MAMBO BAADHI YATAKAYOKUSAIDIA ILI USIWE MLANGO WA IBILISI

Faraja Gasto ✍️✍️✍️✍️

WARUMI 5:12

Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.

UTANGULIZI

Biblia imeweka wazi mtu anaweza kuwa mlango wa Mungu au wa shetani kupitisha vitu mbalimbali.

MIFANO YA KIBIBLIA NAMNA MTU ANAWEZA KUWA MLANGO

✓ADAMU

 (Warumi 5:12)

Kupitia Adamu Dhambi ILIINGIA, kama dhambi iliingia basi kuna mahali iliingilia au ilipitia, Biblia imeweka wazi kuwa ADAMU ALIFANYIKA MLANGO WA KUINGIZA DHAMBI ULIMWENGUNI.

✓YESU

Wakati Yesu alipokuwa duniani alijitambulisha kama mlango (Yohana 10:7,9)

✓ZABURI 24:7,9

Malango yanaambiwa inueni vichwa, maana yake ni kwamba hawa ni watu wanaambiwa inueni vichwa kwa hiyo watu wanaweza kuwa malango.

✓WANAWAKE NI MILANGO (YOHANA 16:21)

Wanadamu wote wanaingia ulimwenguni kupitia wanawake kwa njia kuzaliwa na wanawake.

SABABU YA KUKUTAZAMISHA MIFANO

Nimekutazamisha mifano hiyo ili ufahamu kuwa sisi wanadamu ni MILANGO ambayo Mungu na shetani wanaweza kuitumia kuingiza vitu mbalimbali hapa ulimwenguni.

Kwa hiyo kila mmoja wetu anapaswa kuepuka kuwa mlango wa shetani kwa kuwa shetani anatafuta watu ambao atawatumia kama milango ya kuingiza machafuko na matengano kwenye kanisa, kuingiza machafuko na matengano kwenye familia, kuingiza machafuko na matengano kwenye taifa, kuingiza magonjwa kwenye familia au kwenye jamii, kuingiza umasikini familia, shetani anatafuta watu ambao atawatumia kama milango ya kuingiza makwazo kwenye maisha ya wengine kwenye familia au kwenye kanisa, shetani anatafuta watu ambao atawatumia kama milango ya kuwakatisha tamaa wengine nakadhalika.


BAADHI YA MAMBO YATAKAYOKUSAIDIA ILI USIWE MLANGO WA IBILISI

✓WEKA NENO LA MUNGU MOYONI NA ULITII NENO

Adamu alipoacha kutii neno la Mungu "usile tunda" yeye mwenyewe alifanyika mlango wa Ibilisi kuingiza vitu mbalimbali ulimwenguni ikiwemo dhambi, mauti, magonjwa nakadhalika.

✓JIFUNZE KUTUMIA ULIMI WAKO NA KINYWA CHAKO VIZURI KUTEGEMEANA NA NENO LA MUNGU 

(Hesabu 13:32-33, 14:1-11)

Shetani aliwatumia wapelelezi kumi kama milango ya kupitishia roho ya kutokuamini kwa wana wa Isareli.

Hao wapelelezi kumi walitumia ndimi zao kuwaletea Wana wa Israeli habari mbaya, kutokana na habari mbaya walizosikia walipoteza imani kwa Mungu aliyewatoa Misri wakaamini watafia jangwani.

HITIMISHO

Mtu yeyote asiyetii neno la Mungu ni mlango mzuri wa shetani kupitishia vitu vyake pia mtu yeyote asiyetumia kinywa chake sawasawa na neno la Mungu ni mlango wa shetani kupitishia vitu mbalimbali.


Hivyo basi kila mmoja anapaswa kuzingatia mambo hayo ili aepuke kutumiwa na shetani kama mlango wa kupitishia vitu mbalimbali.



Chapisha Maoni

0 Maoni