✍️ Faraja Gasto
(Mwanzo 3:1-7)
Ukisoma Biblia utagundua kuwa kuna aina nyingi sana za vita, aina mojawapo ya vita ni vita vya imani (1 Timotheo 6:12a)(2 Timotheo 4:7)
Vita vya imani vinalenga mambo makuu matatu
1. Kukufanya uiache imani (Matendo ya mitume 13:8).
2.Kukubadilishia imani ili uwe na imani isiyo sahihi (Mwanzo 3:4).
3. Kuua imani iliyo ndani yako (Yakobo 2:17).
Vita vya imani ndio vita vya kwanza alivyokutana navyo Adamu na mkewe, bahati mbaya walishindwa vita hivi (Mwanzo 3:1-7)
Mungu alipomuumba Adamu na kumuweka kwenye Bustani ya Edeni, MUNGU ALIWEKEZA IMANI ndani ya Adamu kupitia neno lake, kumbuka imani chanzo chake ni kusikia neno la Mungu (Warumi 10:17).
Mungu alimwambia "usile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya maana siku utakayokula matunda ya mti huo utakufa hakika" (Mwanzo 2:16-17).
Hilo neno lilijenga Imani ndani ya Adamu, Adamu akawa na uhakika siku atakayokula matunda ya mti huo atakufa, uhakika huo ulitokana na imani iliyokuwa ndani yake. Biblia inasema Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo ni bayana ya mambo yasiyoonekana (Waebrania 11:1).
Adamu alipoanza kuishi ma mke wake, Adamu aliwekeza Imani ndani ya mkewe, Adamu alimwambia mkewe kuwa Mungu amesema tusile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya maana tukila tutakufa Kwa hiyo mkewe Adamu akawa na imani kama ya Adamu.
Imani ndio ilisababisha wasile yale matunda maana walikuwa na uhakika kuwa siku wakila watakufa kama Mungu alivyowaambia.
SHETANI ALICHOFANYA
Shetani alikuwa anafahamu kabisa Adamu hataki kula Yale matunda kutegemeana na imani iliyokuwa ndani yake kwa hiyo akaamua kumfuata mwanamke.
Kwanza Shetani alitaka ajue kama mwanamke naye ana imani kama ya mumewe ndio maana alianza Kwa kumtega "ati hivi ndivyo alivyosema Mungu msile matunda ya miti yote ya Bustani? (Mwanzo 3:1)
Mwanamke akamjibu shetani matunda ya miti yote ya Bustani twaweza kula lakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya Mungu amesema tusiyale wala tusiyaguse tusije tukafa (Mwanzo 3:2-3).
Shetani aliposikia hilo jibu akajua huyu mwanamke ana imani kama ya mumewe ndio maana hawataki kula Yale matunda.
Palepale shetani akaanza vita ya Imani ili kumbadilishia ile imani mwanamke apate imani nyingine ndio maana shetani alimwambia mwanamke "hakika hamtakufa" (Mwanzo 3:4) yaani shetani alitaka mwanamke awe na uhakika kuwa hata wakila hawatakufa, kumbuka imani ni kuwa na hakika (Waebrania 11:1) kwa hiyo aliposema hakika hamtakufa alikuwa anampa mwanamke imani nyingine.
Bahati mbaya mwanamke akaamini akaingiwa na imani nyingine akala tunda akaenda akampa mumewe naye akala ghafla mambo yakaharibika, (imani waliyopewa na Mungu iliwazuia kula tunda wakawa salama lakini imani waliyopewa na shetani iliwafanya wakala tunda hatimaye wakaharibikiwa).
FAIDA ZA IMANI YA KWANZA WALIYOPEWA NA MUNGU
1. Imani iliwafanya wakaacha kula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya.
2.Imani iliwafanya wakaishi maisha mazuri pale Bustanini.
3.Imani Ile ilisababisha walikuwa na ujasiri wa kuwa mbele za Mungu lakini walipoingiwa na imani nyingine walimkimbia Mungu.
BAADHI YA HASARA WALIZOPATA BAADA YA KUPOKEA IMANI KUTOKA KWA IBILISI
1.Walifukuzwa kutoka kwenye Bustani ya Edeni.
Mauti iliingia duniani.
2.Matatizo mengi yakaanza kutokea duniani.
Vita ya ni vita mbaya sana kama haiko makini unaweza kujikuta umeshindwa na ukasababisha matatizo makubwa sana.
NAMNA SHETANI ANAVYOFANYA VITA VYA IMANI
Ziko njia nyingi anazotumia, baadhi ya njia hizo ni
*Kuwafanya watu wasisome neno la Mungu
*Kuwafanya watu wasinzie wakati wa kusikiliza neno la Mungu
*Kuanzisha mafundisho potofu
*Kuwafanya watu wasilitende neno la Mungu, shetani anajua kabisa usipolitenda neno lazima hiyo imani ife kwa kuwa imani bila matendo imekufa.
*Kuwafanya watu waone Mungu ni muongo, hiki ndicho shetani alichofanya pale Bustani ya Edeni, shetani alimuaminisha mwanamke kuwa Yale ambayo Mungu amewaambia ni uongo kwa kuwa Mungu anajua wakila watafanana na yeye, mwanamke akaamini uongo akala tunda.
BAADHI YA MBINU ZA NAMNA YA KUSHINDA VITA VYA IMANI
1.Usimpe Ibilisi nafasi ya kumsikiliza.
(Mwanzo 3:1-4)
Mwanamke alipompa nafasi ya kumsikiliza shetani hatimaye alijikuta ameingiwa na imani nyingine hatimaye mambo yakaharibika, kwa hiyo ili ushinde vita vya imani hakikisha haumpi Ibilisi nafasi ya kumsikiliza.
2.Msikilize Mungu na utii neno lake.
Kutii neno la Mungu ni pamoja na kulitenda hilo neno, Adamu na mkewe waliambiwa msile matunda wao wakala, hawakutii neno la Mungu.
Weka neno la Mungu kwa wingi moyoni mwako.
(Wakolosai 3:16)
0 Maoni