MWANAMKE KAMA MWEKEZAJI


✍️ Faraja Gasto

Ukisoma Biblia utagundua Mungu amempa mwanamke majukumu mbalimbali ikiwemo kuwa msaidizi wa mumewe lakini katika Biblia pia mwanamke ana jukumu la uwekezaji yaani kuwekeza vitu ndani ya mtoto au watoto.

Bahati mbaya wanawake wengi wamekuwa wakiwekeza mambo mabaya ndani ya watoto, jambo hili halimpendezi Mungu kwa kuwa Mungu anataka ndani ya watoto viwekwe vitu vyema au mambo mema.

Nataka ujifunze kupitia mifano hii michache kuhusu mwanamke kama mwekezaji.

MFANO WA 1: MAMA YAKE MUSA

 (Waebrania 11:24-25)

Biblia inasema Musa alipokuwa mtu mzima alikataa kujiita na kuitwa mtoto wa Binti Farao kwa sababu mama yake Musa alikuwa akimwambia Musa kuwa yeye sio Mmisri bali yeye ni mwebrania ndio maana Musa alikataa kuitwa mtoto wa Binti Farao.

Kilichosababisha Musa ajitambue na kuweza kufanya maamuzi sahihi ni malezi ya mama yake mzazi, mama yake aliwekeza hekima ndani ya Musa.

MFANO WA 2: MAMA YAKE MFALME LEMUELI

(Mithali 31:1-31)

Mama yake Mfalme Lemueli alimfundisha mwanaye Lemueli mambo mengi sana kama maadili kama kiongozi, miiko, masuala ya kifamilia nakadhalika.

Mama yake Lemueli aliwekeza hekima na Maarifa ndani ya mwanaye ili awe kiongozi mzuri na mume Bora katika familia yake.

MFANO WA 4: WANAWAKE WAZEE WAWEKEZE AKILI KWA WANAWAKE VIJANA

(Tito 2:3-5) 

3 Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; 

 4 ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao; 

 5 na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe. 


HITIMISHO

Epuka kuwekeza mambo mabaya ndani ya mtoto au watoto MUNGU hapendi kabisa, Wapo wanawake ambao wamewekeza mbegu za chuki Kwa watoto ili wawachukie baba zao, wasiheshimu watu fulani, Wapo wanawake wamewekeza mbegu ya kisasi ndani ya watoto, Wapo wanawake wamewekeza mbegu za ukahaba ndani ya watoto nakadhalika, UWEKEZAJI WA NAMNA HIYO HAUMPENDEZI MUNGU.

Mwanamke una wajibu wa kuwekeza hekima, akili na maarifa ndani ya watoto haijalishi ni watoto wako au wasio wa kwako.


 


Chapisha Maoni

0 Maoni