BAADHI YA MIFANO KUHUSU NAMNA SHETANI HUTUMIA VINYWA VYA WATU KUFANYA VITA
1. Shetani alitumia kinywa cha Hawa kufanya vita na Adamu, Adamu alipomsikiliza mkewe maisha yao yakaharibika kabisa (Mwanzo 3:1-24).
2. Shetani alitumia vinywa vya wapelelezi kumi waliopeleleza nchi ya Kanaani kuwavunja moyo waisraeli, kuwadhoofisha na kuwaondolea matumaini ya kuingia nchi ya ahadi (Hesabu 13:31-33)(Hesabu 14:1-12).
3. Shetani alitumia kinywa cha mke wa Ayubu kumvunja moyo Ayubu pia alitumia vinywa vya rafiki wa Ayubu kumshambulia Ayubu (Ayubu 2:9-13)(Ayubu 16:10).
4. Shetani alimshambulia Mfalme Daudi kupitia vinywa vya watu (Zaburi 57:4)(Zaburi 140:3).
5. Shetani alitumia vinywa vya manabii waliomwasi Mungu ili kumuangamiza Mfalme Ahabu (1 Wafalme 22:19-37).
NAMNA YA KUMSHINDA SHETANI KATIKA VITA ANAYOTUMIA VINYWA VYA WATU
1. Epuka kuomba ushauri kwa kila mtu, kutendea kazi ushauri unaopewa na kila mtu.
- Biblia inasema yapo mashauri mabaya (Mithali 15:26)
Shetani hutumia watu kutoa mashauri mabaya (Ezekieli 11:2).
Hivyo basi epuka kuomba ushauri au kutendea kazi ushauri unaopewa na kila mtu, si kila mtu ana mashauri mazuri.
2. Usiwe mwepesi wa kuyaamini maneno ya watu na kuyatendea kazi bila kuyachunguza.
(Mwanzo 39:19-20) Potifa aliyaamini maneno ya mkewe bila kuyachunguza hatimaye akamuweka Yusufu gerezani, kumbuka kuwa nyumba ya Potifa ilikuwa inabarikiwa kupitia Yusufu (Mwanzo 39:2-6) kwa hiyo kumuweka Yusufu gerezani ilikuwa sawa na kufukuza baraka za Mungu ndani kwao.
Walifukuza baraka za Mungu kutokana na kinywa cha mke wa Potifa ambaye alimdanganya mumewe.
Jizoeze kuyachunguza maneno kwa njia mbalimbali ikiwemo neno la Mungu.
3. Jizoeze kupangua maneno mabaya yaliyotamkwa juu yako.
(1 Samweli 17:42-47) Goliathi alianza kufanya vita na Daudi kupitia kinywa chake, shetani alikuwa anatumia kinywa cha Goliathi kumshambulia Daudi lakini Daudi aliyapangua yale maneno kwa kutamka maneno ya ushindi na imani.
4. Epuka kusikiliza maneno yasiyotokana na Mungu na kutia moyoni kila neno ulilosikia au uliloambiwa ambalo liko kinyume na neno la Mungu.
- Maneno mengine hubeba roho fulani kwa mfano Yesu alisema maneno aliyowaambia wanafunzi wake ni roho tena ni uzima (Yohana 6:63)
Kwa hiyo ukisikia maneno ambayo hayajatoka kwenye kinywa cha Mungu yanaweza kukuingizia roho chafu.
NB: Ukizushiwa, ukisemwa vibaya, ukitukanwa usikae na hayo maneno moyoni, yapuuze ili yasikae moyoni mwako, yakikaa moyoni mwako yatakujaza uchungu, ghadhabu nakadhalika na yatakupeleka kutenda mabaya.
0 Maoni