UKOMAVU WA KIHISIA


Faraja Gasto

Ukomavu wa kihisia ni uwezo wa kutawala hisia zako ili zisikusababishe kutenda mambo mabaya, kujitendea mabaya wewe mwenyewe au kuwatendea mabaya watu wengine.

Jaribu kufikiri wewe ni Rais wa nchi uko njiani unatembea na walinzi wako halafu ghafla anatokea mtu anaanza kukurushia mawe na mavumbi, je! utamwacha salama au utahakikisha unamshughulikia ili iwe fundisho kwa wengine?

(2 Samweli 16:1-4) Biblia inaripoti tukio la mtu fulani aliyemjia Mfalme Daudi kisha akaanza kumtukana, kumtupia mawe na mavumbi lakini Mfalme Daudi hakuhangaika na yule mtu, Mfalme Daudi alimuacha afanye anachofanya, Mfalme alikuwa na uwezo wa kumfanya chochote lakini hakufanya, HIYO NDIO MAANA HALISI YA UKOMAVU WA KIHISIA.

(Ayubu 1:13-22)Biblia inaripoti mambo yaliyotokea kwenye familia ya Ayubu, ndani ya muda mfupi Ayubu alifilisika pia watoto wake waliuawa, yalipotokea hayo Ayubu hakunywa sumu ili afe wala hakujinyonga ila alisema "Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe" HIYO NDIO MAANA HALISI YA UKOMAVU WA KIHISIA.

MAMBO YA MSINGI YATAKAYOKUSAIDIA KUPATA UKOMAVU WA KIHISIA 

1. Weka neno la Mungu kwa wingi moyoni mwako (Wakolosai 3:16)

2. Kubali Roho Mtakatifu atawale maisha yako, Biblia inasema tunda la Roho ni uvumilivu (Wagalatia 5:22) uvumilivu utakufanya kutulia mpaka wakati sahihi wa kufanya maamuzi juu ya jambo fulani, uvumilivu ni dawa mojawapo ya kutibu tatizo la kuhamaki.

3. Fahamu kuwa ulizaliwa uchi na utaondoka duniani bila kitu, kwa hiyo ukipoteza usijidhuru au kuwadhuru wengine (Ayubu 1:21)

4. Fahamu kuwa jaribu unalopitia wewe sio wa kwanza kulipitia, chochote kilichokupata wewe sio wa kwanza kupatwa na jambo hilo (1 Wakorintho 10:13), usijidhuru au kuwadhuru wengine.

5. Ukitendewa mabaya usilipe mabaya (Warumi 12:19), kulipiza kisasi ni sawa na kujifunga kamba miguu huku ukiwa na nia ya kukimbia.

HITIMISHO

Viongozi ambao hawajakomaa kihisia hutumia mamlaka zao vibaya kwa kushindana na watu, kuwakomoa watu, kuwaumiza na kuwaangamiza wapinzani wao, wakosoaji wao na watu waliowakosea.

Watu mbao hawajakomaa kihisia huwa wanawahi kuhamaki baada ya jambo au mambo fulani kutokea na wanachukua hatua wakiwa wamehamaki.

HIVYO basi hakikisha unachukua hatua za kukomaa kihisia kwa usalama na usitawi wako na kwa usalama na usitawi wa wengine.


Chapisha Maoni

0 Maoni