UTANGULIZI
Kuvuka mwaka mpya ni sawa na kuvuka barabara, kila anayetaka kuvuka barabara huwa anachukua tahadhari mbalimbali ili asidhurike na vyombo vya moto vinavyotumia barabara, baadhi ya tahadhari ambazo watu huchukua ni pamoja na kuvuka kwenye alama ya pundamilia, kuangalia kulia na kushoto kabla mtu hajavuka, kutazama kama taa za barabarani zinaruhusu mtu kuvuka nakadhalika. Vivyo hivyo kabla haujavuka kuingia mwaka mpya kuna tahadhari unapaswa kuzichukua.
BAADHI YA TAHADHARI ZA KUCHUKUA KABLA HAUJAVUKA MWAKA MPYA
· Omba Mungu akutie nguvu ili uvuke na nguvu
(2 Samweli 11:1-4) Mfalme Daudi aliingia mwaka mpya akiwa amechoka kutokana na vita za mwisho wa mwaka, kutokana na kuchoka Mfalme Daudi hakwenda vitani akabaki nyumbani, alipokuwa anatembeatembea nyumbani kwake aliona mwanamke anaoga akamtamani akalala naye hatimaye Yule mwanamke akapata mimba, kwa kuwa Yule mwanamke alikuwa mke wa mtu, Mfalme Daudi aliamua kumuua mumewe ili kujilinda.
Yote hayo yalitokea kwa kuwa Mfalme Daudi aliingia mwaka mpya akiwa amechoka kabisa, hivyo basi kama umechoka kuomba omba nguvu, kama umechoka kumtumikia Mungu omba nguvu, kama umechoka kutenda mema omba nguvu.
· Jiandae kwa vita za mwanzoni mwa mwaka kwa kujifunga silaha
Mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka huwa kuna vita za aina nyingi sana kama vile vita za kiuchumi ndio maana watu wengi husema biashara huwa haziendi vizuri mwanzoni mwa mwaka. Mwanzoni mwa mwaka au mwisho wa mwaka huwa tunashuhudia ajali nyingi sana zikitokea na zinasababisha vifo na hasara za aina mbalimbali.
(2 Samweli 11:1) Mwanzo wa mwaka palikuwa na vita lakini Mfalme Daudi hakwenda vitani kutokana na kutokwenda vitani alijikuta kwenye matatizo makubwa sana.
Hivyo basi vaa silaha za Mungu ili uzitumie kumkabili shetani na hila zake za mwanzo wa mwaka.
· Vuka ukiwa na neno au maelekezo ya Mungu kwa ajili ya mwaka mpya
Mungu hutujulisha mambo yaliyopita, yaliyopo na mambo yajayo, ukimuomba Mungu maelekezo yake atakupa kwa ajili ya mwaka mpya.
(Kutoka 12:1-32) Mungu aliwapa wana wa Israeli maelekezo yake mwanzoni mwa mwaka, maelekezo yake yaliwaepusha na vilio, wakati wamisri wanaomboleza kutokana na vifo vya wazaliwa wa kwanza, wana wa Isareli walibaki salama.
· Jizoeze kutoa sadaka kwa ajili ya mwaka mpya
(Kutoka 12:1-32) Wana wa Israeli walitoa sadaka mwanzoni mwa mwaka mpya, sadaka zile zliwaepusha na vilio, wakati wamisri wanaomboleza kutokana na vifo vya wazaliwa wa kwanza, wao walibaki salama.
0 Maoni