA TEKE MCHOKOO” Matendo ya Mitume 26:14
MCHOKOO NI NINI?
Zamani wakulima walipokuwa wanakwenda kulima na wanyama, hususani ng’ombe, walikuwa wanajua kuwa watakumbana na upinzani wa baadhi ya hawa wanyama, wakati mwingine wapo ng’ombe wenye viburi, ambao walikuwa hawataki kulimishwa, hivyo basi kila wakati walikuwa wanarusha mateke yao tu, na kuwasumbua sana wakulima.
Kwa hiyo wakulima wakabuni kitu mifano wa mkuki ambacho walikisogeza karibu kabisa na migongo ya ng’ombe, ambacho kilikuwa na ncha kali, ng’ombe akitaka kugeuka na kupiga mateke, alikutana nacho na kilimchoma, Hivyo basi kutokana na kuwepo kwa hicho kitu, ng’ombe alikuwa analima kwa utulivu hata kama hataki kulima.
Kazi ya kutokomeza ukristo ni kazi ngumu sana, ni kama kuupiga teke mchokoo, ukiupiga teke mchokoo huwezi kubaki salama lazima uumie.
HITIMISHO
Naamini kufikia hapo umeelewa kabisa hakuna anayeweza kuufutilia mbali ukristo kwa kuwa wakristo ni matawi tu, shina ni Yesu Kristo ambaye ANAISHI MILELE, ALIKUFA AKAFUFUKA, YUKO HAI MILELE.
Sauli aaliyehakikisha ukristo unatokomea aliishia kumwamini huyu Yesu Kristo hatimaye yeye mwenyewe akawa mhubiri wa injili, kama haujamwamini Yesu Kristo mwamini sasa maana yeye ndiye njia, kweli na uzima (Yohana 14:6).
0 Maoni