CHAKULA KAMA NJIA YA KUPITISHA NGUVU ZA MUNGU ZA KUBADILISHA UMBO LA MWILI



✍️Faraja Gasto

Ushuhuda

Sikumoja nilikuwa ninamuombea mtu fulani, nilikuwa naombea umbo lake libadilike tofauti na lilivyokuwa kwa kuwa moyoni nilijisikia kumuombea hivyo, wakati nikiendelea kumuombea, Roho wa Mungu alianza kunifundisha moyoni namna nguvu za Mungu zinavyoweza kubadili miili ya watu hususani umbo la mwili.

Kwa mfano Yesu alikufa kisha siku ya tatu akafufuka, nguvu za Mungu ndizo zilimfanya afufuke. Roho ikiondoka ndani ya mwili hata muonekano wa mwili unabadilika kabisa, kwa hiyo Yesu alipofufuka hata muonekano wa mwili wake ulibadilika (ulikuwa tofauti na ulivyokuwa wakati mwili ukiwa hauna roho).

Roho Mtakatifu alinipa kufahamu namna chakula kinavyotumiwa na Mungu kupitishia nguvu za Mungu kwa ajili ya kutenda kazi mbalimbali ikiwemo kubadili maumbo ya miili ya watu.

Mungu amekuwa akitumia chakula kufanya mambo mbalimbali kwenye maisha ya watu ikiwemo kupitishia nguvu zake kwa ajili ya kutenda kazi mbalimbali kwenye miili ya watu.

 (1 Wafalme 19:5-8)

Biblia inasema Nabii Eliya alikula chakula Kisha AKAENDA KWA NGUVU ZA CHAKULA HICHO SIKU 40 HATA AKAFIKA HOREBU MLIMA WA MUNGU.

Mungu alipitisha nguvu zake kupitia chakula alichokula Eliya ili apate nguvu za kutembea mpaka ulipokuwa mlima Horebu, zilikuwa sio nguvu za kawaida, ni nguvu za Mungu zilizoingia ndani ya Nabii Eliya kupitia chakula alichokula.

Hivyo basi kila mmoja anapaswa kufahamu kuwa chakula ni njia mojawapo ambayo Mungu anaitumia kupitishia nguvu zake kwenye mwili wa mtu ili kutenda kazi mbalimbali ikiwemo kubadili umbo au muonekano wa mwili.

Nataka tutazame mfano mmoja tu kwenye kitabu cha Danieli 1: 12-16

CHAKULA WALICHOKULA DANIELI NA WENZAKE 

(Danieli 1:12-16)

 Daniel na wenzake walikula mtama muda wa siku kumi, miili yao ilibadilika kabisa sio tu Kwa sababu ya chakula bali nguvu za Mungu zilizoingia kwenye miili yao kupitia chakula kile zilibadilisha kabisa miili yao (maumbo ya miili yao yalibadilika).

NB: Sifundishi kwamba ukila mtama umbo lako linaweza kubadilika, ninachofundisha ni habari ya nguvu za Mungu zinavyoweza kubadili umbo la mwili kupitia chakula.

Wakina Danieli walipata ufunuo wa kula mtama, na wewe omba Mungu akupe ufunuo wako ikiwa utahitaji nguvu za Mungu zishughulike na mabadiliko ya umbo la mwili wako.

HITIMISHO

Chakula kinaweza kubeba mambo mbalimbali ya kiroho kutoka kwa shetani au kwa Mungu pia chakula ni njia ya kupitishia mambo mbalimbali kutoka kwa shetani au kwa Mungu kuja kwenye mwili au maisha ya mtu, kitu kimojawapo kinachopitishwa kupitia chakula ni nguvu za Mungu zinaweza kupitia kwenye chakula na kuingia ndani ya mtu ili kutenda kazi mbalimbali ikiwemo kubadili umbo la mtu au muonekano wa mwili wa mtu.

Chapisha Maoni

0 Maoni