✍️ Faraja Gasto
UTANGULIZI
Duniani Kuna mambo mema mabaya wakati mwingine mabaya yanakuja kama mema wakati mwingine mema yanakuja kama mabaya.
Hivyo basi Kila mtu anapaswa kuwa na uwezo mkubwa wa kupambanua mema na mabaya ndio maana tunajifunza namna ya Kuongeza uwezo wa akili katika kupambanua mema na mabaya.
Biblia inaweka wazi kuwa Kuna uhusiano mkubwa wa uwezo wa akili na uwezo wa kupambanua mema na mabaya (Waebrania 5:14)
MABAYA YANAVYOKUJA KAMA MEMA
(Mwanzo 3:1-6)
Shetani alimwendea mwanamke na akaongea naye kama muungwana au anayewatakia mema lakini kumbe shetani alipanga kuwaharibu.
Shetani aliwadanganya wakila tunda watakuwa kama Mungu, huo ulikuwa uongo kwa kuwa hata kabla hawajala tunda walikuwa kama Mungu Kwa kuwa mtu aliumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Mwanzo 1:26) kwa hiyo hata kabla hawajala tunda walikuwa kama Mungu.
Shetani alikuja kama mwema lakini kumbe anapanga kuwaharibu.
(Mathayo 4:8-10)
Shetani alimwambia Yesu ukinisujudia nitakupa mali lakini Yesu alifahamu kuwa shetani hajawahi kuwa mwema, shetani alitafuta kummaliza Yesu ndio maana Yesu alipinga hoja za shetani.
Shetani alikuja kama mwema lakini kumbe alikuwa anakusudia kumuharibu Yesu.
MEMA YANAVYOKUJA KAMA MABAYA
(Mwanzo 22:1-19)
Mungu alimwambia Ibrahimu amtoe Isaka, kibinadamu jambo hilo lilikuwa baya lakini Ibrahimu aliamua kutii hatimaye Mungu alianza kumtendea Ibrahimu mema yeye na uzao wake.
Kabla ya mema kulitangulia jambo ambalo kibinadamu lilikuwa baya.
(Mwanzo 50:20)(Mwanzo 45:5,8)
Kabla mema hayajampata Yusufu, mabaya ndio yaliyotangulia halafu mema yakaja baadaye ndio maana nakuambia Kuna wakati mema yanakuja kama mabaya.
Yusufu alisema "ndugu zake walikusudia mabaya lakini Mungu alikusudia mema"
NAMNA YA KUONGEZA UWEZO WAKO WA AKILI KATIKA KUPAMBANUA MEMA NA MABAYA
1.ZINGATIA ISHARA, HALI, AU NENO AMBALO ROHO MTAKATIFU ANALOWEKA NDANI YA MOYO WAKO
Nataka tuone Roho Mtakatifu anavyoweza kutusaidia Kuongeza uwezo wetu wa kupambanua mema na mabaya
(Matendo ya mitume 5:1-5)
Roho Mtakatifu aliweka wasiwasi ndani ya Petro, Petro akapambanua kuwa Anania anadanganya Kwa hiyo Roho Mtakatifu anapoweka wasiwasi ndani yako anakuwa anakuongezea uwezo wa akili yako katika kupambanua mabaya.
(Mwanzo 27:1-23)
Yakobo alipoleta chakula ili achukue baraka za Esau, ndani ya moyo Isaka alijikuta amepata wasiwasi, akaanza kuuliza ni wewe Esau kweli, Njoo nikupapase.
Wakati mwingine Roho Mtakatifu anaweza kuweka hali fulani ndani Yako, kutoa ishara fulani au kuweka neno ndani ya moyo wako ili akili yako ikusaidie kupambanua mema na mabaya.
2. JENGA TABIA YA KUTAFAKARI
(Yona 1:6-7)
Nahodha wa boti iliyokuwa inakwenda Tarshishi aliitisha kikao ili watafakari chanzo cha mabaya yaliyowapata, walipokaa na kutafakari wakabaini mabaya yamewapata Kwa sababu ya Yona.
Kutafakari kulizisaidia akili zao kupambanua chanzo cha mabaya yaliyowapata.
3.ZINGATIA AMANI YA KRISTO INAVYOAMUA MOYONI MWAKO.
(1 Petro 3:10-11)(Wafilipi 4:7)
Biblia inataka tufahamu kuwa kuna uhusiano mkubwa wa wa AMANI, MEMA NA MABAYA. Mahali popote ambapo hakuna amani watu hutenda mabaya au hutendeana mabaya, ukiona mtu hana amani na wewe basi fahamu kuwa anaweza akakutendea mabaya.
(Yeremia 29:11)
Mungu aliwaambia waisraeli kuwa anawawazia mawazo ya amani wala si mabaya, Mungu anataka tufahamu kuwa amani inasababisha kuwaza mema au kupanga mambo mema, kama mtu ana amani na wewe basi atakuwazia mema au atapanga mambo mema kwa ajili yako.
Sasa nafikiri unaanza kuelewa Kwa nini mtu mbaya anaambiwa ATAFUTE AMANI AIFUATE SANA (1 Petro 3:10-11)
(Wafilipi 4:7)
Biblia inasema amani ya Mungu ipitayo akili zote itawahifadhi mioyo yenu na Nia zenu katika Kristo, ni kwamba amani ya Mungu inaweza kuzisaidia akili zetu kupambanua mema na mabaya ili tuamue kwa usahihi.
Hivyo basi kama unapita njia fulani halafu ghafla unajikuta umekosa amani basi zingatia amani ya Kristo inaamuaje moyoni mwako, kama unataka kwenda mahali fulani halafu ghafla ukajikuta umekosa amani basi zingatia amani ya Kristo inaamuaje moyoni mwako.
4.TENDEA KAZI USHAURI UNAOPEWA NA MUNGU KUPITIA NJIA MBALIMBALI
(Kutoka 18:8)
Kutokana na majukumu mengi aliyokuwa anayatekeleza Musa ilifika akapata shida kwenye akili, ilifika hatua akashindwa kupambanua mema na mabaya, aliona anachofanya ni chema lakini kumbe alikuwa hatendi vema.
Mungu alileta ushauri kupitia baba mkwe wake, AKAMWAMBIA JAMBO UFANYALO SI JEMA, Musa alifanya jambo lisilo jema lakini hakuweza kupambanua, Mungu aliamua kumsaidia kupitia ushauri.
Ni vema ufahamu kuwa Mungu hutoa ushauri kupitia njia mbalimbali, Mungu anaweza akatushauri kupitia watu tunaowazidi umri, hadhi nakadhalika, Mungu anaweza kushauri kupitia neno lake, watumishi wake, watu ambao hawamwamini.
Lengo mojawapo la Mungu kuwapa watu ushauri ni kuwezesha akili zao kupambanua mema na mabaya.
5.JITAHIDI UKUE KIROHO
(Waebrania 5:14)
Biblia inaweka wazi kuwa watu wazima au watu waliokua kiroho wana uwezo mkubwa wa kupambanua mema na mabaya kwa kuwa akili zao zimezoezwa kupambanua mema na mabaya.
Ninasema ujitahidi kukua kiroho kwa kuwa kukua kiroho kunategemea sana jitihada binafsi za kujifunza neno la Mungu ambalo ni chakula Cha kiroho kinachoweza kuwasaidia watu kukua kiroho.
6.KUMUOMBA MUNGU
(Yoshua 7:1-11)
Wana Israeli walijikuta wanashindwa vita, jambo hilo lilikuwa si jambo la kawaida kwa Waisraeli, kutokana na kushindwa huko Yoshua akaamua kumuomba Mungu ili amjulishe kwa nini wamepigwa vitani.
Mungu akamwambia Yoshua ni kwa sababu wana wa Israeli wametenda dhambi kwa kuwa Kuna mtu alificha baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu.
Yoshua alaipambanua chanzo cha mabaya hayo yaliyowapata baada ya kumuomba Mungu, hivyo basi ni vema ufahamu kuwa kumuomba Mungu kunazisaidia akili zetu kupambanua mema na mabaya.
KWA NINI UPAMBANUE MEMA NA MABAYA
Zipo sababu nyingi lakini nitakufundisha sababu mbili Kwa nini upambanue mema na mabaya.
1.Kwa ajili ya usalama wako
(Mwanzo 3:1-7)
Adamu na mkewe waliposhindwa kupambanua mabaya shetani aliyokusudia walijikuta kwenye hatari baada ya kula tunda, usalama wao ulitegemea utii wa kutokula tunda lakini walipokula walihatarisha usalama wao.
(Yona 1:6-7)
Hawa watu waliokuwa chomboni wasingepambanua chanzo cha mabaya wangezidi kuhatarisha maisha yao.
Hivyo basi ni muhimu sana kupambanua mema na mabaya kwa ajili ya usalama wako.
2.Kwa kuwa Mungu hafurahii tunapopatwa na mabaya.
(Yeremia 29:11)
Mawazo ya Mungu ni mema wala sio mabaya, Mungu hafurahii tunapopatwa na mabaya.
Hivyo basi kupambanua mema na mabaya itakusaidia kuepuka mabaya.
Barikiwa sana, waweza kumshirikisha mwingine.
0 Maoni