MOYO MGUMU: CHANZO CHA KUKWAMA KWA MAMBO MBALIMBALI - Seh ya 1


✍️ Faraja Gasto

Nataka nikueleze namna moyo mgumu ulivyo ili uweze kuelewa Kwa urahisi moyo mgumu ni moyo wa aina gani, Nataka tutazame baadhi ya tabia za mtu mwenye moyo mgumu

1.Kukaidi neno la Mungu.

2.Kupuuza neno la Mungu.

3.Kuwa mbishi au kubishia neno la Mungu.

4.Kutokuaminieno la Mungu.

5.Uzito au ugumu wa kutoelewa hata ukifundishwa au ukielekezwa.

Mambo mengi yanakwamishwa na mioyo migumu, ugumu wa mioyo unakwamisha mambo mengi kama vile maendeleo ya aina zote katika ngazi mbalimbali kama mtu binafsi, taifa nakadhalika, kukua kiroho, kukua kiuchumi, Usitawi wa ndoa, familia bora nakadhalika.

Soma mifano ifuatayo uone namna moyo mgumu unavyikwamisha mambo mbalimbali

MFANO WA 1: UGUMU WA MOYO WA MFALME FARAO

(Kutoka 7:3,13)

Mungu aliufanya moyo wa Mfalme Farao kuwa mgumu, kutokana na ugumu wa moyo wa Mfalme Farao wana wa Israeli walichelewa kutoka Misri, maisha ya wana wa Israeli yakawa magumu sana, ni vema uelewe kwamba Mungu aliwaambia anawapeleka kwenye nchi ya maziwa na asali yaani anawapeleka mahali ambapo watapata raha mahali ambapo maisha yao yatabadilika lakini UGUMU WA MOYO WA FARAO ULIWAKWAMISHA KWA MUDA.

Ugumu wa moyo wa Mfalme Farao ulisababisha wana wa Israeli walichelewa kutoka Misri pia nchi ya Misri ikapata mapigo ikiwemo kuuawa Kwa wazaliwa wote wa Kwanza.

NB: Kiongozi anapokuwa na moyo mgumu atakwamisha mambo mengi sana ya kimwili na ya kiroho hivyo basi usisahau kuwaombea viongozi wa taifa lako au kanisa ili wasiwe na mioyo migumu.

MFANO WA 2: UGUMU WA MIOYO YA WANANDOA 

(Mathayo 19:8)

Biblia inatueleza kuwa ugumu wa mioyo ya wanandoa unazaa vitu mbalimbali ikiwemo TALAKA.

Suala la kupeana na talaka ni matokeo ya ugumu wa mioyo, tunaendelea kushuhudia ndoa nyingi zinavunjika Kila inapoitwa Leo, watu wanaachana Kila kukicha KWA SABABU YA UGUMU WA MIOYO.

NB: Unapoombea ndoa usisahau kuombea mioyo ya wanandoa kwa kuwa chanzo kimojawapo cha kuvunjika kwa ndoa nyingi ni ugumu wa mioyo, ugumu wa mioyo unasababisha watu kutokutii neno la Mungu kuhusu suala la ndoa, wanawake kutotii waume zao, wanaume kutokupenda wake zao nakadhalika.

MFANO WA 3: UGUMU WA MIOYO KAMA SABABU YA KUENDELEA KWA UMASIKINI

(Kumbukumbu la torati 15:7-8)

Biblia inaweka wazi kuwa tunaweza kuukabili umasikini Kwa njia mbalimbali, njia mojawapo ni kuwezeshana yaani aliyefanikiwa kiuchumi amkopeshe ambaye hajafanikiwa kiuchumi ili ajikwamue kutoka kwenye umasikini, Biblia inaweka wazi kuwa KAMA UMEFANIKIWA KIUCHUMI USIUFANYE MOYO WAKO KUWA MGUMU UTAKAPOWAONA MASIKINI.

NB: Kukithiri kwa umasikini ni matokeo ya ugumu wa mioyo ya watu kwa hiyo mbinu mojawapo ya kuukabili umasikini ni kushughulikia ugumu wa mioyo.

MFANO WA 4: UGUMU WA MIOYO UNAVYOKWAMISHA MAMBO MBALIMBALI

(Waebrania 3:15)

Ukisoma Biblia utaona kwamba Mungu hutumia neno lake kushughulikia au kufanya mambo mbalimbali kama vile kuponya (Zaburi 107:20), kuokoa (Zaburi 107:20), kubadilisha maisha ya mtu au hali fulani nakadhalika.

Ugumu wa moyo husababisha watu wasipokee neno pia wasitendee kazi neno, hivyo basi kutokana na ugumu wa mioyo watu wanayakosa mema kutoka kwa Mungu (uponyaji, baraka nakadhalika) ndio maana Biblia inasema "UKISIKIA SAUTI YA MUNGU USIUFANYE MOYO WAKO KUWA MGUMU"




Chapisha Maoni

0 Maoni