SABABU 5 KWA NINI UWE MWOMBAJI


 SABABU YA 1: ILI USIINGIE MAJARIBUNI.

(Luka 22:40)

Yesu aliwaambia wanafunzi wake wanapaswa kuwa waombaji ili wasiingie majaribuni.

Maombi yanaweza kuzuia mtu asiingie majaribuni.

Unapaswa kufahamu kuwa ni rahisi sana kuingia majaribuni kuliko kutoka, ili utoke majaribuni ni mpaka Mungu akufanyie mlango wa kutokea.

Ilikuwa rahisi wana wa Israeli kuingia Misri lakini haikuwa rahisi kutoka Misri.

Hivyo basi hakikisha unakuwa mwombaji ili usiingie majaribuni.

SABABU YA 2: KWA KUWA UNA MAADUI.

Una maadui unaowajua na usiowajua, una maadui unaowaona na usiowaona.

Maombi yatakusaidia kuepuka mitego ya maadui, kuepuka hila zao na kukwamisha mipango yao.

(Esta 4:16) Kama wayahudi wasingeomba wangeuawa kutokana na hila ya Hamani, maombi yalisaidia kuwaepusha na mauaji yale yaliyokusudiwa juu yao.

(2 Samweli 22:4,18) Mfalme Daudi alisema maombi yalisababisha Mungu akamuokoa na maadui zake.

Kumbuka ilifika hatua hata mtoto wa Daudi aligeuka kuwa adui wa Daudi lakini maombi yalisababisha Mungu akamuokoa Daudi na maadui zake.

SABABU YA 3: KWA SABABU SHETANI ANAKUTAFUTA ILI AKUUE, AKUIBIE AU AKUHARIBU.

(1 Petro 5:8)(Yohana 10:10)

Shetani akipata nafasi huwa anaua, anaiba au anaharibu.

Maombi huzia mpenyo kwa shetani ili asipate nafasi ya kuua, kuiba au kuharibu.

SABABU YA 4: KWA KUWA HAUJUI YATAKAYOTOKEA KESHO.

(Yakobo 4:13-14) 

Watu wengi wana mipango mingi kwa ajili ya kesho lakini wengi hawajui yatakayotokea kesho.

Ikiwa haujui yatakayotokea kesho unapaswa kuwa mwombaji kwa kuwa hujui yanayoweza kutokea kesho.

SABABU YA 5: KWA SABABU MAOMBI YAKO YNAHITAJIKA SANA KWAKO BINAFSI NA KWA AJILI YA WENGINE.

Watu wengi hawajui kama maombi yao yanahitajika sana.

Msisitizo wa Yesu kwa wanafunzi wake kuhusu maombi ulionyesha kuwa maombi yanahitajika sana kwa ajili ya anayeomba na kwa ajili ya watu wengine, soma (Mathayo  26:40-43)

HITIMISHO

Ziko sababu nyingi kwa nini unapaswa kuwa mwombaji, nimekufundisha hizo sababu tano ili kuamsha shauku ya kuomba ikiwa ulikuwa haujui umuhimu wa maombi. 

Chapisha Maoni

0 Maoni