MAOMBI NA MAOMBEZI KAMA KIFAA CHA UOKOZI


✍️Faraja Gasto


UTANGULIZI

Hapa duniani kuna aina nyingi sana za vifaa vya uokozi (vinavyotumiwa katika kuokoa) baadhi ya vifaa hivyo ni mtungi wa kuzimia moto (fire extinguisher), boya (buoy), mitungi ya gesi ya oksijeni (oxygen gas cylinders), jaketi la maisha (life jacket) na kamba (string).


Pia katika ulimwengu wa roho kuna aina mbalimbali za vifaa vinavyotambuliwa kama vifaa vya uokozi, kifaa kimojawapo ni MAOMBI NA MAOMBEZI, nataka tutazame suala la maombi na maombezi kama kifaa cha uokozi.



MIFANO YA KIBIBLIA INAYOTUSAIDIA KUFAHAMU MAOMBI NA MAOMBEZI KAMA KIFAA CHA UOKOZI


MFANO WA 1: MAOMBEZI YANAVYOWEZA KUOKOA WAGONJWA


Biblia imeweka wazi kuwa maombezi yanaweza kumuokoa mgonjwa yakamtoa katika hali mbaya na kumleta kwenye uzima (Yakobo 5:15).


MFANO WA 2: MAOMBEZI YALIVYOPELEKEA  MTUME PETRO KUTOKA GEREZANI


Mfalme Herode alimfunga Mtume Petro kwenye gereza akiwa na nia ya kumuua lakini kanisa likafanya maombezi yale maombezi yalisababisha Mtume Petro akaokolewa kutoka kwenye gereza ambalo isingekuwa rahisi kutoka (Matendo ya mitume 12:5-16).


Kama kanisa lisingefanya maombezi Mtume Petro angeuawa kama jinsi ambavyo Mtume Yakobo alivyouawa.


MFANO WA 3: MTUME PAULO ALIVYOTAMBUA MAOMBEZI KAMA KIFAA CHA UOKOZI


Mtume Paulo alitambua siri hii kuwa maombezi ni kifaa cha uokozi ndio maana aliliandikia kanisa limuombee ili aokolewe dhidi ya watu wasioamini injili (Warumi 15:30-32).


MFANO WA 4: MAOMBEZI YALIVYOMUOKOA MALKIA ESTA ASIUAWE KWA KUKIUKA UTARATIBU WA KUINGIA MBELE YA MFALME AHASUERO


Katika ufalme wa Mfalme Ahasuero kulikuwa na taratibu nyingi, utaratibu mmojawapo ulikuwa kila anayekwenda kwa Mfalme bila kuitwa lazima auawe, aliyepaswa kwenda kwa Mfalme ni yule aliyeitwa na aliyenyooshewa fimbo ya dhahabu (Esta 3:11)


Kabla Malkia Esta hajaenda kwa Mfalme alitoa wito wa maombezi kwa ajili yake, watu wamuombee kwa muda wa siku tatu (Esta 3:15-16)


Maombezi yalisababisha Malkia Esta hakuuawa, maombezi yalimuokoa kabisa japo aliingia kwa Mfalme kinyume na utaratibu lakini hakuuawa.


MFANO WA 5: DAUDI ALIVYOOKOLEWA KUPITIA MAOMBI


Daudi alipitia mapito magumu sana ikiwemo kuwindwa ili auawe lakini maombi ndio yalipelekea akaokoka dhidi ya mipango ya waovu (Zaburi 57:1-4)


HITIMISHO

Maombi na maombezi yanaweza kumuepusha mtu na mambo mbalimbali kama vile mauti, kuaibika, kushindwa nakadhalika.


Unaweza kujiombea maombi yakakuokoa pia unaweza kuwaombea wengine maombi yakawaokoa.

Chapisha Maoni

0 Maoni