UTANGULIZI
Tatizo linapotokea watu huanza kutafuta ufumbuzi wa tatizo husika kwa kutumia njia mbalimbali za kitaalamu, kimila nakadhalika.
Ukweli ni kwamba hakuna tatizo lisilokuwa na ufumbuzi ila wakati mwingine watu hukosa ufumbuzi wa tatizo kwa kutofahamu njia sahihi za kufikia ufumbuzi wa tatizo husika.
Kuna njia nyingi zinazofundishwa na Biblia zinazoweza kufanikisha kupata ufumbuzi wa matatizo, mbinu mojawapo ni KUFAHAMU HISTORIA MBALIMBALI yaani ili kufikia ufumbuzi wa tatizo fulani ni muhimu sana kufahamu historia fulani zitakazopelekea kupatikana ufumbuzi wa tatizo husika.
BAADHI YA MIFANO YA KIBIBLIA INAYOONYESHA UHUSIANO WA HISTORIA NA UFUMBUZI WA MATATIZO.
(Marko 9:21)
Akamwuliza babaye, Amepatwa na haya tangu lini? Akasema, Tangu utoto.
Kabla Yesu hajatoa pepo lililokuwa limemtesa yule mtoto, Yesu Alitaka kujua historia ya tatizo lile lilianza lini ndio maana Yesu aliuliza "amepatwa na haya tangu lini"
Ile historia ilikuwa na mchango uliopelekea kufunguliwa kwa mtoto ndio maana Bwana Yesu alitaka kufahamu historia ya tatizo lile.
(Esta 6:1-10)
Wakati kumetolewa tangazo la wayahudu kuuawa, wayahudi walimuomba Mungu awaokoe, Mungu alichofanya NI KUMUONDOLEA USINGIZI MFALME AHASUERO ILI ASOME KITABU CHA HISTORIA YA MAMBO YALIYOFANYIKA KWENYE UFALME WAKE.
Historia mojawapo aliyoiona ni historia ya Mordekai kubaini uasi uliotaka kufanywa na watumishi wawili wa ikulu ya Mfalme Ahasuero, historia ile ilipelekea Mordekai akainuliwa hadhi yake ikapanda ghafla.
Kumbuka hayo yote Mungu aliyafanya ili kurahisisha mchakato wa kuwaokoa wayahudi wasiangamizwe kwa hila ya Hamani kwa kuwa kwa nafasi Mordekai aliyopata angeweza kuuzuia mpango ule usifanikiwe.
(2 Samweli 21:1-14)
Kulikuwa na njaa muda wa miaka mitatu wakati wa utawala wa Mfalme Daudi, Mfalme na wataalamu wake walitafuta ufumbuzi kwa njia za kitaalamu lakini walikosa ufumbuzi ndipo Mfalme akaamua kumuomba Mungu kwa ajili ya tatizo husika.
Mungu alichofanya ni kumfahamisha Mfalme historia ya chanzo cha tatizo husika katika nchi yake, historia ile ndio ilipelekea kupatikana kwa ufumbuzi wa tatizo la njaa.
NAMNA YA KUPATA HISTORIA ZINAZOWEZA KUPELEKEA KUPATA UFUMBUZI WA TATIZO
1. Kuuliza watu.
Yesu alimuuliza baba yake na yule kijana mwenye pepo amueleze historia ya tatizo la kijana yule lilianza lini (Marko 9:21).
Kwa hiyo tunaweza kufahamu historia kwa kuuliza watu.
2. Kumuomba Mungu.
Mfalme Daudi alimuomba Mungu, Mungu akamjulisha historia iliyomfanya afahamu chanzo cha tatizo la njaa katika nchi yake, historia ile ilipelekea akapata ufumbuzi wa tatizo la njaa (2 Samweli 21:1-14).
Kwa hiyo tunaweza kufahamu historia kwa kumuuliza Mungu maana yeye anajua yote hata yaliyo sirini.
3. Kusoma historia.
Danieli alifahamu historia ya mambo yaliyotabiriwa na Nabii Yeremia kwa kusoma vitabu (Danieli 9:2)
Mfalme Ahasuero alifahamu historia ya yale aliyoyafanya Mordekai kwa kuwa yaliandikwa kwenye kitabu (Esta 9:1)
UMUHIMU WA KUFAHAMU HISTORIA
Historia itakupa mwanga na utafahamu wapi pa kuanzia kutatua tatizo kwa kuwa utakuwa umefahamu chanzo cha tatizo husika.
Mungu akubariki kwa hayo machache pia Mungu akusaidie kuyatendea kazi.
0 Maoni