UJASIRI WA KUTENDA MAPENZI YA MUNGU


 ✍️Faraja Gasto

Ujasiri ni nini?

Zipo tafsiri nyingi za neno ujasiri lakini mimi nataka ufahamu hizi zifuatazo;-

1.Ujasiri ni hali ya kujiamini.

2.Kutekeleza jambo fulani bila kuwa na hofu.

Ujasiri ni kifaa cha kiroho kinachotumiwa na Mungu na shetani kutekeleza mambo mbalimbali hapa duniani, Kwa mfano ukiona mtu anaweza kujitoa muhanga akaua watu kwa kuwalipua na mabomu huo ujasiri umetoka kwa shetani,  mtu akivunja mlango wa mtu kisha akaiba fahamu kuwa ujasiri huo umetokana na shetani,  mtu akifanya mauaji nakadhalika huo ujasiri umetokana na shetani.

Ukiona mtu anahubiri injili sokoni, kwenye gari nakadhalika huo ujasiri unatoka Kwa Mungu, unapoona mtu anaweza kuitetea imani yake katika mazingira magumu huo ujasiri umetokana na Mungu kama walivyokuwa akina Shadraka, Meshaki na Abednego (Danieli 3:16-18), ukiona mtu ana ujasiri wa kukemea dhambi na maovu fahamu kuwa ujasiri huo umetoka kwa Mungu.

Mungu huwapa watu ujasiri na shetani huwapa watu ujasiri, lengo kuu ni kuwafanya watu watende mapenzi yao au watimize mapenzi yao hivyo basi hakuna awezaye kuyatenda mapenzi ya Mungu bila kuwa na ujasiri.

MIFANO YA KIBIBLIA KUHUSU UHUSIANO WA UJASIRI NA KUTEKELEZA MAPENZI YA MUNGU

MFANO WA 1: Ujasiri wa Petro na Yohana (Matendo ya mitume 4:13)

Ujasiri waliokuwa nao akina Mtume Petro na Yohana ulitokana na mapenzi ya Mungu, huu ni ujasiri Mungu aliwapa ili kutimiza mapenzi yake (kuhubiri injili).

(Matendo ya mitume 4:31)

Baada ya kanisa kumwomba Mungu mahali pale pakatikiswa, wote wakajazwa Roho Mtakatifu Kisha wakanena neno la Mungu Kwa ujasiri.

Ujasiri uliwasaisia kuyatenda mapenzi ya Mungu.

MFANO WA 2: Ujasiri wa Shadraka, Meshaki na Abednego (Danieli 3:16-18)

Ujasiri waliokuwa nao Shadraka, Meshaki na Abednego ulitokana na mapenzi ya Mungu, yaani Kuna aina ya ujasiri uliingia ndani yao walipoamua kutenda mapenzi ya Mungu (kutokuwa tayari kuabudu miungu mingine)

MFANO WA 3: Ujasiri wa kuhubiri injili (Waefeso 6:19-20)

Mtume Paulo aliwataka Waefeso wamuombee ili apewe ujasiri wa kuhubiri injili kwa kuwa hayo ndio mapenzi ya Mungu anayotakiwa kuyatenda.

UNAWEZAJE KUPATA UJASIRI

Zipo namna mbalimbali zinazofundishwa na Biblia kuhusu namna ya kupata ujasiri, mimi ninakufundisha namna mbili za kupata ujasiri;-

1.Kumwomba Mungu

(Matendo ya mitume 4:31)

Kanisa lilipomwomba Mungu mahali pale pakatikiswa wote wakajazwa Roho Mtakatifu Kisha wakanena neno la Mungu Kwa ujasiri.

(Waefeso 6:19-20)

Mtume Paulo aliwaambia Waefeso wamuombee ili Mungu ampe ujasiri, Mtume Paulo alifahamu kuwa mtu anaweza akapewa ujasiri endapo atamwomba Mungu.

2.Kuyajua mapenzi ya Mungu 

Kuyajua mapenzi ya Mungu huwa kunaleta ujasiri ndani ya mtu, jambo mojawapo lililompa Bwana Yesu ujasiri wa kufanya mambo mbalimbali alipokuwa duniani ni kuyajua mapenzi ya Mungu Baba (Yohana 4:34)

HITIMISHO

Ujasiri unaotokana na Mungu utakusababisha kufanya mambo yasiyokinzana na neno la Mungu (utakufanya utende mapenzi ya Mungu), ikitokea ukajikuta umepata ujasiri wa kutenda jambo lolote lililo kinyume na neno la Mungu basi fahamu kuwa ujasiri huo umetoka kwa shetani ili uyatende mapenzi yake.

Unahitaji ujasiri ili utimize au ili uyatende mapenzi ya Mungu. Ujasiri ulimfanya Bwana Yesu ayatende mapenzi ya Mungu Baba, Yoshua alitakiwa kuwa na ujasiri ili ayatende mapenzi ya Mungu ndio maana aliambiwa "uwe hodari na moyo wa ushujaa", Ujasiri ulimsaidia Mtume Paulo, Petro nakadhalika kuyatenda mapenzi ya Mungu.


Chapisha Maoni

0 Maoni