KUSEMEZANA

 

 


(2 Wafalme 7:3-9)

Lengo la somo: ni kukabiliana na matatizo yanayotukabili.

Vipengele vya somo

✓Kusemezana sisi kwa sisi

✓Faida za kusemezana 

Utangulizi

Yapo matatizo mbalimbali ambayo yanayowakabili watu, taasisi, nchi nakadhalika, wapo watu ambao ndoa zao hazina amani, wapo watu ambao wana msongo wa mawazo, wapo watu ambao wanakula kwa shida kutokana na hali mbaya za kiuchumi, wapo watu ambao wanasumbuliwa na magonjwa ya aina mbalimbali, wapo watu ambao wanajiuliza maswali ya aina mbalimbali na hawajui watapataje majibu ya maswali yao nakadhalika, hayo ni baadhi ya matatizo yanayowakabili watu.

Neno la Mungu ni nyenzo mojawapo ambayo Mungu amewapa wanadamu ili iwasaidie kupata ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili, mbinu mojawapo ya kibiblia au mbinu mojawapo iliyoandikwa kwenye Biblia inayoweza kuwasaidia watu kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili ni kusemezana (kuzungumza) ndio maana hata Mungu kuna wakati anataka kusemezana na watu “haya njooni tusemezane asema Bwana” (Isaya 1:18)

Kusemezana sisi kwa sisi

Nataka tutazame mifano michache kuhusu faida ya kusemezana sisi

Mfano wa 1

Biblia inatuambia palikuwa na wakoma wanne katika lango la Samaria ambao waliathirika na njaa  kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na Ben hadadi Mfalme wa shamu (2 Wafalme 6:24-29) ilifika hatua wale wakoma wakasemezana wao kwa wao kwa nini tunakaa hapa hata tufe?

Katika kusemezana kwao walihitimisha mazungumzo kwa maamuzi ya kuliendea jeshi la washami, Biblia inatuambia walipochukua hatua ya kwenda kuna jambo Mungu alitenda lililosababisha washami wakakimbia (2 Wafalme 7:6-7)

Wale wakoma walipofika kwenye kituo cha washami walipata vyakula, mavazi, dhahabu na farasi, wakoma walikula na kunywa na kusaza.

Mafanikio waliyoyapata wakoma yalitokana na kusemezana.

Mfano wa 2

(Yona 1:1-15)

Wakati Yona na wenzake wakiendelea na safari ya kwenda Tarshishi walikumbana na dhoruba kali hatimaye wakawa kwenye hatari ya kufa.

Katikati ya hatari ya kufa waliamua kusemezana wanatafuta kujua mabaya yale yamewapata kwa sababu gani, katika kusemezana kwao wakagundua kuwa mabaya yale yamewapata kwa sababu ya Yona, walipomtupa Yona baharini dhoruba ikakoma wakasafiri salama.

Faida chache za kusemezana

Kusemezana kunatuwezesha kupambanua vyanzo vya matatizo yanayotukabili

→ Kusemezana kuliwasaidia kufahamu kuwa chanzo cha tatizo linalowakabili ni Yona (Yona 1:7-15)

Kusemezana kunatuwezesha kupata suluhisho la matatizo yanayotukabili

→ Kama wangeendelea na safari bila kusemezana yamkini wangekufa kwa sababu ya Yona lakini waliposemezana wakabaini ni Yona ndiye chanzo, katika kusemezana wakapata ufumbuzi ili bahari itulie lazima wamtupe Yona baharini, Yona alipotupwa baharini bahari ikatulia.

Hitimisho

Si kila tatizo litapata ufumbuzi kwa kukemea au kwa kutoa sadaka nakadhalika, kuna matatizo mengine yatapata ufumbuzi kwa kusemezana (kuzungumza) hivyo basi lazima kanisa liwe na muda wa kusemezana (kuzungumza), lazima familia iwe na muda wa kusemezana (kuzungumza), lazima jamii iwe na muda wa kusemezana (kuzungumza) pia lazima taifa liwe na muda wa kusemezana (kuzungumza).

Chapisha Maoni

0 Maoni