JINSI WATU WANAVYOMPA SHETANI NAFASI


(Waefeso 4:27) 

UTANGULIZI 

KUMPA SHETANI NAFASI NI

1. Kumpa shetani idhini ya kufanya kazi zake.

2. Kumfungulia shetani mlango atakaoutumia kufanya kazi zake.

3. Kumtengenezea shetani njia au mazingira rafiki kwa ajili ya kutenda kazi zake.

Jambo pekee ambalo shetani huwa anatafuta ni nafasi au fursa (an opportunity) ya kufanya kazi zake.

Ili shetani aweze kuua, kuiba na kuharibu lazima apate nafasi au fursa.

Tangu mwanzo shetani alipotaka kuharibu maisha ya mtu,  kumtenga mtu mbali na Mungu na kuingiza mambo ya kishetani ulimwenguni ALITAFUTA NAFASI kupitia mwanamke ambaye alimdanganya hatimaye yule mwanamke akamsababishia mumewe matatizo, mwanamke alimpa shetani nafasi kwa kumsikiliza, mwanamume alimpa shetani nafasi kwa kumsiliza mkewe, Soma kitabu cha Mwanzo Sura ya tatu.

Neno la Mungu linaposema tusimpe shetani nafasi maana yake ni kwamba hilo ni katazo, hatupaswi kumpa nafasi kwa kuwa akipata nafasi huua, huiba pia huharibu (Yohana 10:10).

JINSI WATU WANAVYOMPA SHETANI NAFASI

1. KUTOKUOMBA 

Kutokumuomba Mungu ni kumtengenezea shetani mazingira ya kufanya kazi zake.

Unapaswa kufahamu kuwa mbinu mojawapo ya kumzuia shetani kutenda kazi zake ni kumuomba Mungu.

Biblia inahimiza kuomba kila siku (Luka 18:1)(1 Wathesalonike 5:17)

Ukitaka kumzuia shetani asitende kazi zake kwenye mtaa, taifa, mahali pa kazi nakadhalika LAZIMA UMUOMBE MUNGU.

2. MANENO MABAYA

Maneno mabaya ni pamoja na mazungumzo mabaya (1 Wakorintho 15:33) kukiri mambo mabaya (Hesabu 13:32-33)

Ikiwa hautaki kumpa shetani nafasi basi epuka maneno mabaya.

3. MAWAZO MABAYA NA KUTENDEA KAZI KILA WAZO UNALOPEWA AU LINALOINGIA MOYONI MWAKO

Mawazo mabaya ni mawazo yote ambayo yako kinyume na neno la Mungu.

Ukweli ni kwamba huwezi kujizuia kuwaza ila unaweza kuzuia mawazo mabaya yasikae kwenye moyo wako.

Mawazo mabaya ni mlango wa shetani kufanya kazi zake.

Shetani aliyatumia mawazo mabaya kutaka kuzuia Yesu asife msalabani, aliyaweka mawazo hayo ndani ya Mtume Petro, Yesu angeyakubali yale mawazo ya Petro basi Yesu asingekuwa mwokozi wa ulimwengu (Mathayo 16:23)

Hivyo basi ukitaka kumnyima shetani nafasi hakikisha mawazo mabaya hayakai moyoni mwako pia hakikisha hautendei kazi kila wazo unalopewa au linaloingia moyoni mwako.

4. HASIRA

(Waefeso 4:26) ukweli ni kwamba kila mwanadamu huwa anakasirika ila kuna uwezekano wa kujizuia usitende dhambi baada ya kukasirika.

Hasira ni jambo mojawapo linaloweza kumpa shetani nafasi endapo aliyekasirika atakosa umakini.

Hasira ilisababisha Kaini akamuua nduguye Habili (Mwanzo 4:5-7)

Ukikasirika usifuate msukumo ulioletwa na hasira ikiwa baada ya kukasirika unapata msukumo au ari ya kutukana, kupigana, kujeruhi, kuua nakadhalika Usitendee kazi msukumo huo.

5. KUPITIA WANAYOTAZAMA

Hapa nazungumzia filamu, tamthilia nakadhalika.

Ili usimpe shetani nafasi lazima uepuke kutazama baadhi ya filamu, tamthilia, vipindi vya televisheni nakadhalika.

Kwa mfano watu wanaotazama video za uchafu kama ponografia (ponography) huwa wanaingiwa na pepo wachafu pia huwa wanashambuliwa na pepo wachafu kwa kuwa wamempa shetani nafasi kupitia macho yao.

Kwa mfano wengine wakitazama video zenye mambo ya kutisha huwa hawalali usiku kwa amani, wengine hujikuta wameingiwa na roho ya hofu kwa kuwa roho ya hofu iliwaingia kupitia waliyoyatazama.

HITIMISHO

Watu humpa shetani nafasi kwa njia mbalimbali, baadhi ni hizo nilizofundisha.

Hivyo basi ili usimpe Ibilisi nafasi lazima uyajue mambo hayo na ujifunze zaidi kwenye Biblia.


 

Chapisha Maoni

0 Maoni