NAFASI YA VIONGOZI WA DINI KATIKA UCHAGUZI HURU NA WA HAKI

✍Faraja Gasto

"Nao wakuu wa makuhani na wazee wakawashawishi makutano ili wamtake Baraba, na kumwangamiza Yesu" (Mathayo 27:20).

Nitajikita kuzungumzia kundi moja tu la viongozi wa dini na nafasi yao kwenye uchaguzi.

IKO HIVI: Hakuna asiyejua viongozi wa dini ndio wana watu wanaowaongoza hivyo basi wana ushawishi mkubwa kwa watu hao wanaowaongoza.

Tunaona viongozi wa dini kwa kushirikiana na wazee waliwashawishi watu wamkatae Yesu na wamchague Baraba.

Viongozi hao wa dini walitumia ushawishi wao kuathiri maamuzi ya uchaguzi.

Tafsiri yangu, maamuzi ya uchaguzi ni utashi na uhuru wa mtu kumchagua mtu au kitu bila kuingiliwa au kushawishiwa.

Viongozi hao wa dini walitumia ushawishi wao kuingilia utashi na uhuru wa watu kuchagua mtu wamtakaye, kwa hakika uchaguzi ule haukuwa huru na wa haki.

Kisa hicho cha viongozi wa dini kinatupa picha halisi ya nafasi na nguvu ya viongozi wa dini katika jamii jinsi wanavyoweza kusababisha mambo mbalimbali kutokea kwenye jamii.

HITIMISHO

Ni vema viongozi wa dini waepuke kutumika kisiasa kwa maslahi ya vyama vya siasa, ni vema wajikite kulea jamii, kueleza ukweli, kuelimisha jamii ikiwa ni pamoja na kueleza sifa za kiongozi bora na kukemea matendo maovu katika jamii bila kujali nani ameyatenda maovu hayo kwa kuwa kiongozi wa dini sio mali ya chama fulani cha siasa japo ana uhuru wa kuwa mwanachama wa chama cha siasa anachokitaka.

Sio jambo la busara kiongozi wa dini kuwa chawa wa chama cha siasa japokuwa kiongozi wa dini anaweza kuwa mlezi au mshauri wa chama chochote cha siasa endapo chama husika kitataka.

Ni vema viongozi wa dini mjue na muweke mipaka ya nafasi zenu na ukereketwa wenu wa kisiasa ili msiathiri uchaguzi.

●Msiwaambie watu CCM ni nzuri ila vyama vingine ni vibaya, HUO NI USHETANI.

●Msiwaambie watu CCM ni mbaya ila vyama vingine ni vizuri, HUO NI USHETANI.

●Msiwaambie watu kwamba mtu wa kabila fulani hafai kuwa kiongozi, HUO NI USHETANI

●Msiwaambie watu kuwa watu wanaotoka kanda fulani hawafai kuwa viongozi, HUO NI USHETANI.

"tuache watu wamchague mtu wanayemtaka bila kuwaingilia"

 

Chapisha Maoni

0 Maoni