Napenda niwakumbushe ndugu zangu watanzania
"hata shetani ni kiongozi" anaongoza pepo wabaya, wachawi nakadhalika.
Shetani hutumia nguvu na vitisho ili watu wamchague yeye ila Mungu humpa mtu uhuru wa kuchagua.
Kwa hiyo "mtu yeyote anayetumia nguvu, vitisho, rushwa nakadhalika ili achaguliwe, ana tabia ya shetani" ukimchagua tarajia kuumia kwa kuwa atakuwa kiongozi lakini si kiongozi bora.
IKO HIVI: Uchaguzi ni maisha, ukichagua vibaya unajiumiza mwenyewe na unaumiza wengine na ukichagua vema unapata manufaa na unawanufaisha wengine.
Hivyo basi tunapojiandaa na uchaguzi ni vema tumuombe Mungu atupe kuona viongozi bora bila kujali vyama vyao (sisi wananchi ni wa muhimu na wa thamani kuliko chama chochote cha siasa kilichopo hapa Tanzania na kwenye hii sayari ya dunia).
Yapo mambo mengi yanayoathiri maamuzi ya uchaguzi, baadhi ya mambo yanayoathiri maamuzi ya uchaguzi ni CHUKI BINAFSI NA AKILI ZA KUPEWA.
Chuki binafsi zilisababisha wayahudi wamchague Baraba ambaye alikuwa jambazi ili kumkomoa Yesu Kristo auawe (Mathayo 27:17-26)
Wayahudi walifanya maamuzi hayo ya kumchagua Baraba kwa sababu ya akili za kupewa - walishawishiwa na wazee na wakuu wa makuhani (Mathayo 27:20)
Tunapoelekea kwenye uchaguzi tuache chuki binafsi na tuachane na akili za kupewa ili tuchague viongozi tukiwa na akili timamu.
●Kama utaona kiongozi bora yuko CCM, mchague bila kujali chama chake.
●Kama utaona kiongozi bora yuko kwenye vyama vya upinzani (CHADEMA, ACT Wazalendo, TLP nakadhalika) mchague bila kujali chama chake.
NB:
●Chuki binafsi ni jambo baya sana linaweza kukuathiri hata wewe mwenye chuki.
●Usiache kumchagua mtu kwa kuwa unachukia chama chake.
●Nchi ni yetu sote, uchaguzi ni kwa ajili ya maslahi yetu sote - tukachague viongozi bora kwa maslahi yetu sote.
0 Maoni