Nataka tutazame mifano ya watu wawili ambao ni Daudi na Samweli.
DAUDI
Daudi alikuwa mnyenyekevu kwa kiongozi ambaye amemwasi Mungu, kiongozi ambaye alikuwa akimuwazia mabaya lakini bado akazidi kunyenyekea kwake.
Daudi alipopata nafasi ya kumuua Mfalme Sauli, bado Daudi aliendelea kunyenyekea "siwezi kumuua masihi wa Bwana" (1 Samweli 24:6). Wakati huo Daudi alikuwa ameshapakwa mafuta kuwa Mfalme lakini aliendelea kunyenyekea kwa Mfalme aliyepo madarakani.
Jaribu kufikiri unaongozwa na kiongozi mbaya, kiongozi ambaye anawaza kukuua, hafurahii kuona unainuka kiroho, kiuchumi nakadhalika UTAENDELEA KUNYENYEKEA KWAKE AU UTAANZA KUMPAKA MATOPE, UTAMTANGAZA KWAMBA HAFAI AU UTANYAMAZA?
Jaribu kufikiri unaongozwa na kiongozi mnayelingana viwango vya elimu au unamzidi, mnayelingana umri au unamzidi umri, mnayelingana hadhi mbalimbali au unamzidi JE! UTAENDELEA KUNYENYEKEA KWAKE?
ALICHOFANYA DAUDI
Daudi alipofahamu Mfalme Sauli ana mpango mbaya dhidi yake aliamua kujitenga mbali na Mfalme Sauli LAKINI HATA ALIPOJITENGA NA MFALME SAULI HAKUWAHI KUMCHAFUA MFALME SAULI KWA KUMSEMA VIBAYA KWA WATU.
Hivyo ni viwango vya unyenyekevu ambavyo watu wengi hawajavifikia.
SIKUHIZI
✓Mtu akihitilafiana na kiongozi wake basi kitakachofuata ni kuanza kumchafua kiongozi huyo kwa kumsema vibaya kwa watu, kuichafua taasisi ambayo inaongozwa na kiongozi huyo n.k.
✓Mtu akijitenga na kiongozi wake basi kitakachofuata ni kukosa nidhamu kwa kiongozi huyo.
SAMWELI
Samweli alimtumikia Mungu chini ya uongozi wa Kuhani Eli akiwa na nidhamu ya hali ya juu sana, wakati Mungu alipomuita Samweli, Samweli alimwendea Eli kwa haraka akidhani Eli ndiye anamuita (1 Samweli 3:5)
Unapoitwa na kiongozi wako huwa unakwenda kwa haraka au huwa unajishauri uende au usiende?
Samweli aliitwa na Kuhani Eli akaitika kwa unyenyekevu "mimi hapa" (1 Samweli 3:16)
Je! wewe kiongozi wako anapokuita huwa unaitika kwa jeuri au huwa unaitika kwa unyenyekevu?
Baada ya Samweli kufahamu kuwa Mungu ndiye anamuita aliitika kisha Mungu akamwambia Samweli mambo mazito kuhusu nyumba ya Eli LAKINI SAMWELI HAKUANZA KUYATANGAZA KWA WATU ALIMWAMBIA KUHANI ELI PEKE YAKE KISHA AKAKAA NAYO MOYONI (1 Samweli 3:16-18)
Je! wewe Mungu akikuambia mambo kuhusu kiongozi wako, akikufunulia siri kuhusu kiongozi wako UTATANGAZA MAMBO HAYO AU UTAKAA NAYO MOYONI NA KUZIDI KUNYENYEKEA?
HITIMISHO
Ni vema tukumbuke kuwa Mungu huwapinga wenye kiburi na huwapa neema wanyenyekevu (1 Petro 5:5)
0 Maoni