Faraja Gasto ✍️✍️✍️
UTANGULIZI
Mgogoro ni hali ya kutokuelewana au kutokukubaliana.
Ulimwenguni kuna migogoro ya aina nyingi kwa mfano migogoro ya ndoa, migogoro ya kifamilia, migogoro ya ardhi, migogoro kwenye maeneo ya kazi n.k
Migogoro hiyo imekuwa ikisababisha matatizo mbalimbali ikiwemo mauaji nakadhalika.
Migogoro hiyo imekuwa ikiendelea kutegemeana na sababu mbalimbali, sababu mojawapo ni kukosekana maarifa ya kutatua migogoro hiyo.
Katika Biblia kuna mbinu nyingi sana ambazo zimetumika kutatua migogoro mbalimbali ikiwemo migogoro ya ndoa, migogoro ya kifamilia, migogoro ya ardhi n.k
Kupitia chapisho hili nitafundisha baadhi ya mbinu za kutatua migogoro.
BAADHI YA MBINU NI
1.KUTENGANA AU KUTENGANISHA AU KUJITENGA
Nataka tutazame mifano kadhaa namna mbinu hii ya kutengana au kujitenga ilivyosaidia kutatua migogoro.
(Mwanzo 13:1-12)
Kutokana na wingi wa mali walizokuwa nazo Abrahimu (Ibrahim) na Lutu ile nchi haikuwatosha hatimaye wachungaji wa mifugo yao wakaanza kugombana, Ibrahimu alishauri WATENGANE ILI KUTATUA MIGOGORO YAO. Lutu aliamua kujitenga na Ibrahimu huo ukawa mwisho wa migogoro ya wachungaji wao.
(Mwanzo 27:1-45)
Baada ya Yakobo kuchukua baraka ambazo Esau alitakiwa kuzichukua kulitokea mgogoro mkubwa sana kati ya Esau na Yakobo. Mama yao alimshauri Yakobo ajitenge akimbilie kwa mjomba wake kwa ajili ya usalama wake.
NB: Biblia inasema kisichotakiwa kutenganishwa ni kile kilichounganishwa na Mungu (mke na mume waliounganishwa na Mungu) tu (Mathayo 19:6)
2.KUPATANISHA
Biblia inasema Yesu Kristo ndiye alitupatanisha na Mungu kwa kuwa ile dhambi waliyofanya Adamu na mkewe ilisababisha Adamu na mkewe wajitenge na Mungu na sisi kama uzao wa Adamu tulitengwa na Mungu lakini Yesu alikuja kutupatanisha (1 Wakorintho 5:18-19)(Waefeso 2:16)
Biblia inatambua umuhimu wa upatanisho ndio maana neno la Mungu linasema "heri wapatanishi maana hao wataitwa Wana wa Mungu" (Mathayo 5:9)
Baadhi ya mbinu za kupatanisha
a).Kuwaleta pamoja waliohitilafiana ili kuzungumzia tofauti zao
b).Kutoa elimu, elimu ni nyenzo muhumu katika kukabiliana na matatizo mbalimbali. Mtume Yakobo aliposikia kuna mgogoro aliandika waraka wa kutoa elimu (Yakobo 4:1-10)
3.KUFUKUZA
(Mwanzo 21:10)
Kulipotokea mgogoro kati ya Sara na Hajiri, Mungu alimwambia Ibrahimu mfukuze Hajiri na mtoto wake.
(Mwanzo 3:22-24)
Mungu alipoona Adamu na mkewe wamekengeuka aliwafukuza kutoka kwenye Bustani ya Edeni.
Ni vema kufahamu kuwa kufukuza ni mbinu mojawapo ya kutatua migogoro mbalimbali.
HITIMISHO
Migogoro huwa inazaa mambo mengi mabaya ikiwemo uadui, mauaji, visasi nakadhalika hivyo basi migogoro sio mizuri.
Kunapotokea migogoro ya aina mbalimbali ni vema kuchukua hatua za kutatua migogoro hiyo kutegemeana na mbinu mbalimbali zilizomo ndani ya Biblia za kutatua migogoro.
Vipo vikwazo vingi vinavyokwamisha upatikanaji wa suluhu ya migogoro mbalimbali, vikwazo hivyo ni pamoja na baadhi ya watu kutotaka suluhu, baadhi ya watu kujihesabia haki hata kama wamekosea hawako tayari kukubali nakadhalika lakini mambo hayo hayatakiwi kutukwamisha kuchukua hatua za kutatua migogoro.
Kitu cha muhumu zaidi ya hayo yote ni kuzingatia maelekezo ya Mungu katika kutatua migogoro kwa kuwa kila mgogoro una chanzo chake na mbinu sahihi ya kuusuluhisha.
0 Maoni