(LUKA 2:52)
UTANGULIZI
Mojawapo ya tatizo lililopo duniani ni watu kutojua namna ya kuishi na watu wengine, imefika hatua wengine wakasema “kuishi na watu ni kazi” wengine wakasema “mfadhili mbuzi kwa kuwa wanadamu wana maudhi” wengine wakasema “mama nipe radhi kuishi na watu ni kazi” hayo ni baadhi ya mambo yanayoonyesha suala la kuishi na watu linahitaji hekima na maarifa ya kukusaidia kuishi nao.
Tunaishi na watu wa aina mbalimbali kwenye jamii, watu wapole, watu wakali, watu wakorofi, watu wachokozi, watu wagomvi nakadhalika, pamoja na aina zote hizo za watu bado neno la Mungu linatuambia “tutafute kwa bidii kuwa na amani na watu wote”(Waebrania 12:14)
Yesu aliishi kwenye dunia hii hii lakini alimpendeza Mungu na wanadamu (Luka 2:52) maana yake ni kwamba Yesu alishii vizuri na watu. Ni ukweli usiopingika kuwa huwezi kumfurahisha kila mtu lakini neno la Mungu linatuambia tuishi vizuri na watu.
KWA NINI UISHI VIZURI NA WATU
Zipo sababu nyingi kwa nini uishi vizuri na watu lakini baadhi ya sababu ni hizi zifuatazo;-
v ●●Kuishi vizuri na watu kunaweza kukusaidia kuyapata mema ya Mungu.
(2 Wafalme 4:1-7) huyu mwanamke mjane alipewa ufunuo wa namna ya kulipa deni la mumewe aliyefariki, aliambiwa akaazime vyombo kwa majirani kisha amimine mafuta aliyonayo kwenye vyombo vile. Yule mwanamke aliazima vyombo kwa majirani zake, majirani walimpa vyombo vyao kwa kuwa aliishi vizuri na majirani zake, jaribu kufikiri kama angekuwa hana mahusiano mazuri na majirani nani angempa vyombo? Ni wazi kuwa asingepewa vyombo.
Vyombo alivyoazima vilimsaidia kubebea muujiza uliomsaidia kulipa deni la mumewe na akabaki na mtaji mkubwa.
v ●●Kwa manufaa ya watoto wako.
(2 Samweli 9:1-13) Yonathani ambaye alikuwa mtoto wa Mfalme Sauli aliishi vizuri na Daudi, ulifika wakati Sauli alikufa na Yonathani akafariki ila aliacha mtoto aitwaye Mefiboshethi. Ulipofika wakati Daudi akawa mfalme alitenda wema kwa mtoto wa Yonathani kwa kuwa Daudi na Yonathani waliishi vizuri.
NB: Hata kama una cheo kikubwa ishi vizuri na watu kwa kuwa cheo kinapita, wanadamu tunakufa, hata kama una mali ishi na watu vziuri kwa kuwa mali zinapita, ukitumia cheo chako au mali zako kuharibu maisha ya watu ukumbuke kuna wakati utavuna uliyoyapanda au watoto wako watavuna uliyoyapanda.
v ●●Maisha yako yanahitaji watu wengine.
Kwa mfano mtu akifa huwa hawezi kujizika mwenyewe, ukivamiwa na majambazi utapiga kelele watu wengine wakusaidie au wakuokoe, hiyo ni picha inayotosha kukujulisha kuwa unahitaji watu wengine kwenye maisha yako.
v ●●Kwa kuwa haujui yatakayokuwako kesho
Kuna msemo unasema “kesho ni fumbo” unapaswa kuishi na watu vizur kwa kuwa haujui mambo yatakyotokea kesho, unaweza kumtukana au kumdharau mtu leo kumbe kesho mtu huyo ni wa muhimu sana kwako.
MAMBO YA MSINGI YATAKAYOKUSAIDIA KUISHI NA WATU VIZURI
v Salimia watu
v Heshimu watu epuka kudharau watu haijalishi unawazidi elimu, cheo, mali nakadhalika.
(2 Wafalme 5:1-15) aliyemsaidia Naamani kupona ukoma ni binti wa kumsaidia mkewe kazi za ndani (house girl)
Unapaswa kuwaheshimu watu kwa kuwa haujui kesho utawakuta wapi.
v Weka neno la Mungu kwa wingi ndani yako (Wakolosai 3:16)
Neno la Mungu litakusaidia kujua namna ya kuishi na watu bila kujali hulka zao, mienendo yao nakadhalika.
v Cheo, mali, elimu nakdhalika visikufanye ukajiona unastahili kuabudiwa.
Watu wengi hujisahau sana, wanasahau mali zinapita, vyeo vinapita nakadhalika, wengine wanapopata mali, vyeo, elimu nakdhalika hutaka kuona watu wakiwaabudu.
(Esta 3:1-15, 7:10) Hamani alipandishwa cheo akaanza kuwadharau watu, baada ya siku si nyingi alitolewa kwenye cheo kile na akauawa kwenye mti aliouandaa kumuua Mordekai.
HITIMISHO
Ishi na watu vizuri kwa kuwa haujui yatakayotokea kesho, ishi na watu vizuri kwa manufaa ya watoto wako pia ishi vizuri na watu kwa faida yako mwenyewe.
0 Maoni