✍️ Faraja Gasto
Zipo mbinu mbalimbali za kushinda ubinafsi, mbinu mojawapo ni USILAZIMISHE KUHITAJI USICHOKIHITAJI.
Kulazimisha kuhitaji usichohitaji maana yake ni kutaka uwe na vyote wewe peke yako hata kama hauvitumii au ni kutaka uwe na vitu ambavyo kiuhalisia hauvitumii. Yaani unakuwa na fedha nyingi usizozitumia, unakuwa na nguo nyingi mpaka zingine unasahau kama unazo, unakuwa na magari mengi ambayo huyatumii N.K
Ni vema ufahamu kuna wakati Mungu hutupatia vitu mbalimbali sio kwa ajili yetu wenyewe bali kwa ajili ya wengine, Mungu anapitishia mikononi mwako anataka uwape watu wengine.
USHUHUDA WANGU BINAFSI
Kuna wakati Mungu alinijalia kutumiwa nguo nikawa na nguo nyingi lakini moyoni mwangu nilikosa amani kuvaa nguo zote zile, niliamua kuchukua baadhi halafu zingine nikaziweka kwenye begi kwa muda wa miezi kadhaa hatimaye nikajisikia kuwagawia watu fulani zile nguo, nilipowagawia zile nguo nilijisikia amani moyoni.
Baada ya hapo Mungu alinifungulia milango nikaanza kubarikiwa vitu mbalimbali na watu tofautitofauti, si unajua neno la Mungu linasema "Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa" Luka 6:38
NI VEMA UFAHAMU
1. Si kila unachopata ni chako, vingine Mungu anakupa uwape wengine.
2. Ubinafsi ni kikwazo kimojapo kinachowafanya watu wasipokee baraka za Mungu.
UTAJUAJE ULICHOPATA SIO CHAKO?
Angalia amani ya Kristo inaamuaje moyoni mwako, kama unakosa amani kuvaa hizo nguo angalia amani ya Kristo inakuongoza kufanya nini, kama unakosa amani kutumia hiyo gari angalia amani ya Kristo inakuambia nini, kama unakosa amani kuvaa hivyo viatu angalia amani ya Kristo inakuongoza kufanya nini, N.K
USHUHUDA WANGU
Wakati fulani nilikuwa nina uhitaji wa fedha ili zinisaidie kutatua shida fulani, nikiwa katika kumuomba Mungu nilipata amani sana, nikajua Kuna jambo Mungu anafanya kwa ajili ya hitaji hilo.
Baada ya siku chache Mungu aligusa mtu akanipatia fedha ambazo zilinisaidia kutatua shida ile.
Ninachotaka ufahamu ni kwamba ile amani iliashiria kwamba Mungu amenijibu kwa hiyo nilipopata zile fedha nikajua ni kwa ajili ya matumizi yangu binafsi.
NB:Kulazimisha kuhitaji usichohitaji huwa kunazaa KUJILIMBIKIZIA MALI, kujilimbikizia mali ni tunda la ubinafsi na ubinafsi huwa ni kikwazo cha baraka za Mungu.
0 Maoni